Nkupamah blog
Hatimaye marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa wameungana na wajumbe wenzao wa Baraza la Ushauri la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuanza kuwajadili makada waliojitokeza kuwania urais na kutoa ushauri utakaowezesha kupatikana kwa njia bora za kumpata mgombea wa chama hicho.
Tayari
vikao vya baraza hilo vilivyokuwa vikisubiriwa kwa hamu vimeshaanza na
leo vinaingia katika siku yake ya tatu, kwenye ofisi moja nyeti jijini
Dar es Salaam.
Taarifa
za uhakika kutoka ndani ya baraza la wazee hao zinaarifu kuwa vikao
hivyo vina umuhimu wa pekee katika mchakato huo na kwamba vimepewa eneo
tulivu na lenye usalama wa hali ya juu.
"Kikao kimeanza hapa (anataja ofisi) tangu juzi (Jumamosi) na hivi sasa bado tunaendelea,” kilieleza chanzo kimoja toka ndani ya kikao hicho.
Katika hali inayoonyesha umuhimu wa ushauri wa baraza hilo, chanzo hicho kinasema, “tuombe Mungu ili yanayoazimiwa na wazee wetu yakamilike na kuweza kukipa sura mpya chama chetu (CCM).”
Hata
hivyo, taarifa nyingine kutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa hivi sasa
baraza hilo linapewa umuhimu mkubwa kutokana na hali ya ‘mnyukano’
unaowahusisha wanasiasa wakongwe wakiwamo waliotegemewa kutoa ushauri
ili kivuke salama katika mchakato unaohusu Uchaguzi Mkuu utakaofanyika
Oktoba 25 ili hatimaye apatikane mrithi wa Rais Jakaya Kikwete kwa
nafasi ya urais na uenyekiti wa CCM.
Awali,
kikao cha wazee hao kilikuwa kifanyike Jumatano iliyopita lakini
kiliahirishwa na katibu wake, Pius Msekwa, kutokana na kile
alichokieleza kuwa ni baadhi ya wajumbe kuwa safarini.
Wazee
hao, pamoja na mambo mengine kuhusiana na uchaguzi, wanakutana kujadili
mwenendo wa mbio za urais ndani ya CCM ikiwa ni siku chache kabla ya
kufikia Julai 2, mwaka huu, ikiwa ni siku ya mwisho ya kurejesha fomu
kwa wanaowania urais kupitia chama hicho.
Hadi
kufikia jana, makada 42 wa chama hicho walijitokeza na kuchukua fomu za
kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu
utakaofanyika Oktoba 25.
Mbali
na marais wastaafu Mwinyi na Mkapa, wengine wanaounda Baraza la Ushauri
la Wazee kwa mujibu wa mabadiliko yaliyofanywa na CCM mwaka 2012 katika
katiba yake ni marais wastaafu Mwinyi (Mwenyekiti), Mkapa (Mjumbe),
Amani Abeid Karume (Mjumbe) na Dk. Salmin Amour (Mjumbe).
Wengine ni Waziri Mkuu mstaafu na Makamu wa Kwanza wa Rais, John Malecela (mjumbe) na Pius Msekwa (Katibu).
Credit: Nipashe
Credit: Nipashe
0 comments :
Post a Comment