Na Modewjiblog team
MFANYABIASHARA
na mtu mwenye taasisi ya kusaidia jamii, Mohammed Dewji maarufu kama Mo
ametunukiwa tuzo ya jarida maarufu la Forbes ya “Forbes Africa Person
Of the Year 2015” katika hafla iliyofanyika Novemba 27 mwaka huu jijini
Johannesburg, Afrika Kusini.
Mfanyabiashara
huyo pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Mohammed Enterprises T
Ltd (MeTL Group) kampuni iliyoanzishwa na na baba yake katika miaka ya
1970 ambayo sasa imekua na kujikita katika viwanda vya nguo, usagaji
nafaka, utengenezaji wa vinywaji baridi, usindikaji wa mafuta ya kula,
usindikaji wa chai na kuendesha mashamba ya mkonge ambapo tayari anashea
ya asilimia 40 ya soko.
Mo
ametwaa tuzo hiyo kwa kuwashinda watu watano mashuhuri barani Afrika.
Watu hao ni Nkosazana Dlamini Zuma, mke wa Kwanza wa Rais wa Afrika
Kusini, Jacob Zuma. Mama huyo kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa
Afrika (AU). Mwingine ni Rais wa sasa wa Nigeria, Muhammadu Buhari
aliyetambuliwa kutokana na kuanzisha vita dhidi ya rushwa nchini mwake.
Aidha
wapo Arumna Otei, mchumi mahiri raia wa Nigeria ambaye kwa sasa ni
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia. Pia alikuwemo Mwandishi maarufu wa
vitabu wa Nigeria, Chimanda Ngozi Adichie ambaye moja ya vitabu vyake
vinaelezea picha halisi ya Afrika inavyofikiriwa duniani.
Akitoa
neno la shukurani baada ya kukabidhiwa kwa tuzo hiyo Mo, alisema anatoa
tuzo hiyo kwa vijana wa Kitanzania kwani ndio nguvu kazi inayobeba
uchumi wa nchi.
Mo
ambaye kampuni yake ya MeTL inaongoza kwa kutoa ajira nchini, ikiwa
imetoa ajira 26,000 kote katika viwanda vyake 31 vilivyopo nchini na
katika mataifa matano ya Afrika, alisema amefurahishwa na tuzo hiyo
ambayo anaitoa kwa vijana kwa kutambua pia wajibu mkubwa walionao katika
kukabiliana na umaskini.
Alisema
ajira 26,000 zimegusa watu wengi nchini na kwamba ana matumaini makubwa
ya siku za
usoni kutoa ajira zaidi kutokana na biashara zake kuendelea
kukua.
“Heshima
yangu kubwa haitokani na utajiri, maana kama utajiri wako hauna msaada
wala kugusa watu masikini hauna maana yeyote, hivyo basi heshima hii ni
kutokana na kwanza bidhaa zangu kugusa maisha ya watu kila siku kuanzia
sukari na majani ya chai asubuhi pamoja na unga wa ngano, lakini pia
chakula cha mchana kwa unga wa sembe, mafuta ya kupikia na maji ya
kunywa, bidhaa zote hizo za Mohammed Enterprises zinagusa maisha kila
nyakati katika siku.
“Nina
viwanda 31 ambavyo vimekuwa vikitengeneza bidhaa za Kitanzania na
kuziuza kwa Watanzania kwa bei yenye unafuu mkubwa, mathalani tunauza
maji kwa bei chini ya dola moja kwa shilingi za Kitanzania 200, hakuna
hata Ulaya, nina kiwanda cha khanga na vitenge ambacho malighafi zake
zote ni za Kitanzania, hivyo kuna kusaidia serikali kwa kulipa kodi
ipasavyo, lakini pia kusaidia moja kwa moja ajira za Watanzania walio
wengi ambao tatizo lao kubwa katika kundi la vijana ni ajira”
Alitumia
fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza baba yake kwa kumwita mjasiriamali
shujaa ambaye alitoka kuanzia dereva wa malori baada ya kuhitimu kidato
cha nne mwishoni mwa miaka ya 1960 hadi kufikia ubilionea. Alisema
alipata maono ya utajiri hasa kutoka kwa baba yake huyo aliyekuwa
akimshirikisha biashara tangu akiwa mdogo.
“Mwanaume
mwenye ndoto huhitaji mwanamke mwenye maono. Na nimebarikiwa mwanamke
ambaye kwa miaka 15 amekuwa akinipa sapoti isiyoyumba.
“Saira,
nina shukurani nyingi kwako kwa kuwa nguzo ya familia yetu, mama wa
heshima kwa watoto wetu watatu,” alisema Mo kwenye hafla hiyo.
Kwa
utulivu, Mo alisema: “Baba, zawadi kubwa ambayo ulinipa katika maisha
yangu ni muda wako, na kwa hilo nitakuwa mwenye deni la shukurani kwako
siku zote za maisha yangu.”
Mo
ambaye moyo wake wa binadamu ulimfanya awanie uwakilishi Jimbo la
Singida Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda nafasi
hiyo na hivyo kuwawakilisha wanasingida kuanzia 2005 na 2015 amesema
maisha ni changamoto kubwa inayobadilishwa kwa utumishi wenye nia ya
dhati kwa umma.
Alisema
alipowania uwakilishi alikuwa na sababu: “Nilikuwa na umri wa miaka 24,
nilikwenda Singida kutoa heshima kwenye kaburi la marehemu babu yangu.
Sikuwa nimefika huko tangu nilipoondoka nikiwa na umri wa miaka mitatu.
“Nilipokuwa
njiani, nilimuona mzee akiwa na maji yenye rangi ya njano, machafu
ambayo aliyatumia kwa kunywa. Nilishangaa, maana hali ile sikuwahi
kufikiri kama ipo vile. Kipindi hicho nilikuwa nimemaliza Chuo Kikuu cha
Georgetown, Marekani.”
Mo
anasema kuwa aliingiwa na hisia kutaka kujua nini hasa alichokuwa
anahitajika kufanya, alimfuata yule mzee aliyekuwa na maji yale,
alipozungumza naye, aliwazungukia watu wengine na kuridhika kuwa ile
ndiyo hali halisi, hapo ndipo fikra ya kwa nini agombee ubunge
ilipoanzia.
Anasema
kuwa baada ya kujiridhisha hivyo, alirudi kwa mzee wa kwanza,
alizungumza naye na kumuuliza ni kwa nini shida ile ilikuwa haizungumzwi
kwa upana katika mamlaka husika.
“Nilipojitambulisha yule mzee alisema anamkumbuka babu yangu, kisha
akanishauri nigombee ubunge, alinisisitiza mno ili nisaidie kuondoa lile
tatizo la watu wa Singida kunywa maji machafu,” alisema Mo.
Anaeleza
kuwa alipokuwa njiani kurejea Dar es Salaam, alilifikiria tatizo hilo
kwa mapana zaidi, akalifanyia utafiti na kubaini kwamba katika kila watu
10, watatu walikuwa wakipoteza maisha kutokana na maradhi
yanayosababishwa na maji machafu.
Anaendelea
kusema kuwa aligundua kuwa Singida kulikuwa na tatizo kali la maji safi
na salama. Anasema kuwa alibaini uwepo wa tatizo la elimu kuhusu
matatizo ya maji.
Jambo
lingine ambalo anasema aliligundua ni uwepo wa tatizo la huduma za
afya. “Niliwafikiria watoto wangu, jinsi ninavyowapenda, na namna
ambavyo kila mzazi anavyompenda mwanaye. Nilipingana na hali kuwa watoto
wa Uingereza na Marekani wamependelewa zaidi. Maisha ni sawa bila
kujali chochote,” anasema Mo.
“Niliona
lazima nitimize wajibu wangu. Kutimiza malengo yangu ya kusaidia jamii,
kufanikiwa katika biashara. Mambo hayo mawili hisani na biashara
nimeyaweka pamoja na ndiyo maana nimefika hapa leo, tunajivunia sana
kuitwa METL nembo ya Watu. Katika miaka yangu 10 kama mbunge, nimefanya
mabadiliko mengi. Nilikuwa na sababu ya kupata mkopo nafuu wa dola
milioni 35, ambao ulisababisha kuwekwa kwa miundombinu ya maji safi na
salama Manispaa ya Singida.
“Niliitumia
MeTL, tuliweza kudhamini shughuli nyingi za maendeleo ya kijamii.
Kuhusu elimu, nilifanikisha kujenga shule 15, zikawa 17, kabla ya hapo
tulikuwa na shule mbili tu. “Kuhusu huduma za afya, hapa nimshukuru mke
wangu kwa jitihada zake. Alikuwa Mwenyekiti wa taasisi ya Tumaini la
Maisha ambayo imekuwa ikisaidia watu wengi, hasa watoto dhidi ya maradhi
ya saratani.”


0 comments :
Post a Comment