Wednesday, July 8, 2015
Nkupamah blog
MTIA nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Kahama kupitia Chama cha ACT Wazalendo, Clara Masanja amesema endapo atapewa ridhaa na chama hicho na kushinda nafasi hiyo, atahakikisha anawajengea wanawake ujasiri ili waweze kujipigania wenyewe katika kupata nafasi za uongozi wa juu.
Mgombea huyo, aliyasema hayo mjini hapa jana wakati alipotangaza nia
yake ya kuchukua fomu ya kugombea kiti hicho katika ofisi za chama hicho,
na kuwasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi
mbalimbali za uongozi hata kama si za kisiasa.
Masanja anayesomea shahada ya kwanza ya ufamasia katika Chuo Kikuu
cha Kampala nchini Uganda, alisema akiwa kama mwanamke ataonyesha mfano
kwa wanawake kujitokeza kuwania nafasi za uongozi, hasa katika wilaya
hiyo, ambayo haijawahi kupata mbunge mwanamke.
“Nitakapochaguliwa kuongoza jimbo hili la Kahama, nitahakikisha pia
naondoa kero mbalimbali katika Idara ya Afya,” alisema mgombea huyo
ambaye pia alikuwa mtumishi katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga katika
ngazi ya ufamasia daraja la pili.
Alisema kabla ya kuamua kugombea kiti hicho, aliona jimbo hilo lina
changamoto nyingi zilizopo katika jamii, kama vile wananchi kutopata
haki zao za msingi katika mambo mbalimbali ya kijamii.
Aidha, alisema makundi mengi ya watu hususani wazee wamekuwa hawapati
msaada wa kutosha hospitalini licha ya Serikali kutangaza matibabu kwa
wazee ni bure hali inayoweka kundi hilo katika wakati mgumu wa kupata
matibabu pindi wanapoumwa.
“Wazee wakienda Hospitali pamoja na kuambiwa matibabu ni bure,
hujikuta wakiambiwa kuwa hakuna dawa na kulazimika kununua dawa hizo
kwenye maduka ya nje yanayomilikiwa na madaktari wa hospitali husika,”
alisisitiza.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment