Chadema Imepewa Siku Tano Kujieleza


Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi ameipa siku tano Chadema kuwasilisha maelezo ya tuhuma za uvunjifu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na ya maadili ya vyama vya siasa kwa kufanya maandamano Februari 16.
Barua hiyo ya Februari 21 yenye kumbukumbu namba HA. 322/362/16/34 kwenda kwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, inakitaka chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuwasilisha maelezo yake kabla ya Februari 25.
“Kuwasilisha maelezo kuhusu tuhuma za uvunjifu wa sheria ya vyama vya siasa na maadili ya vyama vya siasa,” kinasema kichwa cha habari cha barua hiyo ikirejea maandamano ya chama hicho yaliyofanyika Februari 16 kutoka Mwananyamala kwenda ofisi ya msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni kumtaka awapatie viapo vya mawakala wake wa uchaguzi uliofanyika Februari 17.
Katika maandamano hayo, kuliibua vurugu baina ya polisi na waandamanaji eneo la Mkwajuni na kusababisha kifo cha mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini (22) baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala.
Barua hiyo ya Msajili inasema; “Katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za ubunge za chama chenu za uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni, uliofanyika viwanja vya Mwananyamala kwa Kopa Dar es Salaam. Inaeleza kuwa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, aliongea lugha za kuchochea vurugu ambazo zinakatazwa na Kifungu cha 9(2)(f) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 (RE: 2002) na Kanuni ya 5(1) ya Maadili ya Vyama vya Siasa (GN. 215/2007).
“Natambua tuhuma hizi pia ni za jinai na zinafanyiwa kazi na taasisi nyingine za Serikali. Hata hivyo, sanjali na hatua hizo, Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, vinanitaka nami kuchukua hatua kwa vile Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndiyo inayosimamia utekelezaji wa sheria hizo mbili,” inaeleza barua hiyo na kuongeza,
“Hivyo, kwa barua hii, nakitaka chama chenu kuwasilisha maelezo ya kwa nini kisichukuliwe hatua za kisheria, kwa kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa, kwa kuchochea wananchi kuandamana bila kufuata utaratibu wa sheria na kufanya vurugu.”
Msimamo wa Chadema
Jana, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema walipokea barua hiyo juzi na huenda wakaijibu leo huku akimtaka Msajili kutoingilia mamlaka zingine ambazo zimekwisha kuanza kulishughulikia suala hilo.
“Hoja ya Msajili anasema tumeitisha maandamano kinyume cha sheria na anasema kwa nini asituchukulie hatua. Wakati anaandika barua hiyo anajua kabisa maandamano ni haki yetu kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa na kwa mujibu wa Katiba.
“Kama maandamano yalifanyika ni suala la polisi si Msajili na kama ni jinai si kazi ya Msajili na kama anasimamia sheria mbona tulipozuiwa kufanya maandamano na mikutano ambayo ni haki yetu hakuingilia kati na kueleza sheria na Katiba inavunjwa ila hili kaliona... Ni haki yetu kuandamana asifikiri sheria imefutwa au imebadilika bado ni ileile mpaka sasa.”
Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Jaji Mutungi hakuwa tayari kulizungumzia suala hilo na kusema, “Waulize kama wameiona barua inasema nini na mimi na wao tutawasiliana sio wewe.”     

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment