Kamishna Jenerali wa Magereza
Nchini, John Casmir Minja akitoa hotuba kwa Watumishi wa Jeshi la
Magereza(hawapo pichani) kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na
kuukaribisha Mwaka mpya 2016. Baraza hilo limefanyika Desemba 31, 2015
katika Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Jijini Dar es Salaam.
Askari wa vyeo mbalimbali wa
Jeshi la Magereza wakimsikiliza Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza
wakati akitoa hotuba yake kwenye Baraza la kufunga Mwaka 2015 na
kuukaribisha Mwaka mpya wa 2016.
Maafisa Waandamizi wa Jeshi la
Magereza wakiwa timamu kumpokea Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza,
John Casmir Minja(hayupo pichani) wakati akiwasili tayari kwa
kulihutubia Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya wa
2016.
Maafisa ngazi ya juu wa Jeshi la
Magereza wakifuatilia kwa makini hotuba fupi aliyoitoa Kamishna Jenerali
wa Magereza, John Casmir Minja(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la
Magereza).
…………………………………………………………………………………………………
Na Lucas Mboje, Dar es Salaam
WATUMISHI wa Jeshi la Magereza
wametakiwa kuzingatia utendaji kazi wenye tija mahala pa kazi na kuacha
kufanya kazi kwa mazoea(Business as usual).
Rai hiyo imetolewa na Kamishna
Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja wakati akizungumza kwenye
Baraza la kufunga Mwaka 2015 na kuukaribisha Mwaka mpya 2016 katika
Ofisi za Makao Makuu ya Jeshi hilo Jijini, Dar es Salaam.
Jenerali Minja amewaagiza
Watumishi wote wa Jeshi hilo kuhakikisha kuwa wanawajibika kwenye maeneo
yao ya kazi ili kufikia ufanisi uliotarajiwa pamoja na kutumia vizuri
rasilimali za Ofisi kwa manufaa yaliyokusudiwa.
“Utekelezaji wenu wa kazi za kila
siku lazima uwe na tija na uendane sambamba na kasi ya Serikali ya
Awamu ya Tano ili kufikia ufanisi unaotarajiwa”. Alisema Jenerali Minja.
Aidha Jenerali Minja amezungumzia
baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa Mwaka 2015 ambayo ni pamoja na
kukamilika kwa Sera ya Taifa ya Magereza ambayo italiwezesha Jeshi hilo
kutekeleza mpango wake wa Maboresho ya maeneo mbalimbali, kusainiwa kwa
Mkataba na Kampuni ya Poly Teknology ya China itakayojenga nyumba 9,500
za Makazi ya Maafisa na Askari, kusainiwa kwa Mkataba wa Magari 9,05 na
Kampuni ya Ashok Leyland ambapo magari hayo yanatarajiwa kupokelea
mapema mwakani.
Mafanikio mengine ni pamoja na
Usajili wa kudumu wa Chuo cha Urekebishaji ambapo Chuo hicho kitatoa
elimu stahiki ya Urekebishaji itakayotambulika ndani na nje ya Nchi,
Jeshi la Magereza limepeleka Maafisa wake kwenye shughuli za Ulinzi wa
Amani kwenye nchi mbalimbali zenye migogoro, Jeshi limeingia ubia na
Wawekezaji mbalimbali katika miradi ya Kilimo, uchimbaji madini ya
chokaa, ujenzi wa maduka makubwa(shopping Malls) katika Mikoa ya
Morogoro na Kilimanjaro ambapo miradi hiyo itakuwa na manufaa makubwa
kwa Jeshi.
Vilevile Jeshi limefanikiwa
kuandaa Maandiko mbalimbali ikiwemo andiko la kujitosheleza kwa chakula
na miradi minane ambayo miradi hiyo ikiwezeshwa inaweza kuongeza thamani
za mali zinazozalishwa na Jeshi hilo.
Aidha Jenerali Minja alieleza
changamoto mbalimbali ambazo Jeshi hilo linakabilianazo ambazo ni ufinyu
wa bajeti, uhaba na uchakavu wa vyombo vya usafiri, ukosefu wa zana za
kilimo, mabadiliko ya hali ya hewa hivyo kuathiri Uzalishaji, tatizo la
miundombinu ya magereza na msongamano magerezani hali inayopelekea kwa
kiasi fulani kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Jeshi hilo.
Kamishna Jenerali wa Magereza,
John Minja ametoa Salaam za kheri ya Mwaka mpya 2016 kwa Watumishi wote
wa Jeshi hilo na kuwataka kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
Taratibu zinazotawala uendeshaji wa Jeshi la Magereza.
0 comments :
Post a Comment