Friday, November 6, 2015
@nkupamah blog
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Mhe. Damian Lubuva ametangaza idadi ya wabunge wa Viti Maalum leo katika ukumbi wa ofisi za Tume hiyo jijini Dar es Salaam.
Jaji
Lubuva akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari alisema kwamba, kwa
mujibu wa Ibara ya 66(1) (b) na Ibara ya 78 ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha
86A cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi sura ya 343, Tume imepewa mamlaka ya
kutangaza Viti Maalum vya wabunge wanawake visivyopungua asilimia 30 ya
wabunge. Idadi ya Viti Maalum iliongezeka na kufikia asilimia 40 mwaka
2010 kwa mujibu wa uamuzi wa Serikali.
“Katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 viti maalum idadi yake ni 113, kutokana na
kuwepo majimbo 8 ambayo hayakufanya uchaguzi mgawanyo wa Viti Maalum kwa
sasa ni 110, viti 3 vilivyobaki, vitagawanywa baada ya kufanyika kwa
uchaguzi katika majimbo hayo.” Alisema Jaji Lubuva.
Jaji
Lubuva alisema kuwa, vyama ambavyo vimekidhi vigezo vya kikatiba na
kisheria na kupata angalau asilimia 5 ya kura zote halali za wabunge
ndio vitakavyo kuwa na wabunge wa Viti Maalum. Huku idadi ya wabunge
Viti Maalum kutoka katika vyama vinategemea na idadi ya kura halali za
wabunge ambavyo vyama hivyo vimepata.
Kutokana
na matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini mwishoni mwa mwezi
Oktoba, idadi ya kura halali ya wabunge kwa vyama vitatu vilivyopata
angalau asilimia 5 ni CCM kura 8,333,953 imepata jumla ya Viti Maalum
64, CHADEMA kura 4,627,923 imepata jumla ya Viti Maalum 36 na CUF kura
1,257,051 imepata jumla ya Viti Maalum 10.
0 comments :
Post a Comment