Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bibi Sihaba
Nkinga akifungua Tamasha la 13 la AZAKi lililoandaliwa na shirika la the
Foundation For Civil Society na kufanyika katika ukumbi wa Hoteli ya
Blue Pearl Ubungo Dar es salaam tarehe 1/12/2015
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Bibi Sihaba
Nkinga (mwenye suti ya blue) akiwa
na baadhi ya wadau wa
waliohudhuria Tamasha la 13 la AZAKi lililoandaliwa na shirika la the
Foundation For Civil Society na kufanyika katika ukumbi wa Hoteli ya
Blue Pearl Ubungo Dar es salaam tarehe 1/12/2015.
………………………………………………………………………………………………….
Erasto T. Ching’oro, Msemaji – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Wadau wa Asasi za Kiraia
wamekutana ukumbi wa Blue Pearl Ubungo Dar es salaam kuanzia tarehe 1-
2/12/2015 kushiriki Tamasha la maonesho ya shughuli zinazotekelezwa na
mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Akizindua Tamasha hilo la siku
mbili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto
Bibi Sihaba Nkinga, ametoa shukrani kwa shirika la the Foundation for
Civil Society kwa kuandaa Tamasha hilo la Kumi na Tatu la mwaka 2015
lenye Kauli Mbiu: ‘Wajibu wa Asasi za Kiraia katika Utekelezaji wa
Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030’.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo yenye
dhamana ya kusimamia na kuratibu shughuli za AZAKi hapa nchini ameeleza
kufurahishwa na wadau wa AZAKi kwa kuendelea kushiriki na kuchangia
katika jitihada za kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Ameongeza kuwa ushiriki na kauli mbiu ya Tamasha la mwaka 2015 ni
ushahidi tosha kuwa AZAKi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni wabia
muhimu katika maendeleo.
Akimkaribisha mgeni rasimi, Bibi
DKT. Stigmata Tenga ambaye ni Rais wa Foundation for Civil Society
alieleza kuwa malengo ya Tamasha ni Kutoa fursa kwa washiriki kujadili
na kuainisha masuala yatakayozingatiwa na jinsi ya kuimarishsa ushiriki
mpana wa wananchi na Asasi za Kiraia (AZAKi) na kuyapa kipaumbele wakati
wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu. Aidha, Tamasha hilo
litajenga jukwaa kwa wadau wa AZAKi kujadili namna ambavyo Foundation
for Civil Society itaboresha huduma za kujenga uwezo wa Asasi za Kiraia
nchini kwa kutoa ruzuku na huduma za kuimarisha uwezo wa asasi
kiutendaji na kiutawala.
Tamasha la Azaki linakutanisha
takribani wadau 300 kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini. Bibi Nkinga
amaeleza kuwa fursa hii itatumiwa na wadau kujenga uelewa wa pamoja
kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu na kuweka mikakati ya kukuza
ushiriki katika utekelezaji wa malengo hayo kwa kuzingatia misingi ya
uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji wa jamii. Amewaasa wadu kushiriki
katika mchakato wa kuandaa Malengo Mapya ya Maendeleo endelevu ya mwaka
2030 kusaidia kuwafahamisha washiriki wengine mchakato uliotumika
kuandaa Malengo hayo ili wayafahamu na kuyatekeleza kwa lengo la
kufanikisha azma ya kuondoa umasikini kwa kushirikiana na Serikali na
wadau wengine.
Akifafanua Bibi Sihaba amewataka wadau kutumia Tamasha la Azaki kujadili kwa kina Mafanikio, Changamoto na mambo ya msingi waliyoyabaini wakati wa utekelezaji wa Malengo ya Milenia.Kwani madaliano ya washiriki yataweka msingi wa uelewa wa pamoja na kuwawezesha kujipanga vizuri katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Itakumbukwa kwamba, baada ya
kutolewa kwa Malengo ya Maendeleo ya Milenia yaliyopita, nchi yetu
iliandaa mikakati madhubuti ya kuitekeleza. Mikakati hiyo ikiwa ni
pamoja na MKUKUTA (Tanzania Bara), MKUZA kwa Zanzibar na Mpango wa
Maendeleo wa Miaka 5. Mikakati hii ilikuwa na vipaumbele pamoja na
viashiria vya kupima na kufuatilia ili kuhakikisha kuwa tunafikia
Malengo yaliyowekwa.
Katika utekelezaji wa Malengo ya
Milenia kama nchi tuliweza kupata mafanikio makubwa katika maeneo
mablimbali ikiwa ni pamoja na: Kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi
wanaoandikishwa mashuleni; Kuongezeka kwa Idadi ya wanawake katika
vyombo vya maamuzi kama Bunge hadi kufikia Asilimia 30; Ongezeko la
uwiano wa wanafunzi wa kike na wakiume katika shule za Msingi na shule
za Sekondari; Tanzania imeweza kupunguza kwa Asilimia 70 (2/3) vifo vya
watoto wenye umri chini ya miaka 5; na Kupungua kwa vifo vya mama na
mtoto. Mengine ni Kupungua kwa kiwango cha maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI kwa watu wenye umri kati ya miaka 15-24 na 25-49; na Kuongezeka
kwa idadi ya wananchi wanaotumia maji safi na salama ya kunywa. Katibu
mkuu Bibi Nkinga amaeleza kuwa mafanikio haya yamefanikiwa kwa
ushirikiano tahbiti wa AZAKi na Serikali.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa
Foundation For Civil Society Bw. Francis Kiwanga alimjulisha Mgeni
Rasimi kuwa Tamasha la AZAKi 2015 litakuwa na mada nne amabzo ni: Wajibu
na mikakati ya kuimarisha ushiriki wa asasi za kiraia katika
utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu; Wajibu wa Sekta Binafsi
katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu; Wajibu wa Serikali
katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu; na Utunishaji Mfuko
na Ugharamiaji wa Mpango wa Maendeleo endelevu. Rai imezidi kutolewa
kuzingatia upatikanaji wa rasilimali kutoka ndani na nje ya nchi katika
kutekeleza Malengo Endelevu ya Maendeleo.
Katibu Mkuu Nkinga ameongeza kuwa
yeye ni mmoja wa wanaoamini kuwa bila Asasi za Kiraia makini zenye
uzalendo zinazotanguliza maslahi ya taifa hatutaweza kuwa na Tanzania
tunayohitaka miaka ijayo. Hivyo katika mijadala mnatakiwa kuzingatia
wajibu mkubwa wa AZAKi kwa jamii katika kuchangia kufikiwa kwa malengo
ya maendeleo endelevu, tunapaswa kupitia upya dhamira zetu na kuwa
tayari kujifunza kwa wengine ili kuimarisha utendaji wa Asasi zetu na
kutoa mchango unaokusudiwa. Amewasihi kufanyakazi kazi kwa juhudi na
maarifa ili kuunga mkono dhamira ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli
ya kuwawezesha Watanzania kujiletea maendeleo yao na kuondokana na
umasikini kupitia kauli mbiu ya HAPA KAZI TU!
Watendaji wa AZAKI wametakiwa
kuongeza uwazi na uwajibikaji kwa wadau mbalimbali hususan kwa jamii,
serikali, wanachama, wafadhili na makundi maalum. Hapana buni kuwa na
miundo na taratibu zenye uwazi, ushirikishaji na uwajibikaji. Utamaduni
huu ukiendelezwa sio tu kwamba mtajijengea uhalali kwa wananchi na jamii
bali pia AZAKi zitaweza kuimarisha ubia na Serikali katika ngazi zote.
Mwisho, Bibi Sahiba aliwataka
wadau wa Asasi za Kiraia kurejea maneno ya Muasisi wa Taifa Letu Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kutoka katika Kitabu chake cha ‘Uhuru
na Maendeleo’ ambaye aliwahi kusema: “Mtu anaendelea ikiwa uwezo wake
umekua au kipato chake kimeongezeka kumwezesha yeye na familia yake
kuishi maisha bora zaidi; Mtu haendelei kwa kutegemea kupewa vitu na
watu wengine” (1973).
0 comments :
Post a Comment