Tuesday, July 28, 2015
@nkupamah blog
Gazeti la Mwananchi la Jumatatu, Julai 27, 2015, kwenye ukurasa wake wa 26 limechapisha habari yenye kichwa cha habari, “Marais watano wanaotajwa kuongoza kwa mishahara minono barani Afrika ni hawa hapa”.
Katika habari hiyo ambayo gazeti hilo linadai chanzo chake ni “uchambuzi
wa mtandao wa African Review” inadaiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, anashilikia nafasi ya
tano miongoni mwa viongozi 38 wa nchi za Afrika wanaolipwa mshahara
mnono zaidi.
Gazeti hilo linadai kuwa Rais Kikwete analipwa Dola za Marekani 192,000
kwa mwaka, ikiwa ni malipo ya Dola za Marekani 16,000 kwa mwezi.
Habari hizi siyo za kweli. Ni uongo na uzandiki. Ni uzushi mtupu na ni uzushi wa hatari.
Mshahara wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwezi ama kwa
mwaka haufikii na hata wala kukaribia kabisa kiwango kinachotajwa na
Gazeti la Mwananchi.
Tangu Uhuru, mwaka 1961, Rais wa Tanganyika na baadaye tangu mwaka 1964
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa miongoni mwa viongozi
wanaolipwa mishahara ya chini kabisa duniani.
Mshahara wa Rais wa Tanzania kwa mwezi ni wa chini kiasi cha kwamba
mshahara wake unazidiwa, tena kwa mbali, na mishahara wanayolipwa baadhi
ya watendaji wakuu wa baadhi ya taasisi za umma nchini.
Aidha, ni jambo la kushangaza kwamba Gazeti la Mwananchi,
linalochapishwa hapa nchini, linaweza kupata kiasi cha uongo anacholipwa
Rais wa Tanzania katika mitandao ya nje badala ya kuuliza rasmi na
kupewa majibu sahihi.
Kwa kujiingiza katika uzushi wa kupindua kiasi hiki, Gazeti la Mwananchi
haliwezi kuwa na nia nyingine yoyote isipokuwa nia ya kuwachochea
wananchi na kuwajengea chuki dhidi ya Serikali yao na Kiongozi wao Mkuu.
Ni matarajio yetu, kuwa Gazeti la Mwananchi litafanya jitihada za
makusudi, kama taaluma ya uandishi wa habari inavyoelekeza, kutafuta
usahihi wa jambo hili na kuwaambia Watanzania ukweli.
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
27 Julai, 2015
@nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment