Mratibu wa Vijana wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids), Grace
Kessy akizungumza katika warsha ya siku nne ya wawakilishi wa mashirika
ya vijana yanayojihusisha na vita dhidi ya Ukimwi nchini jijini hapa
alisema, vijana wasipobadili tabia wataendelea kuwapo hatarini.
Alisema katika taarifa zilizokusanywa mwaka 2011 hadi 2012 ilibainika
kuwa, kati ya vijana waliopimwa 40,000 walikuwa na maambukizi Dar es
Salaam, wakifuatiwa na vijana 10,000 kutoka mikoa ya Shinyanga, Kagera
na Mbeya.
“Tatizo la maambukizi ya Ukimwi ni kubwa hasa kwa vijana hivyo ni muhimu
kuwa na mikakati ya pamoja kudhibiti hali hii,” alisema.
Mbunge wa Jimbo la Arusha, Godbless Lema akifungua warsha hiyo alisema,
suala la kuendelea kuenea kwa Ukimwi ni la kimaadili kwani sasa
wanaoharibu watoto ni watu wenye uwezo, wakiwamo wabunge,
wafanyabiashara na viongozi kutokana na umaskini wa vijana.
“Taifa lina tatizo kubwa la kimaadili hivi sasa wazazi wameacha jukumu
la kulea watoto na kuachiwa wafanyakazi wa ndani, mitandao ya kijamii na
simu za mkononi,” alisema.
Alisema ili Taifa lishinde vita hiyo, ni muhimu mashirika hayo kuongeza
jitihada za kulinda maadili katika jamii, kupiga vita umaskini na
utumiaji wa pombe ovyo kwa kushirikiana na watungaji wa sera.
Awali, mratibu wa mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mtandao wa Mashirika ya
Kupambana na HIV katika Ukanda wa Afrika ya Mashariki, Jovinniah Mollel
alisema, vijana kwa sasa wapo hatarini zaidi katika vita dhidi ya
Ukimwi.
MWANANCHI
0 comments :
Post a Comment