KUSEMA MIMI NI TAJIRI WA KUTISHA NI KUNIONEA! Mpenzi msomaji wiki
iliyopita tuliendelea na simulizi hii tamu ya MJUE HUYU ambapo mhusika
mkuu ni Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) lenye makao yake makuu
Ubungo-Kibangu jijini Dar, Anthony Lusekelo maarufu kwa jina la Mzee wa
Upako.
Baada ya kusimulia historia ya maisha yake, Mzee wa Upako aliishia pale
alipokuwa akifafanua kwa nini hajiiti nabii wala mtume kisha akazama
kwenye kusimulia juu ya huduma na makanisa ya kiroho.
Makanisa kama haya ya kwetu (ya kiroho ya hapa nchini) kule Kongo (DR)
yalishaanza miaka mingi. Kenya walishaanza miaka mingi zaidi ya sisi.
Marekani kule walishaanza. Lakini sisi ndiyo kwanza tunaanza moto wa
Injili. Kwa hiyo tunapata changamoto nyingi ambazo zinatokana na uelewa
mdogo wa jamii yetu.
Wanasema makanisa mapya, imani zimekuwa nyingi. Mbona makampuni ya simu
sasa yapo mengi? Zamani tulikuwa na kampuni moja tu ya TTCL. Leo yapo
zaidi ya matatu. Tulikuwa na redio moja tu, Redio Tanzania Dar es Salaam
(RTD). Leo maredio kibao. Tulikuwa na chama kimoja tu cha CCM (Chama
Cha Mapinduzi). Leo vipo vyama vingi. Kwa hiyo wingi wa jambo si tatizo.
Hata mabaa yalikuwa machache, leo yapo mengi.
Hata bendi zilikuwa ni chache leo bendi ni nyingi kila mtaa kwa sababu
dunia inakua. Kwa sababu kuna mabaa mengi na makanisa nayo ni mengi. Ni
vizuri sasa tufungue makanisa mengi zaidi kuliko kufungua baa nyingi
zaidi.
Hivyo changamoto zote huwa nasema ukishakuwa bondia inabidi usiogope.
Mimi changamoto hizo zote naona ni kelele za mlango tu. Watu wanasema
nabii wa uongo, mara najiinua lakini kwangu ni kelele za mlango tu.
Kuhusu suala la kwamba mimi ni tajiri sana, nimezungukwa na watu wengi
wasiojiweza, kwanza mimi nasema basi sisi ni maskini sana kama hata
Lusekelo leo naonekana ni tajiri wa kutisha basi kweli sisi Watanzania
ni maskini wa kupitiliza.
Mimi naamini katika watu wanaoishi maisha ya kawaida, ninalala vizuri,
ninavaa vizuri, ni maisha ambayo kila mtu anataka kuwa nayo. Mimi ni
miongoni mwao. Ninaishi maisha ya kawaida sana tena sana. Lakini sina
fedha ya ziada. Lakini kwenye kauli hizi wanasema mwenye chongo kwenye
vipofu anaona. Kwamba, mimi nina utajiri mkubwa wa kutisha? Sidhani.
Mimi ndiyo miongoni mwa Watanzania wa kawaida sana, tena sana. Sisemi
kuhusu wahubiri wengine maana wapo. Nasema Watanzania kwa ujumla wao au
wenye hela, mimi simo.
Najua kuna Watanzania wana maghorofa, wana majumba, wana maakaunti
benki, wana maakaunti mpaka nje ya nchi. Kusema leo mimi ni miongoni mwa
matajiri wa kutisha ni kunionea. Kama vile miaka michache iliyopita
tulikuwa tunasalia darasani, hata kujenga jengo tulikuwa hatuwezi,
tulikuwa tunaazima majengo ya serikaki, tunaitwa hawa walokole maskini
hawa, ona maskini hawa. Yale mambo Mungu alikuwa anaona, ameamua kulipa
kisasi, ameamua kutubariki.
Moja, uchumi wa kila kanisa, wa msingi wa makanisa ikiwezekana makanisa
yote, nguzo kuu ya uchumi ni sadaka. Kama siyo za Walutheri wa Tanzania,
kwani mimi mwenyewe ni Mlutheri kwa asili, tena familia yetu ni ya wale
Walutheri kabisa, wale ambao huwaambii kitu kabisa. Yaani familia ya
Wamisioni.
Sasa utajiri wa makanisa ukiacha miradi ni sadaka za waumini. Dini zote
zinajengwa, zinasimama, wananunua viti, magari ya wachungaji, fedha ya
msingi ni sadaka. Kuna tofauti sana kati ya mchungaji wa kijijini ambako
kuna watu maskini, hata akiwa nao wengi sana, bado ataonekana mchungaji
wa kijijini kwa sababu uchumi wa mchungaji wa kanisa ni sadaka.
Hata ukiwa Dar es Salaam, mchungaji ambaye ana kanisa Oysterbay ni
tofauti kwa sababu wanaosali kule ni matajiri. Vilevile mchungaji
anachunga kanisa Marekani, nchi ya watu matajiri akiwa na watu 500 ni
tofauti na mchungaji anayechunga watu 500 walioko Geita, Mwanza.
Mzee wa Upako ameanza kusimulia juu ya utajiri wake.


0 comments :
Post a Comment