Tuesday, December 1, 2015
@nkupamah blog
KESI ya matokeo ya ubunge katika Jimbo la Kigoma Kusini iliyofunguliwa na David Kafulila, inamkutanisha uso kwa uso na Jaji John Utamwa lakini pia wakili Kennedy Fungamtama..
Fungamtama
alikuwa wakili wa Kampuni ya Dowans katika kesi dhidi ya Shirika la
Umeme nchini (Tanesco) wakati Jaji Utamwa ndiye aliyetoa hukumu ‘tata’
ya kesi ya kampuni ya kufua umeme wa dharura (IPTL) mwaka 2013 iliyozaa
sakata la ufisadi kwenye Akaunti Escrow.
Kwenye
kesi ya Dowans dhidi ya serikali (Tanesco), Wakili Fungamtama akiitetea
Dowans alishinda wakati katika kesi ya IPTL, Jaji Utamwa alitoa hukumu
inayotajwa kuwa chanzo cha sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh. 306
bilioni kwenye Akaunti ya Esrcow bungeni mwaka 2014.
Hatua ya kuchotwa kwa fedha hizo ndiyo iliyomuibua Kafulila ambapo alidai kuwepo kwa ufisadi katika uchotaji huo.
Katika
kesi ya uchaguzi ya Kafulila, wakili Fungamtama amesimama kumtetea
mbunge wa jimbo hilo, Hasna Mwilima aliyetangazwa kushindwa kupitia
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo Jaji Utamwa ndiye aliyepangiwa
kusikiliza kesi hiyo.
Kwenye
kesi hiyo Kafulila anayetetewa na wakili Daniel Lunyemela ambapo
anaiomba Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imtangaze kuwa mshindi halali wa
uchaguzi huo kama ambavyo kura za jumla katika fomu za matokeo ya vituo
vyote 382 zinaonesha tofauti na matokeo yaliyotangazwa.
Wakili
Fungamtama anayekumbukwa kama wakili wa kampuni ya Dowans katika kesi
ya madai Na.8/2011 iliyofunguliwa na Tanesco kupinga kusajiliwa katika
Mahakama Kuu nchini hukumu ya kuilipa Dowans kiasi cha fedha zaidi ya
bilioni 94 sasa anamkabili Kafulila ambaye ndiye mlalamikaji katika kesi
hiyo.
Fungamtama
pia anatajwa kama wakili ghali sana hapa nchini na duniani kutokana na
gharama kubwa ambazo hutoza wateja wake wanaohitaji huduma ya kisheria
huku akisifika pia kwa kumudu na kujua kucheza ‘siasa za kisheria’
katika kesi mbalimbali anazosimamia.
Hata
hivyo Kafulila anaeleza kuwa kesi yake ipo ‘wazi’ kwa kuwa anavyo
vielelezo vyote kutoka katika vituo 382 vya kupigia kura na kwamba
atashinda.
Mwandishi
wa habari hizi amemtafuta Kafulila ili kueleza mtazamo wake juu ya kesi
hiyo kusikilizwa na Jaji John Utamwa lakini pia Mwilima kutetewa na
Fungamtama, hata hivyo hakupatikana.
Kesi
hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi namba 2/2015 katika Mahakamu Kuu ya
Tabora inaendelea leo jumatatu Novemba 30 ambapo Jaji Utamwa
atasikiliza ombi lililowasilishwa na Kafulia akitaka kupunguziwa malipo
ya dhamana kwani anatakiwa kulipa dhamana ya Sh. 15milioni kutokana na
kulalamikia washitakiwa watatu.
Washitakiwa
hao watatu ni Hasna Sudi Mwilima (CCM) ambaye ni mbunge, msimamizi wa
uchaguzi huo Reuben Mfune pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Geoge
Masaju.
0 comments :
Post a Comment