Tuesday, December 1, 2015
@nkupamah blog
Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la kuchunguza makosa ya jinai (AFO), imeibua kashfa ya rushwa katika ununuzi wa dhamana (hati fungani) ya serikali katika kipindi cha uongozi wa aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete.
Madai
hayo yametolewa jijini Dar es Salaam jana na Kiongozi Mkuu wa Chama cha
ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, katika taarifa yake aliyoisambaza kwenye
vyombo vya habari jana.
Katika
taarifa yake hiyo, Zitto alidai kuwa biashara hiyo iliyofanyika kati
mwaka 2011 na 2012, iliyohusisha serikali na benki ya Standard Group ya
Afrika Kusini kupitia Stanbic ya Tanzania ilikuwa na thamani ya Dola za
Marekani milioni 600 (sawa Sh. Tanzania trioni 1.2).
Benki
ya Standard Group ambayo ni benki mama ya Stanbic Tanzania, imekiri
makosa hayo na kukubali kulipa faini ya Dola milioni 25.2 (sawa na Sh.
bilioni 54 ) kwa kosa hilo.
Ilikubali
kulipa faini hiyo mbele ya Jaji Lord Justice Leveson, wakati shauri
hilo liliposikilizwa jana kwenye Mahakama ya Southwark nchini Uingereza.
Benki
hiyo ilikubali shauri hilo limalizwe kwa njia ya muafaka baada ya
kukiri ilitoa kiasi cha fedha ili kuwahonga maofisa wa Tanzania kinyume
na Sheria ya Rushwa ya Uingereza ya mwaka 2010 kufanikisha mpango wao.
Pia
benki hiyo imekubali kulipa kiasi cha Dola milioni saba (sawa na Sh.
bilioni 15.1) kwa Serikali ya Tanzania kama fidia ya shauri hilo baada
ya kubainika walihonga baadhi ya maofisa wa Tanzania kufanikisha mpango
huo.
Hata
hivyo, fedha hizo hazitakabidhiwa moja kwa moja kwa Serikali ya
Tanzania bali zitapitishwa kwenye Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya
Uingereza ili kupangiwa kazi ya kufanya.
Pia
benki hiyo inatakiwa kulipa kiasi cha pauni 300,000(sawa na Sh. milioni
974) ikiwa ni gharama za shauri hilo kusikilizwa nje ya mahakama.
Katika
taarifa yake, Zitto alitaka mamlaka zenye kuchunguza sakata hilo
ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Kudhibiti Biashara Haramu ya
Fedha (FIU) Tanzania na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini
(Takukuru) waungane na SFO kutoa taarifa za chunguzi huo na sababu ya
kutoziweka hadharani mapema.
Aliomba vyombo vya sheria kuwachukulia hatua wote waliohusika na upotevu fedha hizo za Watanzania.
Alisema
hati fungani hiyo ya serikali iliuzwa na serikali kupitia Wizara ya
Fedha kwa benki hiyo ya kigeni ambayo ni miongoni mwa kundi la mabenki
ya Afrika ya Kusini, yenye makao makuu yake London, Uingereza.
Alisema
ni jambo la kawaida duniani serikali kuuza dhamana zake za hati
fungani, lakini kwa Tanzania uligubikwa na harufu ya rushwa na
kuisababishia nchi hasara.
Alidai
kuwa kwa mujibu wa uchunguzi huo, sehemu ya fedha hizo hazikuingia
kwenye akaunti za Serikali ya Tanzania na pia gharama za hati fungani
hiyo zilipaishwa kupitia wakala wa kati.
Kutokana na upaishaji wa gharama hizo, takriban Dola milioni 60 zilitolewa kwa maofisa waliothibitisha biashara hiyo.
Zitto
alimuomba Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati suala hilo akisema
jambo hilo lina maslahi mapana ya nchi, hasa ikizingatiwa na uzoefu
katika masakata kama hayo yanayohusisha nchi za kigeni, kama ununuzi wa
rada, vyombo vya uchunguzi vya hapa nchini, vilitoa majibu ya kutokuwapo
kwa rushwa na kisha kuja kuthibitishwa na Serikali ya Uingereza.
“Baada
ya kuthibitishwa na Uingereza, serikali yetu ilirudishiwa sehemu ya
fedha zilizozidi kwenye manunuzi ya rada, ni vyema Rais Magufuli
akaliingilia kati,” alisema Zitto.
Alisema
ACT-Wazalendo inasubiri taarifa ya makubaliano kati ya SFO na benki
mama ya iliyonunua hati fungani hiyo ili ashauri zaidi hatua za
kuchukua.
“Ikumbukwe
kuwa Benki ya…(anaitaja jina), ilihusika na kashfa ya Tegeta Escrow na
mpaka sasa haijachukuliwa hatua zozote kama ilivyoagizwa na Bunge. Benki
hiyo imewaficha waliochota fedha za Escrow mpaka leo,” alisema Zitto.
Alisema
kashfa hiyo iliwafanya washauri uongozi wa benki hiyo hapa nchini
kuondolewa na kurejeshwa nchini Uingereza kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Hazina, Ramadhani Kijja, alisema kuwa halifahamu suala hilo na kwamba kwa sasa hana maelezo yoyote juu ya jambo hilo.
“Kama Zitto ndiye katoa hiyo taarifa, mimi sina na wala siwezi kuizungumzia kwa sasa,” alisema Kijja.
0 comments :
Post a Comment