Rais Magufuli Atangaza Kupunguza Wafanyakazi Katika Mshirika Ya Umma Ambayo ni Mzigo kwa Serikali

Tuesday, December 1, 2015

  @nkupamah blog

Mamia ya wafanyakazi katika mashirika na taasisi mbalimbali za umma zinazoendeshwa kwa hasara likiwamo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) wako hatarini kufutwa kazi kufuatia amri ya serikali  ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli ya kupunguza mzigo wa gharama za uendeshaji katika taasisi hizo.

Mashirika hayo yameelezwa licha ya kuwa na watumishi wengi, lakini bado uzalishaji na utendaji wake umekuwa hauna tija kwa taifa.



Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Msajili wa  Hazina,  Laurence Mafuru,  katika kikao na wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wa taasisi na mashirika ya umma.

“Kuna kampuni ambazo zimepewa mtaji na serikali, lakini zinashindwa kuzalisha. Zinaandika barua kuomba msaada Serikali Kuu. Kama unaona (mkuu wa taasisi) una wafanyakazi wengi na huzalishi kwa namna inayotarajiwa, ni vyema upunguze watu,” alisema Mafuru.

Kadhalika, licha ya kutoa maelekezo hayo, Mafuru alizitaja taasisi kadhaa zinazoendeshwa kwa hasara au kuzalisha chini ya kiwango kinachotarajiwa kuwa ni Tanesco, Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Shirika la Ndege (ATCL), Kampuni ya Simu Tanzania ( TTCL) na Shirika la Bima la Taifa (NIC).

Maafuru alizitaja taasisi na mashirika mengine yasiyofanya vizuri kuwa ni Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Bandari (TPA), Kampuni ya Miliki ya Rasilimai za Reli (Rahco) na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

Mafuru alisema Serikali haihitaji kuvuna fedha katika taasisi hizo, bali jambo kubwa ni kuona kuwa zinajiendesha na kutimiza malengo yanayotarajiwa na umma wa Watanzania.

“Serikali haihitaji kuchukua fedha katika taasisi hizi. Isipokuwa tunataka (taasisi za umma) zifanye kazi na ziwe nguzo za uchumi wa nchi. Tuache bajeti inayotengwa (na serikali) ifanye kazi nyingine ya maendeleo kwa Watanzania,” alisema, huku akiyataja Tazara na TRL kuwa ni vinara wa kuomba fedha kwa Serikali Kuu ili kulipa mishahara ya wafanyakazi wake.

“Kwa mfano Tanesco, kwa kipindi chote ilichoanza kufanya kazi mpaka sasa tulitarajia iwe imefanya kazi nzuri ya uzalishaji, lakini badala yake tunaona kinyume chake na hapo isitegemee kwamba endapo itaendelea kufanya hivyo serikali itakuwa inaangalia tu,” alisema.

“Ni vema kama kuna shirika au taasisi ya umma ambayo inaona haizalishi na ina wafanyakazi wengi iwapunguze wafanyakazi hao. Kama tunaona tunashindwa, ni vyema tupunguze watu au turudi nyumbani tukapumzike,” alifafanua Mafuru.

Mafuru aliongeza kuwa baadhi ya sababu za kufanya vibaya kwa taasisi na mashirika ya umma ni uzembe wa baadhi ya watumishi ambao hawafanyi kazi kwa kiwango kinachotarajiwa na wala kuwajibika ipasavyo katika kutimiza majukumu yao.

Alisema tatizo jingine ni viongozi wa baadhi ya taasisi na mashirika hayo ya umma kuchukulia nafasi za uteuzi wanazopewa kuwa ni zawadi, fikra ambazo hivi sasa wanapaswa kuzifuta mara moja na kutanguliza zaidi uwajibikaji hasa kwa kutambua kuwa serikali ya awamu ya tano inaangalia zaidi utendaji wenye matokeo chanya kwa umma na siyo kinyume chake.

“Msifikiri kwamba nyie ndiyo wapishi (wajuzi) pekee… wapo watu wengine wanaojua zaidi, kwa hiyo mjiandae kufanya kazi. Kila mtu atawajibika kwa nafasi yake,” alisema.

Alisema  pamoja na kwamba serikali imezipa mali  taasisi hizo kujiendesha, lakini zimendelea kuwa mzigo kwa serikali kwani baadhi hushindwa kuzalisha na kuwa vinara wa ‘kutembeza bakuli’ kwa maana ya kuomba msaada kwa Serikali Kuu mara kwa mara.

Mafuru alikitaja Chuo cha IFM kuwa ni mojawapo ya taasisi za serikali zinazoshangaza kwani licha ya kuwa na fursa ya kuzalisha, bado kimekuwa kikiendeshwa kwa hasara na kuwa miongoni mwa vinara wa kuomba msaada kwa Serikali Kuu.

“Kwa mfano Chuo Kikuu binafsi cha Tumaini, kinajiendesha kutokana na ada za wanafunzi pekee. Kwa nini IFM inashindwa kufanya hivyo?” alihoji.

Alisema taasisi zinazojiendesha kwa hasara zimekuwa mzigo mzito kwa serikali, hivyo ni lazima sasa kwa wakuu wa taasisi husika kuhakikisha kuwa wanaongeza ufanisi ili kujikwamua kutoka katika hali mbaya kiuchumi waliyonayo.

“Hivi sasa serikali ina taasisi 220 kutoka 600 zilizokuwapo awali. Pamoja na kwamba taasisi za serikali zimepewa assets (mali) za kuzalisha, bado (baadhi) zimeshindwa kufanya hivyo, badala yake nyingine kila siku zinaandika barua kuomba fedha katika Mfuko Mkuu wa Serikali kuongezewa mtaji,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mafuru alisema inasikitisha kuona kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) ni miongoni mwa taasisi zisizozalisha kwa kiwango kinachotarajiwa na kwamba hadi sasa, hakuna faida yoyote ambayo imekuwa ikirudisha serikalini.

Alisema kama TPA inafanya vizuri, ilitakiwa kufanya maendeleo mengine ikiwamo kujenga bandari nyingine.
 
Aliitaka taasisi hiyo na nyinginezo kama TPDC kujifunza kutoka kwa taasisi binafsi juu ya namna ya kuongeza uzalishaji.

Alisema kutokana na uendeshaji wa hasara kwa baadhi ya taasisi na mashirika ya umma, matokeo yake mashirika na taasisi hizo, kwa pamoja huchangia asilimia 22 tu ya pato la Taifa kwa mwaka, hali ambayo haipaswi kuendelea.

Wakati huo huo, Mafuru alitoa agizo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa taasisi za umma ifikapo Desemba 15, zikiwamo zote zilizobainika kuwa hazikuwa zikifanyiwa ukaguzi hapo kabla.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment