Mchezaji Bora mara tano wa tuzo ya Ballon d’Or, Lionel Messi amefunguka na kuweka wazi kuwa anazipenda ligi za Uingereza na Italia.
Messi alisema hayo wakati akizungumza na kituo cha tv cha Misri, MBC na kueleza kuwa licha ya kuzipenda ligi hizo bado anataka kusalia Barcelona kwa maisha yake ya soka kabla ya kuhamia katika timu yake ya utotoni, Newell’s Old Boys.
“Ninapenda mpira wa Uingereza na Italia” alisema na kuongeza “Huwa natazama michezo mikubwa lakini nilishasema ninataka kuendelea kuchezea Barcelona kwa miaka mingi na hadi nitakapostafu”
Awali kabla ya Messi kuzungumzia jambo hilo amekuwa akihusishwa kujiunga Manchester City na dili hilo linaonekana kuwa rahisi kukamilika kutokana na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola kujiunga na Manchester City baada ya msimu huu kumalizika.