Huku kikosi cha Simba, leo hii kikitarajia kuingia kambini kujiandaa na
mechi yake ya Jumamosi dhidi ya Prisons ya jijini Mbeya, balaa jipya
limeibuka ndani ya kikosi hicho linalomhusu nahodha wa timu hiyo, Jonas
Mkude.
Baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wanadaiwa kumtaka kocha mkuu wa timu
hiyo, Mcameroon, Joseph Omog kumpokonya Mkude cheo cha unahodha wa klabu
hiyo kutokana na vitendo vyake vya utovu wa nidhamu ambavyo amekuwa
akifanya kila wakati klabuni hapo.
Wachezaji hao wamefikia hatua hiyo baada ya kutofurahishwa na kitendo
cha Mkude cha kutojiunga na timu hiyo katika safari ya kwenda mkoani
Songea kwa ajili ya mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Majimaji pasipo kuwa
na sababu zozote za msingi.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba ambazo zimedai kuwa kutokana
na hali hiyo Omog amewataka wachezaji hao kutulia na kuwahakikishia kuwa
atalifanyia kazi suala lao hilo na kwa kuanza kumpa nafasi ya kucheza
dhidi ya Prisons siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es
Salaam.
“Wachezaji wengi hawafurahii kabisa tabia ya Mkude kwani hata leo hii
(jana) katika mazoezi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha
Polisi, Kurasini ameelezwa.
“Wamemwambia kuwa hawafurahii kuendelea kuongozwa na nahodha ambaye
ndiye kinara wa utovu wa nidhamu ambaye amekuwa hana uchungu na timu na
wakamkumbishia matukio yote kama hilo kukacha kwenda Songea pasipo
sababu yoyote ya msingi lakini pia alifanya hivyo wakati tulipokuwa
tunakwenda Zanzibar katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
“Hakuambatana na timu na kuja siku iliyofuatia peke yake jambo ambalo
lilimfanya kocha ampige benchi katika mechi ya kwanza ya michuano hiyo,”
kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipotafutwa Omog ili aweze kulizungumzia suala hilo hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokelewa.


0 comments :
Post a Comment