Kamati Kuu ya chama hicho jana Jumatano, Mach 28 ilikutana na kutoa msimamo wake ambapo walidai kuwa hawapo tayari kuendelea kuonewa.
Juzi Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na viongozi wenzake walifikishwa mahakamani na kuswekwa rumande baada ya kunyimwa dhamana,
Baadhi ya viongozi wa Chadema waliozungumza ni pamoja na Makamu mwenyekiti wa Chadema, Profesa Safari, Godbless Lema na John Mrema, ambapo mkutano huo pia ulihudhuriwa na Wajumbe wa Kamati Kuu akiwemo Edward Lowassa, Fredrick Sumaye na Meya Boniface Jacob.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Abdallah Safari alisema tukio la kunyimwa dhamana na kupelekwa rumande kwa viongozi hao ni uonevu kwani dhamana ni haki ya mtuhumiwa anapokamatwa.
“Licha yaa jitihada za mawakili wetu kuwatetea viongozi wetu lakini wamewanyima dhamana. Tumemwandikia barua Jaji Mkuu kumwambia mbona kila tunapokamatwa linapofika swala la dhamana tunakataliwa? Jaji Mkuu kajibu kirahisi sana eti kateni rufaa,” alisema Prof. Abdallah Safari.
Kwa upande wake, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema kwamba anafahamu kuwa upo mkakati wa kuwafunga Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe pamoja na viongozi wengine waliowekwa mahabusu tangu jana.
“Huo mchezo wanaotaka kufanya waendelee nao, wamewanyima dhamana ili kesi iendeshwe haraka na wawafunge kama alivyofanyiwa Sugu. Tunajua vikao vyao na nia yao. Wakitaka tusema, ukiogopa kufa utakufa.
“Sisi tutaweka mambo mengi hadharani, sina uhakika kama Mwenyekiti wetu kesho(leo) atapewa dhamana. Hapa tulipofika hatuwezi kuendelea kuishi kwa hofu. Hii vita si ya Chadema, hii ni vita ya demokrasia, Akwilina hakuwa mwanachama wa Chadema lakini aliawa, sasa nafikiri inatosha.
“Baada ya kutoka mahakamani kesho(leo) tutakutana na kuamua iwapo tufungulie maji na tuanike kila kitu kwa sababu hatuna namna. Yeyote aliyehusika tutamuanika,” alisema Lema.
0 comments :
Post a Comment