Tanzania Kuingia Kwenye Orodha Ya Nchi Zisizo Na Uhuru Na Demokrasia






Ripoti mpya iliyotolewa na taasisi huru ya Freedom House imesema misingi ya demokrasia ikiwemo uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kukusanyika imeendelea kudhoofika nchini Tanzania na hali hiyo isiporekebishwa itaingia kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa duniani.

Kulingana na Freedom House ambao walichambua data katika nchi 195 za ulimwenguni katika mwaka 2017 wamebaini kuwa nchi 88 zina uhuru, 58 zimejumuishwa kwenye kundi la nchi zenye uhuru kiasi huku 48 zikiwekwa kwenye kundi la nchi zisizo na uhuru kabisa.

Tanzania imewekwa kwenye nchi 88 ambazo zina uhuru kiasi lakini inatahadharishwa kuwa inaweza kuingia kwenye nchi zisizo na uhuru kabisa. Tahadhari hiyo inatokana na mwenendo wa viongozi wa serikali kufungia vyombo vya habari, kuzuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, kushtakiwa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kwa tuhuma za uchochezi na kukamatwa kwa wapinzani wa kisiasa ambao wanakosoa na kutoa mawazo yanayotofautiana na serikali.

Pia utekelezaji wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 umekuwa ukilalamikiwa na wadau wa maendeleo kuwa ni mkakati wa kudhoofisha uhuru wa kutoa maoni, uwazi na uwajibikaji.

Tathmini hiyo iliibua mambo mbalimbali ikiwemo matumizi mabaya ya nguvu ya vyombo vya dola, matukio ya watu kutekwa na watu wasiojulikana, watu kupigwa, kujeruhiwa kwa lengo la kuharibu na kuvuruga uchaguzi na vilevile kuwatia hofu wapiga kura.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) nchini hivi karibuni kilitoa tamko la tathmini ya uchaguzi mdogo wa marudio wa kuchagua madiwani uliofanyika katika kata 43 kwenye mikoa 19 ya Tanzania Novemba 24 mwaka jana ambapo kilibaini mambo mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa misingi ya demokrasia ikiwemo uchaguzi usio huru na haki, uhuru wa kujieleza umeendelea kushuka kwa mwaka wa 12 mfufululizo duniani kote.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment