KWA mara ya kwanza, Rais John Magufuli jana alitaja sababu zilizomfanya amteue Dk. Wilbroad Slaa kuwa Balozi.
Rais Magufuli alimteua Katibu Mkuu wa zamani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Slaa (69), kuwa Balozi Novemba 23, mwaka jana.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, siku hiyo ilisema tu kuwa Rais amefanya uteuzi huo na kwamba angeapishwa baada ya taratibu kukamilika.
Lakini akizungumza jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema alimteua Dk. Slaa kwa kuwa ni mtu anayeipenda Tanzania, kuchukia ufisadi na asiyependa majizi.
Akizungumza mara baada ya kukutana na 'kuteta' na Balozi huyo mteule, Rais Magufuli alisema sifa hizo ndizo zilimfanya amteue ili amsaidie kwenye kazi ya ubalozi.
"Kwa sifa yake ya kuipenda Tanzania, kuchukia ufisadi na kuchukia majizi, nimesema huyu atanisaidia kwenye kazi yangu ya ubalozi, ndiyo maana nimemchagua kwa moyo safi kabisa," alisema Rais Magufuli kwa mujibu wa taarifa nyingine ya Msigwa.
Rais Magufuli alisema Dk. Slaa ni mtu safi anayezungumza kutoka moyoni, mwenye kuipenda nchi ya Tanzania na anayempenda Rais, ilielezwa.
"Dk. Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija angependa kuja kuniona na nikampangia leo (jana)," alisema Rais Magufuli akinukuliwa katika taarifa hiyo ya Ikulu.
"Tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi."
Baada ya mazungumzo hayo, taarifa ilisema, ofisa mteule huyo alimshukuru Rais Magufuli kwa kumuamini na kumteua kuwa Balozi na ameahidi kuwa yupo tayari kutekeleza majukumu atakayopangiwa kwa kutanguliza maslahi ya taifa.
"Tangu (Rais Magufuli) ukiwa Waziri na tukiwa bungeni, ulifika Karatu (jimbo la Slaa wakati akiwa Mbunge), hukuweka pembeni na wakati huo niko upinzani, nadhani si kawaida, wapinzani huwa wanawekwa pembeni lakini wewe hukuniweka pembeni," alisema Dk. Slaa ambaye alikuwa Mbunge wa Karatu miaka 1995-2010.
Alijiuzulu nafasi ya ukatibu mkuu na uanachama wa Chadema mwaka 2015 baada ya chama hicho kumpokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye alipewa nafasi ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu.
Dk. Slaa ndiye alikuwa mgombea wa urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 na kushika nafasi ya pili kwa asilimia 27.05 ya kura zote halali, nyuma ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete wa CCM aliyeongoza kwa kupata asilimia 62.83.
UONGOZI BORAAidha, taarifa ya Ikulu ya jana ilisema Dk. Slaa alimpongeza Rais Magufuli kwa uongozi bora wenye maono na uthubutu wa kutekeleza mambo makubwa yenye maslahi kwa nchi ikiwemo miradi mikubwa.
Miradi hiyo ilitajwa kuwa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), ujenzi wa daraja la juu (flyover) katika makutano ya Barabara za Nyerere na Mandela (Tazara), mradi wa uzalishaji umeme katika Maporomoko ya Mto Rufiji (Stieglers' Gorge) na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
"Kwa kweli naona faraja, ninafurahi serikali ya awamu ya tano inatekeleza hatua kwa hatua karibu yote
tuliyokuwa tunayapigania kwa miaka takribani 20 ya huko nyuma," taarifa ya Ikulu ilimkariri mwanadiplomasia huyo mtarajiwa.
"Na mimi Dk. Slaa nilikuwa napiga kelele kwa sababu nilikuwa naona kuna upungufu.
"Mimi kama Dk. Slaa niliyekuwa napiga kelele, nilikuwa napiga kelele kwasababu nilikuwa naona kuna upungufu, leo nina furaha maana yale niliyokuwa napigia kelele yanatekelezwa, ninaona."
Kwa mujibu wa taarifa, Dk. Slaa alisema kikubwa ni macho na kwamba ushabiki katika maendeleo hauna tija kama ambavyo ushabiki katika siasa nao hauna tija.
"Kama nilivyowahi kueleza huko nyuma siasa ni sayansi," taarifa ilimkariri zaidi Dk. Slaa akisema na kuwa "wapo wanaofikiri siasa ni upotoshaji na siasa ni udanganyifu lakini siasa ni sayansi, na siasa kama ni sayansi ina misingi yake inayohitaji kusimamiwa.
"Na misingi yake ni nini kilikuwa ni tatizo na tatizo hilo linatatuliwa kwa misingi ipi, sasa haya tunayoyasema ni hivi, tulikuwa na tatizo la umeme, Stieglers’ Gorge inaanza kujengwa, na miradi mingine mikubwa inatekelezwa."Haya ndio mambo ya msingi.”
0 comments :
Post a Comment