Thursday, November 12, 2015
@nkupamah blog
Aliyekuwa mgombea wa urais wa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa anatarajiwa kupanda jukwaani Jumamosi kumuombea kura mgombea wa ubunge wa Chadema Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema.
Akizungumza
katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge katika jimbo hilo
uliofanyika Soko Kuu jana, Lema alisema Lowassa atazungumza na
Watanzania na kuwashukuru pia kwa kura nyingi walizompa.
Awali,
mbunge mteule wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alieleza kuwa
Lowassa na viongozi wa Chadema watatoa tamko zito siku hiyo na kuwataka
wakazi wa Arusha na Watanzania kutega masikio.
Lema
ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwataka wakazi wa
Arusha, kutokatishwa tamaa na kuendelea kuwa na huzuni kutokana na
matokeo ya urais yaliyotangazwa na kuwa bado kuna harakati za chama
hicho kusaka haki.
“Ndugu
zangu msikate tamaa, tumesikia wengine wametupa shahada zao, hapana,
kazi ndiyo imeanza na lolote linaweza kutokea kwa uwezo wa Mungu,”
alisema.
Alisema
huzuni ya matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
haipo kwa wananchi tu, bali hata wajumbe wote wa kamati kuu.
“...Kwenye
kikao cha kamati kuu, kuna wajumbe walimuomba Lowassa atoe tamko...
kama angetoa tamko la kupinga matokeo na kukubali watu kuingia mitaani,
Tanzania ingekuwa imeingia katika machafuko makubwa.
“Tunaendelea
kutumia taasisi za kimataifa kudai haki, ndiyo sababu mnaona Zanzibar
wameshindwa kujitangazia matokeo, hii ni kazi kubwa ya Ukawa,” alisema.
Katika
mkutano huo, Lema alieleza njama alizosema zinapangwa kumnyima ushindi
na akaonya kuwa hatakuwa tayari kuona ameshinda lakini mwingine
akatangazwa kushinda.
“Najua Arusha nitashinda kwa kura nyingi, lakini kama wakitaka kunipora ushindi sitakubali,” alisema Lema.
Aliwaomba
wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi Desemba 13 kumpigia kura nyingi,
ili pia kuwezesha Chadema kupata viti viwili zaidi vya wabunge wa viti
maalumu.
0 comments :
Post a Comment