Katapila
likiwa ndani ya gari tayari kwa kazi ya bomobomoa eneo la Salasala
jijii Dar es salaam ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu
Chini hadi jijini Dar es salaam.
Kazi
ya kubomoa baadhi ya nyumba ikiendelea mwishoni mwa wiki eneo la
Salasala jijii Dar es salaam ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka
Ruvu Chini.
Baadhi
ya wakazi wa eneo la Salasala jijini Dar es salaam wakishuhudia
kazi ya kubomoa baadhi ya nyumba mwishoni mwa wiki ili kupisha ujenzi
wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini.
Kazi
ya kubomoa baadhi ya nyumba ikiendelea mwishoni mwa wiki eneo la
Salasala jijii Dar es salaam ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka
Ruvu Chini.
Mafundi
wakiendelea kubomoa nyumba iliyopo eneo la Salasala kwa hiyari ya
mmiliki wa nyumba hiyo ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu
Chini.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
………………………………………………………………………………………………..
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Zoezi la kubomoa nyumba na
majengo yaliyoingia ndani ya ya hifadhi ya miundombinu ya bomba la maji
kutoka Ruvu Chini limeendelea mwishoni mwa wiki ili kuhakikiha
kunakuwepo usalama wa bomba hilo na kuwapatia wakazi wa jiji la Dar es
salaam na maeneo ya mkoa wa Pwani uhakika wa maji ifikapo Februari,
2016.
Bomo bomoa hiyo ya mwishoni mwa
wiki ilihusisha maeneo ya Salasala ambapo baadhi ya nyumba, karakana na
uzio vyote viljengwa ndani ya hifadhi ya miundombinu hiyo ya maji.
Akizungumzia ubomoaji huo,
Mkurugenzi wa Usimamizi na Ufundi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka
Dar es Salaam (DAWASA), Romanus Mwang’ingo alisema kuwa ni wajibu wa
wakazi wa maeneo hayo kuvunja sehemu za makazi yao yaliyoingia ndani ya
hifadhi ya mradi kwa hiyari ama nyumba hizo kuvunjwa baada ya kukaidi
agizo la kubomoa ili kupisha ujenzi wa bomba la maji kutoka Ruvu Chini
hadi jijini Dar es salaam.
“Umbali sahihi unaopaswa wakazi
hao kujenga makazi yao kutoka lilipo bomba la maji ni mita 15 kila
upande ambapo hatua hiyo inapelekea kuwa jumla ya mita 30 ya umbali
unaotakiwa ili kuhakikisha kunakuwepo na usalama na kuruhusu matengenezo
mengine tofauti na hali ya awali ambayo huwezi hata kufanya kazi maana
bomba limepita ndani ya uzio na makazi ya watu ambayo ni hatari kwa
usalama wa maisha yao na mali zao” alisema Mwang’ingo.
Vile vile Mwang’ingo alizitaja
changamoto zilizochangia kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo kwa
wakati ni kuwepo kwa kesi zilizofunguliwa na wananchi kuzuia ufanisi wa
kazi hiyo ambapo kulikuwa na kesi 17 katika mahakama mbalimbali katika
maeneo hayo ikiwemo mahakama ya ardhi.
Kwa mujibu wa Mwang’ingo hadi
sasa DAWASA imeshinda kesi 13 na kupewa haki ya kutumia njia hiyo
kukamilisha upanuzi wa mradi na zimebaki kesi nne ambazo bado zipo
mahamani na zimefikia hatua mbalimbali kulingana na taratibu za
kimahakama.
Kwa upande wake mkazi wa
Salasala Mhandisi Josephat Nakapange ambaye sehemu ya nyumba yake pamoja
na uzio vipo ndani ya hifadhi hiyo ya bomba la maji kutoka Ruvu Chini
hadi Dar es salaam alisema kuwa yeye hana tatizo wala ugomvi na mradi
huo, wamepokea maelekezo na wanayafanyia kazi.
“Hivi sasa ninavyoongea mafundi
wapo kwenye eneo langu wanaendelea na zoezi la kutoa mabati na baadaye
kuvunja kuta zilizo ndani ya umbali unaotakiwa kuachwa wazi kwa ajili ya
mradi wa bomba la maji” alisema Josephat.
Aidha, Josephat aliongeza kuwa
ni vema ziwekwe alama katika maeneo yote yanayotakiwa kuachwa wazi
ambayo yapo ndani ya hifadhi ya mradi ili kuepusha usumbufu na gharama
zisizo za lazima kwa wakazi ulipopita mradi huo.
Maeneo yaliyohusishwa na
ubomoaji huo mwishoni mwa wiki ni pamoja na Bunju, Bondeni, Boko,
Tegeta, Mbezi Intacheki, na Mbezi Tangibovu ili kuruhusu kukamilisha
ujenzi wa bomba hilo la maji kutoka Ruvu Chini ha jijini Dar es salaam

0 comments :
Post a Comment