Mkurugenzi
wa Idara ya Tathmini ya Athari ya Mazingira kutoka Baraza la Taifa la
kuhifadhi Mazingira (NEMC), Eng. Ignance Mchallo akielezea kuhusu Sheria
ya Mazingira ya mwaka 2004 kwa mafundi sanifu wa Wakala wa Ufundi na
Umeme TEMESA.
Mafundi
Sanifu wakifanya tathmini na ukaguzi wa mazingira katika karakana ya
TEMESA mjini Morogoro wakati wakiwa katika mafunzo ya tathmini,
usimamizi na ukaguzi wa mazingira.
Ofisa
Manunuzi wa Wizara ya Ujenzi, Bw. Shukuru Sikunjema akipokea cheti
kutoka kwa Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama na Mazingira kutoka
Wizara ya Ujenzi, Eng. Melania Sangeu baada ya kuhitimu mafunzo ya
tathmini, usimamizi na ukaguzi wa mazingira yaliyofanyika mkoani
Morogoro.
Mgeni
rasmi Bw. Melkizedeck Mlyapatali ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Ujenzi,
Morogoro akiwa na wahitimu wa mafunzo ya tathmini, usimamizi na ukaguzi
wa mazingira kwa mafundi sanifu wa TEMESA, kutoka mikoa mbalimbali ya
Tanzania mjini Morogoro.
Mafundi
sanifu wa Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA), kutoka mikoa mbalimbali
nchini wameaswa juu ya umuhimu wa tathmini, usimamizi na ukaguzi wa
mazingira katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kudhibiti athari za
mazingira zinazowakabili na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.
Hayo
yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Tathmini ya Athari ya Mazingira
kutoka Baraza la Taifa la kuhifadhi Mazingira (NEMC), Eng. Ignance
Mchallo wakati wa mafunzo ya tathmini na usimamizi wa mazingira kwa
mafundi sanifu yaliyofanyika mkoani Morogoro.
Aidha
amewataka mafundi hao kutumia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kwa kuwa
sheria hiyo si tu kulinda haki peke yake bali pia kuondoa vikwazo,
kutoa mwongozo wa utendaji na kupunguza mzigo wa kiutendaji, pamoja na
kuboresha uwajibikaji na ufanisi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya
nchi.
“Sheria
ya mazingira ni sheria mama ya mazingira na yenye nguvu katika
utekelezaji, na pia inaweza ikawa juu ya sheria nyingine pindi matatizo
yanapojitokeza. Ni haki kwa kila mtu kuishi katika mazingira salama na
safi, endapo mazingira yakaharibiwa unayo haki ya kuitumia sheria hii
kwa kushtaki ukiukwaji wa utunzaji wa mazingira eneo husika”,
alisisitiza Mkurugenzi Mchallo.
Mkurugenzi
Mchallo aliongezea kuwa Sheria ya mazingira inahitajika kuzingatiwa na
kutekelezwa na watu wote hususan wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi
ili kuhakikisha wanaboresha afya zao na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi
zaidi na manufaa ya Taifa kwa ujumla.
Akizungumza
katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama na
Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi, Eng. Melania Sangeu amewataka mafundi
sanifu hao kuzingatia mafunzo hayo na kutathimini mazingira katika
maeneo wanayofanyia kazi kwa kuwa lengo ni kujenga uelewa wa masuala ya
mazingira pamoja na mbinu za kufanya tathmini ya mazingira na
utekelezaji wake.
“Mazingira
salama ndiyo chachu ya ufanisi mzuri wa kazi, hivyo basi maeneo yenu ya
kazi yawe katika mazingira safi kwa kufuata utunzaji mzuri wa mazingira
unaotakiwa pamoja na kutengwa maeneo sahihi ya kumwaga mafuta machafu
ya magari, maeneo ya kuchomea taka, mpangilio mzuri wa vifaa vya
kufanyia kazi, na kuwa na vifaa vya kutosha vya usalama pamoja na
kufahamu namna na wakati wa kuvitumia”, alisema Eng. Sangeu.
Kwa
upande wake, Mhadhiri wa Taasisi ya Ufundi Dar es Salaam (DIT), Eng.
Kinyawa Kirama ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa jitihada zake za
kutambua umuhimu wa mazingira ambapo amesema kupitia mafunzo hayo
mafundi sanifu hao watakuwa mfano kwa wengine katika masuala ya
usimamizi na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao ya kazi.
“Mkirudi
katika karakana zenu mtathmini na kuangalia ni aina gani ya uharibifu
wa mazingira ambao umekuwa ukifanyika na kutafuta mbinu zakufanya ili
msiendelee kuharibu mazingira pamoja na kujikinga dhidi ya magonjwa na
matatizo yanayoweza kuibuka kutokana na ukiukwaji huo”, alisema Eng.
Kinyawa.
Ameongezea
kuwa kumekuwa na tabia ya kutokuwa makini juu ya suala la mazingira
katika maeneo yetu ya kazi na hivyo kusababisha ukiukwaji na uharibifu
wa mazingira ambao athari zake ni kubwa na nyingine kushindwa kuzuilika.
Wito
umetolewa kwa taasisi na makampuni mengine kuweka mifumo mizuri ya
kutathimini na kusimamia utunzaji wa mazingira pamoja na ushirikishwaji
kwa watu wote hasa katika sekta ya nishati ya umeme, kilimo, miundombinu
ya barabara pamoja na afya, ili kupunguza athari za mazingira
yanayopelekea mabadiliko ya tabia nchi.
0 comments :
Post a Comment