Saturday, July 11, 2015
Nkupamah blog
Hatimaye leo wabunge wote wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) wanakutana na viongozi wao kumchagua mgombea urais atakayeviwakilisha vyama hivyo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mkutano huo wa wabunge umekuja baada ya vikao
kufanyika mfululizo wiki hii, huku kukiwa na mvutano kuhusu nani au
chama gani kisimamishe mgombea urais.
“Tumeshakubaliana namna ya kugawana kata na
majimbo 13 yaliyobaki na Jumamosi tutaweka wazi kwa wananchi. Pamoja na
hilo pia tutamtangaza mgombea urais na chama anachotoka,” alisema Dk
Makaidi jana.
Umoja huo umekuwa ukiongezeka nguvu tangu wakati
wa mchakato wa Katiba mwaka jana, hali inayosababisha wafuasi wake
kuamini kuwa yeyote atakayesimamishwa na umoja huo na kupigiwa kampeni
kwa pamoja anaweza kujikuta anakuwa rais, mbunge au diwani.
Mvutano
Vikao vya umoja huo vilitawaliwa na mvutano baina
ya wajumbe ndani ya umoja huo hasa katika nafasi ya mgombea urais baada
ya kuwapo kwa watia nia zaidi ya mmoja.
Chanzo cha uhakika kutoka ndani ya umoja huo
kilisema kuwa isingekuwa rahisi vikao vya namna hiyo vikakosa mvutano
huo, kutokana na baadhi ya wajumbe kushindwa kukubaliana na vigezo
vilivyowekwa tangu mikutano ya awali.
Iliilazimu Kamati Kuu ya Ukawa kufanya kazi ya
ziada kuhakikisha kuwa maridhiano yanafikiwa ili kumpata mgombea, ndipo
ikaamuliwa waalikwe wabunge wote wapige kura kupata mgombea.
Taarifa zaidi zilisema kuwa wajumbe walio wengi
walikuwa wanaipa nguvu Chadema kutoa mgombea urais kutokana na nguvu
yake hasa katika mikoa ya Bara, na ukweli kwamba tayari CUF
imekwishapewa fursa hiyo Zanzibar.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam jana,
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa alisema leo vyama hivyo
vitalitangazia dunia chama kipi kitatoa mgombea wa Ukawa.
Siku chache baada ya baadhi ya wabunge kupewa adhabu ya
kutohudhuria vikao vya Bunge na Spika Anne Makinda, Jumanne ya wiki hii
Chadema ilifanya mkutano wa dharura kujadili mambo kadhaa ya kitaifa.
Siku moja baada ya kikao hicho, viongozi wa
waandamizi wa Ukawa walikutana na kujadili mambo yanayohusu umoja huo
kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Baada ya vikao hivyo, mpaka jana Chadema
iliendelea na vikao vyake vya ndani kujadili mambo kadhaa kabla ya kikao
cha Kamati Kuu ya Ukawa kinachotarajiwa kufanyika leo kupitisha mgombea
urais.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John Mnyika
licha ya kuthibitisha kuendelea kwa vikao vya ndani juzi, hakuwa tayari
kusema chochote kwa sababu ajenda bado zinajadiliwa na kwamba kesho
taarifa za uhakika zitatolewa kwa vyombo vya habari.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment