Wednesday, August 26, 2015
@nkupamah blog
MUUNGANO wa wapiga kura Tanzania (TANVU), umeiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumchukulia hatua, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kwa kitendo alichokifanya kuvitukana vyama vya upinzani kwa kuwaita viongozi na wanachama wake malofa, vibaka na wapumbavu.
Kauli
ya TANVU inakuja ikiwa ni siku chache baada ya Mkapa kutoa maneno ya
kuvihadaa vyama vya upinzani wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) kilipokuwa
kinazindua kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika kwenye viwanja vya
Jangwani, Dar es Salaam.
Pia
muungano huo umekipatia CCM muda wa siku saba kuanzia leo kuwaomba
radhi watanzania kwa kutumia Shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu
nchini (SHIVYAWATA) kwenye uzinduzi wa kampeni hizo huku kikitambua ni
makosa kisheria kwa vyama vya siasa kutumia Taasisi zisizokuwa za
serikali kwenye kampeni za uchaguzi.
Kauli
hiyo ya TANVU imetolewa leo jijini Mwanza na Rais wake, Militon
Lutabanana wakati akizungumza na wandishi juu ya hali ya kisiasa nchini,
demokrasia na kuelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Amesema
hatua ya SHIVYAWATA kushiriki kwenye uzinduzi wa kampeni za kisiasa za
CCM ni makosa kwa kuwa kwa mujibu wa sheria za nchi taasisi yoyote isiyo
ya serikali hairuhusiwi kujiingiza kwenye shughuli za kisiasa.
“Kwa
kitendo hicho wote wanamakosa CCM na SHIVYAWATA lakini kama CCM
haitaomba radhi tutatoa tamko lingine ambalo sisi kama muungano wa
wapiga kura nchini hatupendi tufike huko,” amesema na kuongeza.
“Tunaiomba
Tume ya Taifa ya Uchaguzi itende haki kwa kumchukulia hatua stahiki
Rais Mkapa kama ambavyo jana tumeshuhudia aliyewahi kuwa waziri wa mambo
ya ndani ya nchi Laurence Masha alivyoshughulikiwa,” amesema.
Amesema
wapiga kura hawahitaji kusikia matusi wala vijembe kutoka kwa wagombea,
viongozi au wanachama wa vyama vya siasa wanachotaka kusikia ni sera za
vyama hivyo vya siasa na sio vinginevyo.
“Tunawaomba
makada wa CCM waache kuendesha kampeni kwa mabavu, Magufuli (John)
hatuna tatizo naye tunamshauri asikubali kuombewa kura na watu
wanaotumia matusi,” amesema.
Aliongeza
kuwa kitendo cha Rais Mkapa kutoa lugha za matusi kitamharibia mgombea
wa CCM na kumpunguzia idadi ya kura kwa kuwa yeye alikuwa kama mdhamini
wake kwa wapiga kura.
0 comments :
Post a Comment