Mbunge
wa jimbo la Musoma Vijijini ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo ameanza kwa kishindo kutekeleza ahadi zake kwa
wananchi wa jimbo hilo na huku akiahidi maendeleo kwa kasi zaidi.
Profesa
Muhongo alidhihirisha hayo juzi katika kijiji cha Murangi, Mkoani Mara
katika kikao chake na baadhi ya wananchi wa jimbo hilo, watendaji wa
Halmashauri ya Musoma Vijijini na madiwani huku lengo la kikao likiwa ni
kujadili mipango na miradi ya uchumi na maendeleo ya jimbo hilo.
Katika
kikao hicho, iliazimiwa kuanzishwe Mfuko wa Elimu wa Jimbo ambapo
Profesa Muhongo aliahidi kutoa kiasi cha Shilingi Milioni mia moja
ambazo atakopeshwa na Bunge kwa ajili ya kununulia gari.
Alisema
badala ya kununulia gari, fedha hiyo ataiingiza kwenye Mfuko huo ili
kuleta maendeleo kwenye jimbo hilo. “Dhamira yangu ni kuhakikisha jimbo
letu linasongo mbele kiuchumi na kimaendeleo na siyo maneno bila mipango
madhubuti,” alisema.
Mbunge
wa Jimbo la Musoma Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo akizungumza jambo wakati wa kikao chake na wananchi wa
jimbo hilo pamoja na wadau wa maendeleo.
Katika
maelezo yake ya mikakati ya maendeleo kwa jimbo hilo, Profesa Muhongo
alisema kufikia Mwezi Januari mwanzoni, ataanzisha Ofisi tano za Mbunge
jimboni humo ili kufikisha huduma kwa wananchi kiurahisi.
Alisema
Ofisi hizo zitakuwa na mtumishi mmoja ambaye ataajiriwa na Mbunge na
atapatiwa vitendea kazi vya kuanzia ambavyo ni pikipiki ili kumuwezesha
kuwafikia wananchi kirahisi na kompyuta mpakato (laptop) kwa ajili ya
kutunza taarifa na mawasiliano.
Profesa
Muhongo alitaja maeneo ambayo ofisi hizo zitaanzishwa kuwa ni kijiji
cha Murangi ambapo ndio patakua makao makuu, Busekela, Sangana, Mugango
na Nyegine na alitoa wito kwa vijana wa maeneo hayo kuomba kazi kwa
nafasi husika na kwamba watakaofaulu watatakiwa kuwepo maeneo hayo ili
kila watakapohitajika waweze kupatikana kiurahisi.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria Kikao cha Profesa Muhongo (hayupo pichani).
Alisema
usaili wa kuwapata watumishi hao utafanyika tarehe 26 na 27 mwezi huu
na watakaofaulu wataanza kazi tarehe 1 Januari, 2016 kwa uangalizi wa
kipindi cha miezi mitatu (probation period) na alitaja vigezo
vitakavyotumika kwenye kuwapata kuwa ni elimu kuanzia kidato cha nne na
ujuzi wa kompyuta.
Mbali
na hilo, katika kuimarisha elimu jimboni humo, Profesa Muhongo ametoa
vitabu vya kujifunzia vipatavyo 20,000 (elfu ishirini) katika shule
mbalimbali na huku kipaumbele kwa wakati huu ni kwa shule zilizofanya
vibaya kwenye matokeo ya mwaka huu.
Alisema
tayari ameagiza vitabu vingine 22,000 kutoka nchini Marekani na
vitakapoingia nchini ameagiza Madiwani kuvisambaza kwenye shule ambazo
hazina vitabu vya kutosha.
Mbunge
huyo alisema kwa kutumia Mfuko huo wa Elimu wa Jimbo, pamoja na fedha
za Halmashauri, kila shule itapatiwa huduma ya umeme, maji pamoja na
kujenga na kukarabati shule hizo pamoja na nyumba za walimu.
Akizungumzia
suala la miundombinu ya barabara, Mbunge huyo aliahidi kusimamia ujenzi
wake ambapo alisema barabara kutoka Musoma mjini hadi makao makuu ya
jimbo itajengwa kwa kiwango cha lami na alisema tayari tathmini imeanza
na itakamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Mbali
na hilo, kwa barabara zilizo chini ya Halmashauri, Profesa Muhongo
aliagiza madiwani wakae na kupitisha bajeti kwa ajili ya kukarabati
barabara hizo na aliagiza kikao hicho kifanyike kabla mwezi huu
haujamalizika.
Kuhusu
suala la Afya, Profesa Muhongo alisema tayari ameagiza gari la wagonjwa
ambalo linatarajiwa kuingia nchini ndani ya wiki mbili zijazo.
Kikao
hicho cha maendeleo ya jimbo la Musoma vijijini kilihudhuriwa na wadau
mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi miongoni mwao kukiwa
na wazawa wa jimboni humo ambao kwa sasa wanaishi nje ya jimbo hilo na
wageni kutoka Ujerumani.
0 comments :
Post a Comment