Thursday, July 2, 2015
Nkupamah blog
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru Kada wa CCM Rajabu Maranda na wenzake waliokuwa wanakabiliwa na kesi wizi wa Sh milioni 207 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jopo la mahakimu watatu likiongozwa na Hakimu John Utamwa, Ignas
Kitusi na Eva Nkya liliwaachia washitakiwa hao baada ya upande wa
Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa hao.
Mbali na Maranda washitakiwa wengine walioachiwa huru ni Farijala
Hussein na waliokuwa wafanyakazi wa BoT, Ester Komu, Bosco Kimera na
Imani Mwakosya.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Utamwa alisema washitakiwa waliokuwa
wanakabiliwa na mashitaka manne kula njama, kughushi, kuwasilisha
nyaraka za uongo BoT na wiziwa Sh milioni 207.2 wako huru kutokana na
upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka hayo bila kuacha
shaka kama inavyotakiwa kisheria.
Alisema upande wa Jamhuri umeshindwa kuithibitishia mahakama jinsi
Maranda na Farijala walighushi makubaliano ya kukusanya deni kati ya
Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni ya Rashas (T) ya
Tanzania.
Katika hukumu hiyo iliyosomwa bila Mwakosya kuwepo mahakamani, Hakimu
Utamwa alisema upande wa Jamhuri wameshindwa kumleta mpelelezi wa kesi
hiyo ili aweze kuithibitishia Mahakama saini ambazo zinadaiwa kuwepo
katika makubaliano hayo hivyo udhaifu huo hauwezi kuwatia washitakiwa
hatiani.
Aliongeza kuwa, upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha shitaka la
kughushi, kwa hiyo shitaka la kuwasilisha nyaraka za uongo litakuwa
limekufa,kwa sababu wameshindwa kuonesha kweli nyaraka ni za kughushi.
Aidha alisemwa wameshindwa kuonesha ni jinsi gani fedha hizo
zilihamishwa kama wanavyodai kuwa mchakato huo ulifanikiwa kwa sababu
Maranda na Farijala walitumia nyaraka za kughushi.
“Hakuna shahidi aliyeweza kutoa ushahidi ukaenda sawa na hati ya
mashitaka iliyofunguliwa mahakamani hapo dhidi ya washitakiwa,” alisema
Hakimu Utamwa.
Nyaraka zinazodaiwa kughushiwa ni hati za makubaliano ya kuhamishiwa
deni kutoka Kampuni ya General Marketing ya India kwenda Kampuni ya
Rashas (T) ya nchini Tanzania, ambazo walizutumia na kuiba fedha hizo.
Baada ya Hukumu hiyo, Farijala alirudishwa rumande kwa sababu
anatumikia kifungo cha miaka miwili jela alichohukumiwa katika kesi
nyingine na Maranda aliachiwa lakini bado ataendelea kwenda mahakamani
kwa kuwa anakabiliwa na kesi nyingine.
Ndugu na marafiki waliokuwepo katika eneo hilo la mahakama
walishukuru mahakama kutoa uamuzi wa haki na kusema kweli Mungu ametenda
miujiza.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment