Amir Jamal (kushoto)akifurahia jambo na Mwalimu Julius Nyerere.
Wakati ikiwa imebaki miezi miwili kwa Serikali ya awamu ya tano ambayo ni mpya kuingia madarakani, macho na masikio ya Watanzania wengi yanasubiri kushuhudia mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali.
Moja kati ya hayo likiwa muundo wa Bunge jipya ambalo ndilo ‘injini’ katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali. Kwa mujibu wa Katiba, Bunge pia hujumuisha mawaziri ambao huteuliwa kutoka miongoni mwa wabunge.
Mawaziri hao hubeba majukumu ya kufanya kazi katika sekta mbalimbali za nchi hii kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wa mawaziri, huenda matamanio ya wengi yakawa ni kufahamu ni nani atakayepewa dhamana ya kusimamia kitengo nyeti cha Hazina kupitia Wizara ya Fedha.
Wizara hiyo ambayo ndiyo ‘kibubu’ kinachobeba jukumu zito la kutoa gawio kwa ajili ya matumizi ya kila sekta ya nchi hii, ambazo hugusa maisha wa wananchi kwa namna moja au nyingine. Lakini wakati shauku na ‘sintofahamu’ hiyo ikiwa bado imetawala miongoni mwa Watanzania wengi, ni vyema kuwafahamu mawaziri waliowahi kupewa dhamana ya kusimamia wizara hiyo nyeti kabla na mara baada ya kupata uhuru, hasa wakati huu Taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa tano wa vyama vingi, tangu mfumo huo uliporejeshwa mwaka 1992.
Mwaka mmoja kabla ya Tanzania kupata uhuru, 1960 kabla iliyokuwa Tanganyika, sasa Tanzania Bara haijaungana na Zanzibar, Wizara ya Fedha ilikuwa chini ya Mwingereza, Sir Ernest Vassey.
Vassey alisimamia wizara hiyo kwa mwaka mmoja, hadi 1961 na mapema baada ya kupata uhuru, wizara hiyo ilikabidhiwa kwa wazawa chini ya utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Paul Bomani ambaye sasa ni marehemu, aliteuliwa kushika wadhifa huo na kuwa Waziri wa Fedha wa kwanza mwafrika. Alikaa kwenye nafasi hiyo kwa miaka mitatu, kuanzia 1962 hadi 1965.
Mwaka mmoja baada ya Tanganyika kuungana na Zanzibar, Amir Jamal aliteuliwa kuwa waziri wa pili wa fedha na kutumikia nafasi hiyo kwa miaka sita, kuanzia 1966 hadi 1972.
Baada hapo, Cleopa Msuya alipewa jukumu la kusimamia wizara hiyo kwa mwaka mmoja.
Msuya ambaye sasa ni Waziri Mkuu mstaafu, alifuatiwa tena na Jamal. Awamu hii alikaa madarakani kwa mwaka mmoja tu.
Mwaka uliofuata, Edwin Mtei aliteuliwa kusimamia wizara hiyo kwa miaka minne, kuanzia 1978 hadi 1981.
Kutokana na utumishi wake uliotukuka, Jamal ambaye sasa ni marehemu, alipewa tena jukumu la kusimamia wizara hiyo kwa mara ya tatu.
Kwa kuteuliwa mara tatu kuongoza wizara hiyo, Jamal anaweza kutajwa kuwa amevunja rekodi kwa kuongoza wizara hiyo kwa miaka 10 kwa vipindi tofauti chini ya utawala wa Mwalimu Nyerere.
Ilipobaki miaka miwili kabla ya Mwalimu Nyerere kung’atuka katika urais mwaka 1985, alimteua Profesa Kighoma Malima kuwa Waziri wa Fedha naye alitumikia nafasi hiyo kwa miaka miwili.
Profesa Malima ambaye sasa ni marehemu, alifikisha idadi ya mawaziri watano, walioteuliwa na Mwalimu Nyerere kushika jukumu la kusamamia Wizara ya Fedha kwa kipindi alichoongoza nchi.
Idadi hiyo inakaribia kulingana na ya mawaziri wa fedha waliobalidishwa kwa vipindi tofauti chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye anakaribia kumaliza muhula wake wa pili na kukamilisha miaka 10 ya kukaa madarakani.
Awamu ya pili
Rais Ali Hassan Mwinyi aliyepokea kijiti kutoka kwa Mwalimu Nyerere, baada ya kuingia madarakani, alimteua Msuya kuwa Waziri wa Fedha akishika nafasi hiyo kwa mara ya pili.
Akiwa chini ya Serikali ya awamu ya pili, Msuya alishika wadhifa huo kwa miaka mitatu, kuanzia 1986 hadi 1989.
Msuya ambaye anakumbukwa kwa kauli yake ya “Kila mtu atabeba msalaba wake,” aliyowahi kutoa akiwa bungeni, alimkabidhi ofisi, Steven Kibona.
Ikumbukwe kuwa wakati Msuya anatoa kauli hiyo ambayo aliwahi pia kunukuliwa akisema haijutii, Taifa lilikuwa katika wakati mgumu kuichumi.
Lakini hata baada ya Kibona, ambaye sasa ni marehemu kupewa dhamana na kuongoza wizara hiyo nyeti bado hali haikuwa shwari.
Baada ya miaka mitatu (1990 hadi 1993) Profesa Malima aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Fedha kwa mwaka mmoja.
Rais Kikwete, aliteuliwa na Mwinyi kuwa Waziri wa Fedha kwa mwaka mmoja, akipokea ofisi kutoka kwa Profesa Malima.
Mwaka 1995 wakati Kikwete akiwa Waziri wa Fedha, Tanzania ilikuwa kwenye kipindi kama cha sasa kuelekea uchaguzi, ambako aliingia kwenye kinyang’anyoro hicho cha kuwania kiti cha urais, lakini kura hazikutosha.
Awamu ya Tatu
Rais Benjamin Mkapa, ambaye kura zake zilitosha na kuibuka mshindi wa nafasi hiyo, uteuzi wa Wazira wa Fedha ulimwangukia Profesa Simon Mbilinyi.
Alishika wadhfa huo kwa mwaka mmoja kabla ya Daniel Yona kuteuliwa kwa nafasi hiyo aliyodumu nayo kati ya mwaka 1997 hadi 2000.
Yona ambaye sasa anatumikia kifungo kutoka na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka, alifuatiwa na Basil Mramba aliyeteuliwa pia na Mkapa kuongoza wizara hiyo.
Mramba ambaye pia anatumikia kifungo baada ya kuhukumiwa pamoja na Yona kwa matumizi mabaya ya madaraka, aliitumikia nafasi hiyo kwa miaka minne.
Mawaziri hao watatu wa fedha ndiyo pekee walioteuliwa na Rais Mkapa kusimamia wizara ya fedha.
Idadi hiyo inafanya Serikali ya awamu ya tatu kuwa na mawaziri wachache katika wizara hiyo kwa kipindi cha miaka 10, Rais Mkapa alipokuwa madarakani.
Wanawake
Uongozi wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Kikwete, ulifungua pazia la uteuzi wa mawaziri wa fedha wanawake. Tofauti na Serikali za awamu zilizopita, Wizara ya Fedha haikuwahi kuwa na waziri mwanamke.
Katika uteuzi wake wa Baraza la Mawaziri baada tu ya kuingia Ikulu, Rais Kikwete alimteua Zhakia Meghji kuwa Waziri wa Fedha.
Meghji alitumika nafasi hiyo kwa miaka miwili na baadaye Rais Kikwete alimteua Mustafa Mkulo kuwakatika wizara hiyo. Alifanya kazi kwenye ofisi hiyo kwa miaka minne, kuanzia 2007 hadi 2012.
Dk William Mgimwa ambaye ni marehemu, aliteuliwa kumrithi. Alifariki dunia akiwa bado waziri. Baada ya kifo chake, pengo lake lilizibwa na aliyekuwa naibu wake, Saada Mkuya ambaye anashikilia wadhifa huo hadi sasa na bila shaka atahitimisha utawala wa awamu ya nne katika historia ya wizara hiyo.
Mkuya ambaye ni mwanamke wa pili kushika nafasi hiyo nyeti kati ya mawiziri 15 waliyowahi kushika nafasi hiyo tangu uhuru, amewahi kukaririwa akisema kuwa wadhifa huo si jambo dogo. Ni wadhifa wenye changatomo lukuki, hasa ikizingatiwa hali ya uchumi wa nchi.
Pia, alisema inakuwa ngumu kupanga bajeti kwenye nchi kama Tanzania ambayo matumizi ni makubwa kuliko mapato.
Vigogo hao ndiyo waliosimamia sera na uchumi wa Taifa katika miaka 54 tangu uhuru, kila mmoja akiwa na mazuri pia changamoto zake kiutendaji.
Swali linalobaki ni je, nani atapokea kijiti cha kuongoza wizara hiyo ambayo ni kama ‘kibubu’ cha Taifa?
Je, uteuzi utamwangukia mwanamke au mwanamume?
Bila shaka jibu litapatikana baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 ambapo mshindi wa uraisi atapata fursa ya kuunda Serikali kwa kuteua Baraza la Mawaziri.
0 comments :
Post a Comment