Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesema suala la maendeleo linapigwa vita sana hivyo amewataka watanzania waunge mkono hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali ili kuweza kuimarisha uchumi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo leo (Machi 09, 2018) wakati alipokuwa anafanya ufunguzi wa benki ya CRDB tawi la Chato mkoani Geita.
"Niwaombe watanzania tutangulize uzalendo kwanza, mahali popote tulipo tujue hatuna baba wala mama hii ndio Tanzania yetu tukiichafua tumechafuka wote na maneno muda mwingine huwa yanaumba. Nchi yetu inakwenda vizuri sana na mtu yeyote ukifanya vizuri watu hawakupendi. Uzuri una gharama", amesema Dkt. Magufuli.
Pamoja na hayo, Dkt. Magufuli ameendelea kwa kusema "tunapoweza kujenga reli ya kisasa (Standard Gauge) kwa Trioni 7.6 hela za ndani usifikili watu wanafurahi, tunapoweza kuamua kujenga uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto rufiji (Stieglers Gorge) tunapoweza kununua ndege 6 kitu ambacho tulikishindwa ndani ya miaka 50 usifikili wengine wanafurahi.
"Maendeleo yanachangamoto na vita kubwa ni lazima watanzania mjifunze na kuangalia mbele. Tumezungumza Tanzania ya viwanda ila zipo nchi zilizolalamika eti ni kwanini sisi tuwe na viwanda vya nguo kwa maana wanataka waendelee kutupa mitumba yao.
Kwa upande mwingine, Rais Dkt.John Magufuli kesho (Machi 10, 2018) anatarajia kufanya ziara ya siku moja mkoani Shinyanga, kukagua na kuzindua baadhi ya miradi ya maendeleo ikiwemo barabara inayounganisha Tanzania na Rwanda inayoanzia katika eneo la bandari kavu ya Isaka wilayani Kahama hadi Rusahunga mkoani Kagera.
0 comments :
Post a Comment