Wednesday, August 26, 2015
@nkupamah blog
Chama
cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), kimekata rufaa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), kwa majimbo ya Mlalo, Bumbuli, Ludewa na Peramiho
yaliyotangazwa kuwa wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wamepita bila
kupingwa kwa madai kuwa waliotangaza hawana mamlaka hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Wakili wa Chadema, Peter Kibatala alisema tayari utaratibu wa kuandaa rufaa hizo umeshakamilika.
“Ninasimamia
rufaa ya kesi tatu. Tunapinga wakurugenzi wa halmashauri kutangaza
majimbo yao kuwa yana wagombea waliopita bila kupingwa wakati sheria
haiwaruhusu kufanya hivyo.
“NEC pekee ndiyo wanaweza kusema lolote baada ya kusikiliza kilichoamuliwa na mkurugenzi,” alisema Kibatala.
Taarifa
zilizopo zinaonyesha kuwa wagombea watano wa ubunge kupitia CCM
wamepita bila kupingwa baada ya wawakilishi wa vyama vya upinzani
kushindwa kujitokeza au kuwekewa pingamizi kutokana na makosa kadhaa ya
kikanuni.
Mgombea
wa Chadema Jimbo la Bumbuli, David Chanyezhea alisema baada ya kupokea
barua ya kuenguliwa na mkurugenzi wa uchaguzi wilayani kwa maelezo kuwa
amekosa vigezo, amekata rufaa NEC kupinga uamuzi huo.
Chanyezhea
alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya jitihada za kumtaka ajiondoe
kwenye kinyang’anyiro hicho na wapambe wa mgombea mwenzake wa chama
kingine.
“Nimeshaandika
barua ya kukata rufaa na kuituma NEC. Ninaamini haki itatendeka kwani
sheria inaruhusu mtu kugombea udiwani na ubunge kwa wakati mmoja na wapo
wabunge wa namna hiyo kwenye mabunge yaliyopita,” alidai mgombea huyo.
Hata
hivyo, Wakili Kibatala alisema kutokana na makosa hayo, ana imani kuwa
NEC itakuwa makini na kutoa majibu sahihi dhidi ya rufaa hizo.
Alipoulizwa
kuhusu mustakabali wa majimbo mawili yaliyosalia, Kaimu Katibu Mkuu wa
Chadema, Salum Mwalimu alisema tayari hatua zimeshachukuliwa kwa lile la
Peramiho na la Nanyamba.
Mwalimu alisema hawawezi kulizungumzia Jimbo la Nanyamba kwa kuwa mgombea aliyesimamishwa alikuwa wa CUF.
“Huko
kwingine yalikuwa masuala ya kiufundi pekee ndiyo yaliyoleta
changamoto, lakini hali imekuwa ya kushangaza kidogo… mgombea
hakurudisha fomu,” alisema Mwalimu.
Taarifa
kutoka kwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo
zilieleza kuwa kuna harufu ya rushwa kwenye jimbo la Nanyamba ambako
mgombea wa chama hicho hakurejesha fomu na kumfanya yule wa CCM kukosa
mpinzani.
0 comments :
Post a Comment