Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu aapa kujibu mashambulizi dhidi ya Wanamgambo wa Kipalestina

Majeshi ya Israel yameushambulia Ukanda wa Gaza baada ya wanamgambo wa Kipalestina kufanya mashambulizi mapya ya makombora kuelekea kusini mwa Israel.

Jeshi la Israeli limefanya mashambulizi katika Ukanda wa Gaza baada ya wanamgambo hao wa Kipalestina kurusha takriban makombora 28 ndani ya Israeli, ambayo yaliufyatua mfumo wa kinga dhidi ya silaha wa Israel wa Iron Dome.

Kundi la Hamas linalotawala katika Ukanda wa Gaza, na washirika wake wa kundi dogo la wapiganaji la Islamic Jihad wamethibitisha kwamba kambi zao za kijeshi zimeshambuliwa kwa mabomu ingawa hakuna watu walioripotiwa kujeruhiwa kwenye mashambulizi hayo ya Israel.

Mashambulizi ya  kutoka Gaza ndiyo ya kwanza kutokea tangu kuanza wimbi jipya la maandamano tarehe 30 Machi. 

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amelaani mashambulizi hayo kuilenga jamii ya Waisraeli kutokea kwenye Ukanda Gaza na amewalaumu wanamgambo wa Hamas kwa kuchochea vurugu na hali ya wasiwasi.
 
Msemaji wa jeshi la Israel Jonathan Conricus amewaambia waandishi wa habari kwamba mashambulizi hayo ya roketi na mizinga ni makubwa ukilinganisha na vita vya mwaka 2014 hali kadhalika lilivyokuwa jibu la Israeli. 

Msemaji huyo wa jeshi la Israel ameelezea kwamba wameyashambulia malengo zaidi ya 30 ya kijeshi ya mashirika ya kigaidi.

Wakati huo huo mashua iliyokuwa na wanaharakati 20 wa Kipalestina waliokuwa wakijaribu kuvunja marufuku ya miaka 11 katika pwani ya Gaza ilizuiwa na vikosi vya Israeli kwa mujibu wa mratibu wa maandamano hayo.
 
Israeli imesema kutokana na sababu za usalama inazizuia boti zote kutoka Gaza kuvuka eneo la uvuvi lililowekewa marufuku kwa umbali wa kilomita kadhaa. 

Hapo awali wavuvi wa Gaza walipigwa risasi na majeshi ya Israel kwa sababu ya kuivunja amri hiyo. Mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo, Adham Abu Selmeya, amesema manowari za kijeshi nne za Israel zilitumika kuyazuia maandamano ya mashua maili tisa kutoka pwani.

Mvutano katika Ukanda wa Gaza umefikia kiwango cha juu katika wiki za hivi karibuni. Wapalestina zaidi ya 100 waliuawa na majeshi ya Israeli wakati wa maandamano makubwa yaliyofanyika mpakani mnamo mwezi Machi.

Eneo la Ukanda wa gaza linakumbwa na hali mbaya ya kiuchumi, kutokana na uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na vita vilivyotokea mara tatu kati ya Wanamgambo wa Hamas huko Gaza na Israeli na  pia kuna ukosefu mkubwa wa bidhaa.

Credit: DW
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment