MAMBO anayoyafanya winga wa vinara wa ligi kuu, Simba, Shiza Kichuya, kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayofanyika kwenye uwanja Chuo cha Bandari yamewakosha mashabiki wa timu hiyo.
Kichuya amekuwa akijituma kwenye mazoezi hayo na kuepelekea kupigiwa makofi kila anapogusa mpira na mamia ya mashabiki wanaohudhuria mazoezi hayo.
Mara baada ya kumalizika kwa mazoezi ya jana, kundi la watoto pamoja na watu wazima walimvamia Kichuya na kutaka kumbeba kumpeleka kwenye basi la timu hiyo.
Akizungumza na Nipashe, Kichuya, alisema kuwa mapenzi anayoonyeshwa na mashabiki hao yanamfanya kujituma zaidi ili asiwaangushe.
“Kwangu hii ni hamasa kubwa, hii itanifanya nijitume zaidi mazoezini ili kwenye mechi niisaidie timu yangu ipate ushindi,”alisema Kichuya.
Alisema, anajipanga kuhakikisha Simba inapata ushindi kwenye mchezo wao wa Jumapili dhidi ya Ruvu Shooting utakaochezwa kwenye uwanja wa Taifa.
Katika mzunguko wa kwanza timu hizo zilipokutana kwenye uwanja wa Uhuru, Simba waliibuka na ushindi mnono wa mabao 7-0.
0 comments :
Post a Comment