Leo nimekuja na mada hii; UNAPIGIWA SIMU HUPOKEI, UNASONYA...UNATUMA MESEJI...MPENZI WAKO AKUELEWE VIPI?
Mada hii inawahusu wapendanao wote. Wewe mwanamke na wewe mwanaume. Nimefuatilia kwa makini sana suala lenyewe na kubaini kwamba, ni la kweli na limekuwa likiwakera wengi.
ISHU ILIVYO
Utakuta mtu amekaa na mpenzi wake. Mara simu yake ya mkononi inaita. Mpenzi huyo anaiangalia. Badala ya kupokea, anasonya. Halafu baada ya simu kukatika, anatuma meseji tena anaandika kwa kasi halafu anaiweka simu mezani na kuendelea na mazungumzo.Hivi, kama kweli wewe una moyo kama mpenzi uliyekaa naye. Unadhani anawaza nini? Au jiulize ukifanyiwa wewe hivyo utawaza nini?
WANAVYOSEMA WADAU
Nilibahatika kuzungumza na baadhi ya wadau wangu kuhusu tabia hiyo ambapo wengi walisema kuwa, tafsiri ya tukio hilo ni kwamba, aliyepiga simu ni mpenzi mwingine. Kwa sababu amekaa na mpenzi mwingine anaogopa kupokea ndiyo maana anaamua kutuma meseji.
Hilo ni kweli! Hata mimi ikinitokea nitawaza hivyohivyo. Kama umekaa na mwenza wako mahali, simu yako ikaita, pokea. Na kama ni kimeo kwa maana ya mtu anayekudai basi muoneshe simu mpenzi wako huku ukimwambia anayepiga ni nani!
“Da! Baby, huyu jamaa anayepiga ananidai. Hivyo sipokei simu yake, lakini nitampigia baadaye.” Ukifanya hivyo utakuwa unamweka mwenza wako katika mazingira mazuri ya kukuamini.
KINACHOWAZWA
Madhara ya kuidumisha tabia hii ya kutopokea simu na baadaye kutuma meseji huku ukiwa humwambii chochote mwenza wako ni kumpa maswali mengi ambapo mwisho wa yote, majibu yanakuwa kwamba, ‘ulishindwa kupokea simu kwa sababu aliyepiga ni mchepuko wako’.
MADHARA YAKE
Madhara ya tabia hiyo sasa...kama utampata mwenza ambaye hapendi kuulizauliza naye atajikuta akiamua kutafuta mwingine wa pembeni.Kama ni wanandoa, mara nyingi kununiana kunaanzia hapo. Ukijaribu kusema hivi ili acheke, unashangaa yeye ameuma midomo kumbe moyoni anauliza kimyakimya, ‘huyo aliyepiga simu kama ni mwema kwa nini hukupokea badala yake umesubiri simu imekatika halafu umetuma meseji?’
USHAURI WANGU
Kama kweli wasomaji wangu mnapenda kuelimika, ninachotaka kuwaambia hapa ni kwamba. Maisha ya wawili wapendanao si sinema wala maigizo. Ni kazi hasa, tena nzito.Ukitaka kujenga penzi lako siku zote liwe na amani, hakikisha unatumia muda mwingi kuwa muwazi kwa mwenzako.
Upo kazini, simu yako imeisha chaja, tafuta namna wasiliana na aliye nyumbani. Umekaa baa ya Mchelechele mwambie mwenzako nipo baa ya Mchelechele. Utakuta mtu anapigiwa simu akiwa amekaa na mwenza wake sebuleni, anasimama mbio kwenda kuzungumzia chumbani. Anaongea weee! Akirudi, anakaa na kuendelea na mazungumzo bila kusema chochote. Hii si tabia yenye uwazi.
Lazima mwenzako atajiuliza ni simu yenye umuhimu wa kiasi gani mpaka imekufanya ukaongelee mbali? Na je, huyo uliyekuwa ukiongea naye, yeye hatakiwi kumjua? Kama anatakiwa kumjua, mbona sasa humtaji badala yake unashika mazungumzo yale ya awali?
Naomba jamani mjirekebishe. Ni mambo madogo kwako lakini ni makubwa kwa mwenza wako. Tukutane wiki ijayo.
GPL
0 comments :
Post a Comment