Saturday, November 14, 2015
@nkupamah blog
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
amerejea kauli yake ya kutotambua kufutwa kwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar
uliofanyika tarehe 25 mwezi uliopita.
Akizungumza na waandishi wa
habari jijini Dar es Salaam mara baada ya kikao cha mashauriano na
viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA, Maalim Seif amesema
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar Bw Jecha Salim Jecha hana
mamlaka ya kufuta uchaguzi huo, na kinachohitajika na kuendelea na
mchakato wa kuhakiki kura zilizobakia na mshindi kutangazwa.
Kuhusu
tamko lililotolewa na serikali juu ya kufutwa rasmi kwa uchaguzi huo
kupitia tangazo lililochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali tarehe
sita mwezi huu, Maalim Seif amesema tamko hilo limekosa uhalali tangu
lilipotolewa na Mwenyekiti wa ZEC.
Maalim Seif ambaye pia ni
Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CUF amesema Chama chake
hakijalizingatia tamko hilo na wala hakijadili uwezekano wa kurejewa kwa
uchaguzi huo, kwa madai kuwa uchaguzi ulikamilika bila ya kuwepo
malalamiko kutoka chama chochote cha siasa na wala Tume ya Uchaguzi.
Mapema
akizungumza baada ya kikao hicho cha mashauriano, aliyekuwa mgombea
Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema Mhe. Edward
Lowassa amesema kikao hicho kilichojadili Mkwamo wa kisiasa Zanzibar
kimekwenda vizuri.
Hata hivyo amesema ufafanuzi zaidi utatolewa
Jumapili ijayo ambapo viongozi hao wanakusudia kuzungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kikao hicho Maalim Seif
alifanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Filberto
Seregondi katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kuelezea hatua
zinazochukuliwa kukwamua mkwamo wa kisiasa Zanzibar.
0 comments :
Post a Comment