Mawakili wa utetezi katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara tajiri wa madini ya tanzanite ‘Bilionea’ Erasto Msuya (43), jana walitumia saa nne na nusu kuwasilisha hoja tisa za majumuisho kwa lengo la kuonyesha mahakama kuwa wateja wao hawana hatia.
Hoja hizo zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi chini ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza shauri hilo namba 12 la mwaka 2014, zilijikita zaidi kuhoji utaratibu mzima wa ukamataji washtakiwa.
Jaji Maghimbi alianza kusikiliza hoja za upande wa utetezi jana saa 4:08 asubuhi hadi saa 7:32 mchana alipoahirisha kwa muda usikilizaji wake hadi saa 7:45.
Washtakiwa walioonekana wana kesi ya kujibu ni mshtakiwa wa kwanza Sharif Athuman (35), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, mshtakiwa wa pili Shaibu Saidi maarufu kama Mredii (42), mkazi wa Songambele, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara na mshtakiwa wa tatu Mussa Mangu (34), mkazi wa Shangarai kwa Mrefu.
Wengine ni mshtakiwa wa tano Kihundwa, mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha, mshtakiwa wa sita Sadiki Jabir a.k.a Msudani (36), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, na mshtakiwa wa saba Alli Musa maarufu Majeshi, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.
Aliyekuwa mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo iliyobaki na washtakiwa sita, Jalila Said (32) mkazi wa Babati aliachiwa huru Mei 14 baada ya Jaji Maghimbi kuona ushahidi uliotolewa dhidi yake haumgusi kiasi cha kufanya awe na kesi ya kujibu.
Msuya, aliuawa kwa kupigwa risasi 22, Agosti 7, 2013, majira ya saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando ya barabara kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
Mawasilisho ya uchambuzi wa hoja hizo yaliyofanywa na Wakili Majura Magafu katika waraka wenye kurasa 34, ulijikita zaidi kwenye uchambuzi wa mkanganyiko wa tarehe halisi za ukamataji wa watuhumiwa, utata wa tarehe za kupatikana vielelezo muhimu vya ushahidi kama bunduki aina ya SMG, pikipiki mbili zinazodaiwa kutumiwa na wauaji, maelezo yanayodaiwa ni ya kukiri kosa na ripoti ya DNA.
Hoja nyingine ni mateso ya washtakiwa, umiliki wa namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina la Motii Mongululu inayodaiwa kutumika kumvuta marehemu kwenda eneo la tukio na kama ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka ni ushahidi wa moja kwa moja au ni wa ushahidi wa kimazingira.
Akichambua hoja hizo, Wakili Magafu alidai hakuna ubishi kwamba Msuya alikufa kifo ambacho si cha kawaida cha kupigwa risasi na kuvuja damu nyingi, lakini pia hakuna ubishi kwamba shahidi pekee aliyeshuhudia mauaji hayo ni kijana wa miaka 19, Noel Thomas, mkazi wa Kijiji cha Ormelili, Wilaya ya Siha aliyekuwa akichunga mifugo lakini hakuweza kumtambua aliyefyatua risasi kumuua.
“Mheshimiwa Jaji (Maghimbi), kumekuwa na utata kuhusu ukamataji wa watuhumiwa, washtakiwa waliopo mbele yako wanasema tarehe zilizotajwa katika maelezo yao sizo tarehe walizokamatwa," alidai wakili Magafu na kueleza zaidi:
"Swali la kujiuliza ni hili je, hiyo caution statement (maelezo ya onyo) iliyokuwa admitted (pokelewa) hapa mahakamani na kusajiliwa kama Exhibit P.II (kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka namba II) kina sifa ya kuitwa confession statement (maelezo ya kukiri kosa)?
"Ni lazima confession statement iweze kukutia kwanza wewe hatiani na vile vile tunasema haiwezi kutumika kuwatia wenzako hatiani. Hakuna ushahidi uliotolewa hapa mahakamani ukionyesha Musa Mangu alihusika kununua na kuchonga laini za simu zilizotumika katika mauaji hayo zaidi ya maelezo ya wapelelezi.
"Mtu pekee ambaye angeweza kuisaidia mahakama na hakuletwa mahakamani kutoa ushahidi wake ni Adam Leyani.”
Wakili Magafu aliendelea kudai kwamba mshtakiwa wa kwanza, Mussa Mangu anadaiwa alikamatwa kati ya Agosti 11 na 13, 2013 na mkanganyiko huo umeletwa na shahidi wa 27 wa upande wa Jamhuri ambaye anakinzana na shahidi wa 18 na wote ni maofisa wa polisi.
Aidha, aliendelea kudai kuwa katika ukamataji wa bunduki upande wa mashtaka umedai kuwa ilikamatwa Septemba 11, 2013 lakini ushahidi huo huo unaonyesha kwamba watuhumiwa walikamatwa Septemba 13, 2013.
“Swali tunalojiuliza na ambalo mahakama inapaswa ilizingatie ni kwamba ni nani kati ya washtakiwa waliopo mbele ya mahakama alitumia bunduki hiyo (SMG) kumfyatulia risasi marehemu Msuya? Ushahidi huo haupo," alidai Wakili Magafu.
"We submit the gun was planted by the police (tunasema bunduki ilibambikwa na polisi) kwa sababu ilipatikana kabla ya watuhumiwa kukamatwa. Kukosekana kwa chronological events (mtiririko wa matukio) kunaacha utata.”
Aidha, wakili huyo aliyekuwa akiwasilisha hoja hizo kwa niaba ya wenzake watatu alidai kwamba hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba miongoni mwa watuhumiwa hao alikuwapo anayemiliki pikipiki aina ya King Lion na kutumia SMG hiyo kumuua Bilionea Msuya na kwamba ni jukumu la upande wa mashtaka kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka.
Wakili Magafu aliendelea kudai kuwa kwa mshtakiwa wa pili Athuman ushahidi wa Jamhuri una mkanganyiko kwa vile shahidi wa 27, Mkaguzi wa Polisi Damian Chilumba alidai alikamatwa Agosti 12, 2013 lakini shahidi wa tisa, Mkaguzi wa Polisi Samuel Maimu akaieleza mahakama kwamba alikamatwa Agosti 13 mwaka huo.
Zaidi aliendelea kudai kwamba kwa 'Mredii’ ushahidi wa shahidi wa upande wa mashtaka alidai mahakamani hapo kwamba Mredii alikamatwa Agosti 16,2013 lakini shahidi wa utetezi ambaye ni yeye Mredii alidai kwamba hakukamatwa na polisi isipokuwa aliitwa kwa wito na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mirerani na alitii na kwenda siku ya Agosti 17, 2013.
Kuhusu ushahidi wa uchunguzi wa DNA, Wakili Magafu alidai kwamba ushahidi wa shahidi wa 25 wa upande wa mashtaka, Gloria Omari (55) aliyekuwa akifanya kazi za kemia na utafiti kwenye Maabara ya Idara ya Sayansi ya Jinai ya Vinasaba katika Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali mwaka 2013, ushahidi wake hauungi mkono ushahidi wa shahidi wa 26, Kaijunga Brassy (35) ambaye alikuwa Mkemia kutoka Makao Makuu ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kaskazini.
Wakati anahitimisha uwasilisha hoja hizo, Wakili Magafu aliieleza mahakama hiyo kwamba hakuna ushahidi wa moja kwa moja katika kesi hiyo na kwamba mahakama imebaki na ushahidi mmoja ambao ni wa kimazingira.
"Mheshimiwa Jaji na waungwana wazee wa mahakama ili ushahidi wa circumstantial uweze kutumika ni matakwa ya sheria kwamba mnyororo wa ushahidi haupaswi kukatika," alidai.
"Ushahidi wa prosecution (Jamhuri) unakatika mno na ushahidi huo wa kimazingira wanaojaribu kuuleta mnyororo wake umekatika. Mahakama inastahili iwaone washtakiwa hawana hatia, prosecution wameshindwa kuthibitisha kesi yao na washtakiwa waachiwe huru."
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo ambayo ni gumzo katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini, unaongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Abdala Chavula, akisaidiwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Omari Kibwana na Wakili wa Serikali, Kassim Nassir.
Mawakili wanaounda jopo la utetezi katika kesi hiyo ni Hudson Ndusyepo anayemtetea mshtakiwa wa kwanza, Magafu anayemtetea mshtakiwa wa pili na wa tano, Emmanuel Safari anayemtetea mshtakiwa wa tatu na John Lundu anayemtetea mshtakiwa wa nne, sita na saba
0 comments :
Post a Comment