Ndugu zangu, Kwa niaba ya
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania kupitia kwenu wanahabari ninaomba
nitoe salam za mwaka za Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania TFF.
Awali ya yote tumshukuru Mwenyezi
Mungu ambaye ametulinda kwa mwaka mzima na kupitia Baraka zake tumeweza
kuwa na nguvu, uwezo na hekima za kutimiza majukumu yetu
mbalimbali
katika kipindi hiki cha mwaka 2015. Tuzidi kumuomba atuvushe salama
mwaka 2015.
Ninaomba nichukue fursa hii
kuwapongeza Watanzania wenzangu kwa kukamilisha mchakato wa uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015. Ninampongeza Mh. Dr John Pombe Magufuli kwa
kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hongera sana
Mama Samia Suluhu kwa kuwa Makamu wa Rais na hongera kwa mwanamichezo
mwenzetu Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa kwa kushinda ubunge jimbo
la Ruangwa na kwa uteuzi wa kuwa Waziri wetu Mkuu. Hongera za kipekee
kwa Mheshimiwa Nape Nnauye kwa uteuzi wa kuwa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo na hongera pia kwa Mama Anastasia Wambura
kwa kuteuliwa kuwa naibu waziri wa wizara hii muhimu kwa mustakabali wa
afya na ajira kwa vijana na utangazaji wa jina la Nchi yetu ya Tanzania
nje ya mipaka ya nchi. Ninashukuru Mh. Waziri Nnauye majuzi alinipatia
fursa ya kuwa mmoja wa viongozi wa kwanza wa vyama vya Kitaifa vya
michezo ya kukutana naye na kujitambulisha rasmi kwake, ahsante sana.
Ndugu zangu, Shirikisho la mpira
wa miguu Tanzania lipo kwa ajili ya kuendeleza na kusimamia mpira wa
miguu Tanzania. Tunafanya hivyo kwa niaba ya Watanzania wote wapenzi wa
mpira wa miguu. Kwa kutambua uzito na umuhimu wa jukumu hili ndio maana
wakati wote TFF inafanya jitihada za dhati kuhakikisha timu zetu za
Taifa zinafanya vizuri. Kwa sasa tunazo timu za Taifa kumi ambazo ni za
soka la ufukweni wanawake na wanaume, umri chini ya miaka 17 wanawake na
wanaume, umri chini ya miaka 20 wanawake na wanaume, umri chini ya
miaka 23 wanawake na wanaume na mbili za wakubwa za wanawake na
wanaume. Katika kuingiza timu kwenye mashindano ya kimataifa tumekuwa
tukizingatia vigezo kadhaa lakini kikubwa ikiwa ni utayari wa timu
kushiriki mashindano na uwezo wa kugharamia mchezo wenyewe. Kwa wastani
gharama za kushiriki mkondo mmoja wa mechi ya Kimataifa kwa kucheza
nyumbani na ugenini ni takribani shilingi million mia moja (USD
50,000.-), hii inajumuisha gharama za kambi, usafiri kwenda ugenini,
posho, nauli na posho za waamuzi na kamisaa, malazi ya waamuzi na
kamisaa nk. Kwa kuwa timu yenye udhamini kwa sasa ni timu ya Taifa
wanaume tuu hivyo TFF imekuwa inabeba yenyewe gharama nyingine zote kwa
timu zote zilizobakia. Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utashuhudia
ufadhili unapatikana kwa timu zetu nyingine za Taifa.
Ninaomba sasa nichukue fursa hii kuzungumzia maeneo kadhaa ambayo yamehusu mpira wetu na taasisi yetu kwa mwaka 2015:
1. Timu ya Taifa ya wanaume “Taifa Stars”
Baada ya timu yetu ya Taifa,
Taifa Stars kutofanya vizuri katika michuano ya COSAFA huko Afrika
Kusini mwezi Mei mwaka huu na baadae kufuatia kufanya vibaya katika
mchezo wa kwanza katika mtoano wa mashindano ya CHAN, Kamati ya Utendaji
ya TFF ilichukua maamuzi ya kusimamisha ajira ya kocha wa kigeni Martin
Nooj na badala yake kuingia mkataba na makocha wazawa Boniface Charles
Mkwasa akisaidiana na Hemed Morocco. Tangu walimu hawa wamechukua timu
ya Taifa Stars tumefungwa mechi mbili tuu za mashindano dhidi ya Algeria
na Malawi ugenini, tumetoka sare na Uganda ugenini, tumetoka sare na
Nigeria na Algeria nyumbani na kuwafunga Malawi nyumbani. Aidha timu ya
Kilimanjaro Stars chini ya kocha Abdalla Kibadeni na msaidizi wake Juma
Mgunda katika mashindano ya CECAFA Challenge katika mechi nne
ilizocheza Ethiopia haikufungwa hata mechi moja kwa muda wa mchezo (Open
Play) ingawa ilitolewa kwa penati tano tano katika hatua ya nusu
fainali. Katika mashindano hayo Taifa Stars ilishinda mechi mbili na
kutoka sare mbili. Kipindi chote ambacho tumekuwa na makocha hawa wazawa
kiwango cha Tanzania FIFA kimekuwa kikipanda mara zote. Tunawapongeza
sana makocha wetu hawa na benchi zima la ufundi. Kwa sasa tunajiandaa na
mechi mbali mbali za kufuzu kucheza fainali za Afrika Afcon 2017 nchini
Gabon. Mechi hizi ni dhidi ya Tchad tarehe 25/03/2016 ugenini Ndjadema
na mechi ya marudiano siku tatu baadae hapa Dar es Salaam tarehe
28/03/2015. Imani yetu ni kuwa timu yetu itaendeleza wimbi la ushindi.
Katika kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Nigeria, Taifa Stars iliweka
kambi nchini Uturuki na pia timu iliweka kambi Afrika Kusini kujiandaa
na mechi dhidi ya Algeria. Kambi hizi zimesaidia sana kuimarisha timu
yetu kabla ya mechi hizi kubwa mbili. Katika kujiandaa na mechi dhidi ya
Tchadi mwezi Machi mwakani ratiba ya ligi kuu ikiruhusu timu itaweka
kambi pia nje ya nchi.
2. Timu ya Taifa Wanawake “Twiga Stars”.
Timu yetu ya Taifa ya wanawake
Twiga Stars chini ya kocha Rogasian Kaijage ilifanikiwa kuiondoa Zambia
na hivyo kufuzu fainali za michezo ya Afrika Kusini Kongo Brazaville.
Katika fainali hizi Tanzania ilifungwa na Ivory Coast na Nigeria na
kutoka sare na Congo, hivyo kutolewa kaika hatua za makundi. Tunaamini
uzoefu uliopatikana katika mashindano hayo utaimarisha timu na kufanya
Twiga Stars iweze kushiriki fainali ya Afrika ya mpira wa wanawake
nchini Cameroon mwaka 2016.
Hatua ya awali Tanzania
itapambana na Zimbabwe mwezi Machi 2016 na mshindi wa michezo huo
atacheza hatua ya pili dhidi ya mshindi kati ya Namibia na Zambia.
3. Udhamini na michuano mipya.
Kwa kipindi hiki cha mwaka 2015 tumefanikiwa katika maeneo yafuatayo:
3.1 Kufufua Kombe la Shirikisho Azam Sports Federation Cup.
Kwa kushirikiana na mdhamini Azam
Sports Kombe la Shirikisho limefufuliwa na kuboreshwa. Kwa mwaka huu
tumeanza na timu 64 ambazo ni za ligi kuu (16), Ligi daraja la kwanza
FDL (24) na Ligi daraja la pili SDL (24). Ili kupanua uwigo wa ushiriki
wa Mikoa yote kwa misimu ya usoni timu mabingwa wa mikoa (RCL) nazo
zitashirikishwa katika mashindano haya ili kila mkoa wa Tanzania upate
fursa ya kushiriki katika mashindano haya. Fainali itachezwa mwezi Mei
na bingwa wa Kombe hili ataiwakilisha Tanzania katika kombe la
Shirikisho la Afrika CAF Confederation Cup.
3.2 Udhamini Ligi daraja la kwanza.
Tumefanikiwa kupata wadhamini
wawili kwa ligi daraja la kwanza FDL. Tumempata STARTIMES ambayo ni
mdhamini mkuu wa ligi na pia kampuni ya Television ya Sahara Media
kupitia STAR TV imepewa haki za kuonyesha mechi hizi moja kwa moja. Haya
ni mafanikio makubwa kwa ligi ya daraja la kwanza. Tunaishukuru kampuni
ya Geita Gold kwa kuidhamini timu ya daraja la kwanza ya Geita Gold
Sport na tunazidi kutoa wito kwa washirika wengine wazidi kujitokeza
kudhamini timu zetu.
3.3 Mkataba wa Vodacom na Ligi Kuu.
Kampuni ya Vodacom baada ya
mazungumzo marefu tuliafikiana na kutuliana saini ya mkataba mwingine wa
miaka mitatu wa udhamini wa ligi kuu wenye ongezeko la thamani ya
udhamini kwa asilimia 40%. Jitihada zimefanyika kuvutia wadhamini
wengine nao waje waongeze udhamini kwa ligi kuu. Tunaishukuru kampuni ya
ACACIA ambayo imejitolea kuidhamini klabu ya ligi kuu ya Stand United
haya ni mafanikio makubwa kwa ligi yetu na tunazidi kuvipa moyo vilabu
vizidi kupata wadhamini zaidi. Tunayashukuru sana makampuni yote ambayo
yamejitokeza kudhamini vilabu mbali mbali na tunazidi kutoa wito kwa
makampuni mengine yajitokeze kutoa udhamini ikiwa ni sehemu ya kutangaza
biashara na kukuza jina la chapa zao.
3.4 Udhamini tarajiwa.
Tunatarajia kupata wadhamini kwa
ajili ya Ligi Kuu ya vilabu vya wanawake (Women Premier League) pamoja
na ligi kya vilabu vya ligi kuu ya vijana chini ya umri wa miaka 20
(U-20).
Jambo hili likifanikiwa matumaini
yetu ni kuwa tutaanzisha ligi mpya mbili mwaka 2016, Ligi ya vilabu vya
wanawake (Women Premier League) na ligi ya vilabu vya ligi kuu ya
vijana umri chini ya miaka 20 (U-20). Mechi hizi nazo zitakuwa
zinaonyeshwa moja kwa moja kwenye television.
Kwa matarajio haya sasa ni vyema
uongozi wa kila mkoa kufanya jitihada za kuhakikisha vilabu vya mpira
vya wanawake vinaanzishwa ili tuweze kuwa na ligi ya ushindani.
Ninaomba nichukue fursa hii
kuwashukuru washirika wetu wote, ambao kama sio kujitolea kwa haya
mafanikio tusingeweza kuyafikia/kuyapata.
Ahsante Kampuni ya Bia Tanzania kwa kupitia bia ya Kilimanjaro Lager.
Ahsante Vodacom.
Ahsante Azam Tv kwa kupitia channel ya Azam Sports HD.
Ahsante Startimes Media kwa kupitia king’amuzi cha STARTIMES.
Ahsante Sahara Media kwa kupitia Star Tv.
Ahsante AIRTEL kwa kutuletea Airtel Raising Star kwa mara nyingine mwaka huu.
Ahsante Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya NHIF.
4. Soka la Vijana.
4.1 Fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17 (U-17) mwaka 2017 Madagascar.
Kikosi chetu cha Taifa cha vijana
chini ya umri wa miaka 17 (U-17) kinachojiandaa na hatua za mtoano
mwezi Juni, 2016 ilikuwa kifanye ziara ya kimichezo katika nchi za
Rwanda, Uganda na Kenya, lengo ilikuwa kuwapatia vijana hao uzoefu wa
Kimataifa. Wakati tayari kikosi kimejiandaa na kukabidhiwa bendera,
akaunti za TFF zilifungiwa na mamlaka za mapato TRA na hivyo safari
kuvunjika kwa ukosefu wa fedha. Mpango mkakati ni kuwa mwezi Aprili,
2016 timu hii itaweka kambi nje ya nchi ili kujiandaa na hatua ya mtoano
(qualifiers).
4.2 Fainali za Afrika U-17 mwaka 2019.
Maandalizi ya fainali hizi ambazo
Tanzania itakuwa mwenyeji yanaendelea vizuri vikao na Wizara tayari
vimeanza kwa ajili ya kufanya maandalizi muhimu ya awali ya Tanzania
kuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Pia maandalizi ya timu itakayoshiriki
fainali hizi yameanza kwa vijana umri chini ya miaka 13 (U-13)
kujumuishwa pamoja katika shule ya Alliance jijini Mwanza. Imani yetu ni
kuwa Tanzania tutafanikiwa kuandaa mashindano mazuri mwaka 2019 na pia
kunyakua kombe hili.
4.3 Vituo vya mikoa vya kukuza na kuendeleza vipaji.
Azma ya TFF ni kuhakikisha kuwa
kila chama cha mpira wa miguu cha mkoa kinakuwa na kituo mama cha kukuza
na kuendeleza vipaji vya mpira. Mkataba wa mfano (template) umekwisha
pelekwa katika kila mkoa ili vyama vya mkoa ambavyo havina vituo vyake
basi viingie mkataba wa ushirikiano na kituo kimoja kwa lengo la
kukifanya kiwe kituo mama cha mkoa. Kupitia vituo hivi TFF itaweza
kuratibu shughuli za maendeleo ya mpira wa vijana katika mikoa yetu,
kuongeza nguvu kwa kuvipatia vifaa na walimu. Mipira 5,000 ya 3 na 4 ya
ukubwa (size), koni 3,000, beeps 2,000 tayari vimeagizwa toka nje ya
nchi kwa kutumia vyanzo vya fedha vya TFF yenyewe bila kuomba msaada
kutoka popote kwa ajili ya kuendeleza program hii. Tayari kila mkoa una
mwalimu angalau mmoja aliyefanya kozi ya FIFA ya ukocha wa vijana
isipokuwa mikoa miwili tu ya Manyara na Njombe, jitihada zitafanyika nao
wapate walimu stahiki. Hivyo mtaji wa kutosha tunao wa kuanzisha vituo
hivi. Pindi vituo hivi vikiimarika yataanzishwa mashindano ya kiumri
(age categories) baina ya vituo hivi kuanzia ngazi ya mkoa, kanda na
hatimaye Taifa. Ninatoa wito kwa viongozi wenzangu wa mikoa tujizatiti
tuweke nguvu katika uwanzishwaji na uendelezaji wa vituo hivi ambavyo
vitakuwa chachu kuu ya kutoa wachezaji wa Taifa wa kike na wakiume.
Baada ya mazungumzo haya nitawakabidhi viongozi wa vyama vya mpira vya
mkoa wa Manyara na Dar es Salaam mpira mmoja mmoja ikiwa ni ishara ya
kuanzishwa rasmi kwa program hii ya kitaifa.
5. Kozi mbalimbali.
Kwa kushirikiana na CAF na FIFA
Shirikisho letu limeandaa, kuratibu na kutoa kozi mbali mbali za waamuzi
na makocha katika ngazi mbalimbali. Jitihada kubwa zimefanyika
kuhakikisha mikoa iliyokuwa na hazina ndogo ya makocha na waamuzi
inapewa fursa ya kuratibu kozi hizi. Tunashukuru viongozi wote wa mikoa
na wilaya ambao tumeshirikiana nao kutimiza azma hii. Juhudi zinaendelea
ili tuweze kupata makocha, waamuzi, madaktari wa michezo na watawala
zaidi. Ninaomba tuwape moyo wakina mama wazidi kujitokeza kwa wingi
kufanya kozi hizi maana wao ndio nguzo kuu ya kuendeleza mpira wa
wanawake nchini mwetu. Ninatoa rai kwa waajiri, hasa wakurugenzi wa
Halmashauri ambao ni waajiri wa walimu wanaofundisha mpira mashuleni,
wazidi kutupatia ushirikiano kwa kutoa ruhusa kwa waajiriwa wao pindi
wanapoomba kuhudhuria kozi mbalimbali zitolewazo na TFF.
6. Bodi ya Ligi na Vilabu.
Utendaji katika bodi yetu
umeimarishwa kwa kutoa ajira kwa mtendaji mkuu Ndugu Boniface Wambura.
Mipango ya kuimarisha sekretariet ya Bodi ikiwa ni pamoja na kupata
nafasi kubwa zaidi ya kufanyia kazi iko mbioni. Matarajio yetu ni kuwa
chombo hiki kikiweza kuimarika kitakuwa ni chachu ya kuandaa ligi zilizo
bora zaidi na zenye ushindani.
Pamoja na jitihada za kutafuta
wadhamini wa mashindano mbalimbali yanayohusisha vilabu, jitihada pia
zinaendelea kufanyika kuhakikisha vilabu vyetu vinaimarisha utawala
bora. Kufuatia CAF na FIFA kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni kwa
vilabu (Club Licencing) jitihada sasa zinafanyika kuhakikisha vilabu
vinaelimishwa kwa kina juu ya mahitaji ya leseni hizi. Katika utaratibu
wa leseni za vilabu, vilabu vyetu sasa vitalazimika kuwa na ofisi,
watendaji wa kuajiriwa, kuwa na maeneo ya kufanyia mazoezi, kuwa na
program ya maendeleo ya vijana, kuajiri walimu wenye sifa n.k. Tunaamini
utaratibu wa leseni za vilabu ukitekelezwa ipasavyo uendeshaji wa
vilabu vyetu utaboreshwa na hivyo kuongeza tija kwa vilabu vyetu.
7. Tiketi za Eletroniki.
Kutokana na matatizo
yaliyojitokeza matumizi ya tiketi za eletroniki yalisimamishwa na
mmiliki wa uwanja wa Taifa ambaye ni Serikali. Baada ya mazungumzo na
mtoa huduma ambaye ni Benki ya CRDB ilikubaliwa atafutwe mshauri
mwelekezi (Consultant) kwa kupitia mfumo mzima ili kubaini matatizo na
baadae kutoa ushauri wa namna ya kuboresha mfumo huo. Tenda ya kumpata
mshauri huyu ilikwishatangazwa na kinachofuatia ni TFF kwa kushirikiana
na CRDB kuteua mshauri huyo. Imani yetu ni kuwa kazi ya mshauri
ikikamilika basi mwongozo utapatikana ili utekelezaji wa uboreshaji wa
mfumo ukamilike na matumizi ya tiketi za eletroniki yaweze kuendelea.
8. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira (Football Development Fund).
Baada ya mfuko huu kuanzishwa
kikatiba katika mkutano mkuu uliopita, kamati ya utendaji ya TFF iliteua
wajumbe wa kamisheni ya uendeshaji wa mfuko huu chini ya Mwenyekiti
Ndugu Tido Mhando na Mtendaji Mkuu Henry Tandau. Mfuko huu tayari
umefanikiwa kupata ofisi yake na shughuli zake zitaanza punde baada ya
kuwekewa vitendea kazi. Lengo la mfuko huu kama ilivyoanishwa ni kuwa
chanzo kikuu cha kupata rasilimali kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa
miguu nchini mwetu. Ninaomba tuwaunge mkono na kuwapa ushirikiano
watendaji wa mfuko huu huku tukitambua kuwa maendeleo ya mpira
yanahitaji rasilimali nyingi.
9. Kufungiwa akaunti za TFF.
Kutokana na madeni ambayo
yamekuwa kwenye mafaili ya mamlaka ya mapato kwa kipindi karibia miaka
mitano iliyopita, mamlaka ya mapato nchini TRA iliamua kuzifungia
akaunti zetu na pesa yote kuhamishiwa Benki kuu. Mazungumzo yanaendelea
kati ya TFF, Mamlaka ya mapato na Wizara husika ili fedha hizi ziweze
kurudishwa. Tunaushukuru uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo ambao wametusaidia kutuongoza namna ya kukabiliana na
changamoto hii.
OMBI KWA SERIKALI.
Duniani kote, iwe katika nchi
tajiri au maskini, michezo huendelezwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya
Serikali na taasisi zinazoendesha shughuli za michezo husika. Tunaiomba
serikali tuzidi kushirikiana kwa karibu katika kuandaa timu zetu za
Taifa, kuboresha miundo mbinu ya kuchezea mpira, kusaidia upatikanaji wa
vifaa vya michezo kwa gharama nafuu, kuto fursa kwa waajiriwa wake,
hasa walimu, wafanye kozi mbalimbali za ukocha na uamuzi. TFF
itafarikika sana iwapo itapewa fursa na Serikali ya kuratibu na
kusimamia mpira wa miguu katika mashindano ya Taifa ya shule za msingi
(UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA). Tunaamini TFF ikipewa fursa hiyo
itaongeza uweledi katika usimamizi wa mashindano hayo na kuhakikisha
vipaji vinaibuliwa kila mwaka kuliko ilivyo sasa.
Ndugu zangu, wakati tunauaga
mwaka 2015 na kuelekea kuingia mwaka 2016 ninaomba nimalizie kwa kutoa
wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania tuzidi kushirikiana,
penye makosa tukosoane japo kwa staha na penye kuhitaji ushauri
tushauriane.
Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utakuwa ni mwaka wa mafanikio kwa mpira wetu.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Ibariki Afrika.
Ahsanteni,
Jamal Malinzi
Rais wa TFF
Dar es Salaam.
30 Desemba, 2015.
0 comments :
Post a Comment