Baadhi ya wazazi wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wameonekana kutolielewa vizuri tamko la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli la kuzuia michango kwa shule za sekondari na msingi.
Wazazi hao tangu tamko hilo litolewe wamekuwa wakivamia shule mbali mbali za msingi na sekondari wakitaka kurudishiwa fedha za michango yao.
Kufuatia hali hiyo Baraza la halmashauri ya Mji wa Mbinga limeitisha kikao cha dharura kujadili changamoto hizo na namna ya kuzitatua.
Tayari Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Halmashauri hiyo, Bw. Donald Msigwa amewaagiza madiwani walijadili suala hilo kwa kina bila kupingana na agizo la Rais Magufuli.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Mhe. Egno Kipwere amesema kuwa agizo la Rais Magufuli halijahalalisha wazazi kurudishiwa fedha za michango yao ya zamani na halijafuta michango ambayo wazazi walishakubaliana kuitoa.
Rais John Magufuli alitoa tamko kupiga marufuku michango kwa shule za msingi na sekondari nchini na kuonya kuwa mtu yeyote atakayekiuka agizo hilo atachukuliwa hatua kali.
0 comments :
Post a Comment