Rais Dkt. John Pombe Magufuli amezindua ofisi na matawi mawili ya benki ya NMB Tanzania ambayo imepewa jina la Baba wa Taifa, NMB Kambarage lililopo jengo jipya la PSPF Dodoma Plaza lililopo mkoani Dodoma.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Rais Magufuli ameipongeza NMB kwa huduma bora ambazo inazitoa na kuitaka kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha kila Mtanzania anatumia benki kuhifadhi fedha kwani ni sehemu salama.
“Nikiwa kama mteja na kiongozi wa serikali huwa najisikia vizuri sana kuona benki hii inazidi kufanikiwa napenda niwahakikishe serikali itaendelea kushirikiana na NMB.
"Mkurugenzi wenu ametueleza mambo mengi ambayo mnayafanya mkiwa mmefika kila sehemu hapa nchini napenda kuwahakikishia kwamba tupo pamoja,” alisema Magufuli na kuongeza.
“Lakini Mkurugenzi kwakuwa umekubali kuchagua jina la Kambarage Nyerere yawezekana ni mbinu nzuri ya kuwavuta wateja wakaja kwa kutambua jina la Kambarage Nyerere kuwe na uwiano wa huduma zinazotolewa na vitendo vya Kambarage Nyerere, sitarajii kusikia mtu amekuja alafu akaanza kuombwa hata rushwa, wote tunajua kuwa Baba wa Taifa alikuwa mpinga rushwa.”
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker alisema benki hiyo kwa sasa imefika maeneo yote nchini na hivyo kurahisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kwamba wamejipanga kuendelea kuboresha huduma kwa kushirikiana na serikali.
“Tunafungua ofisi na matawi mapya mawili katika jengo la PSPF, NMB Kambarage inalenga kuhudumia wateja wengi ikiwepo wa kawaida na wa serikali na katika kufanikisha hili tunamshukuru Mama Maria Nyerere kwa kuturuhusu kutumia jina la mme wake ambaye ni Baba wa Taifa na Rais wa kwanza Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,
“NMB imedhamiria kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za kifedha, kwa kutumia matawi, ATM na Wakala kupitia njia ya kidigitali ya intaneti, apps na simu za mkononi. Kwa sasa NMB ina matawi 218 na zaidi ya ATM 800 nchi nzima,” alisema Bussemaker.
Aidha Bussemaker alisema pamoja na hilo pia wamekuwa wakitenga asilimia moja ya faida wanayopata kwa kila mwaka kwa ajili ya kusaidia jamii katika sekta ya afya, elimu na elimu ya fedha ambapo wamekuwa wakitoa misaada katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na uhitaji uliopo.
“Tumekuwa tukitenga asilimia moja ya faida yetu baada ya kulipa kodi kwa ajili ya Kitengo cha Masuala ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Kwa mwaka 2017 pekee tulitumia Tsh. 1.4 bilioni ambazo tulisaida shule kwa kutoa madawati 6,000, kompyuta 300 na vifaa vya maabara,” alisema Bussemaker.
Katika hafla hiyo benki ya NMB imekabidhi msaada wa Sh. 50 milioni kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma ambazo watazitumia katika shughuli za maendeleo. Hata hivyo Rais Magufuli ameshauri kuwa mradi ambao pesa hizo zitatumika upewe jina la NMB.
0 comments :
Post a Comment