Nkupamah media




Serikali
imewataka wananchi waliojenga nyumba zao ndani ya soko la Tandale
ambalo lipo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es salaam kuzibomoa na
kuacha mipaka yote ya soko hilo wazi, na imewapa siku saba kufanya hivyo
kabla ya majengo hayo kubomolewa.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa
George Simbachawene ameyasema hayo tarehe 22 Desemba wakati alipofanya
ziara yake katika Manispaa tatu za jiji la Dar es salaam kwa ajili ya
kujionea hali ya usafi katika Manispaa hizo.
Akihitimisha
ziara yake katika soko la Tandale, Waziri Simbachawene licha ya
kuridhishwa na hali ya usafi katika maeneo mengi ya jiji la Dar es
salaam, alisema mipaka yote ya masoko nchini yanapaswa yawe wazi ama
sivyo serikali itachukua hatua ya kuyabomoa majengo hayo.
“Wale
wote waliotumia njia za ujanja ujanja kuharibu master plan za mipaka ya
masoko nyumba zao tutazivunja na tutakutana mahakamani,”alisema.
Alisema
kuwa hatua hiyo ni muhimu ifanyike ili serikali iweze kuruhusu miradi
ya maendeleo ifanyike katika maeneo hayo ya masoko na kuongeza kuwa kwa
hali ilivyo sasa ni vigumu kwa wafadhili wa miradi kama benki ya dunia
kusaidia uimarishaji wa miundombinu ya soko hilo.
Aidha
Waziri Simbachawene aliwapongeza wakazi wa jiji la Dar es salaam kwa
namna walivyoshiriki katika kufanikisha zoezi la kufanya usafi wa
mazingira katika maeneo yao na hivyo kuitikia vyema wito wa Rais wa
jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Magufuli.
Aliwataka
wananchi wote kuuenndeleza utamaduni huu wa kufanya usafi mara kwa mara
na kwamba serikali kwa upande wake itahakikisha kuwa inaandaa mpango wa
muda mfupi na mpango wa muda mrefu wa uzoaji taka katika makazi ya
watu.
Alisema
moja ya mikakati ya muda mfupi ni kuhakikisha kuwa taka zinazokusanywa
hazikai muda mrefu katika makazi ya watu na kwamba ameziagiza
halmashauri kuhakikisha kuwa zinaandaa utaratibu maalum kwa magari ya
kuzoa taka yawe yanafanya zoezi hilo usiku.
Waziri
simbachawene alisema mpango huo utarahisisha uzoaji taka kwa wingi na
kwa haraka kwani usiku hakuna msongamano mkubwa wa magari kama ilivyo
mchana na kwamba hatua hiyo itapunguza gharama na pia kuyawezesha magari
hayo kufanya safari nyingi zaidi za kutupa taka hizo katika maeneo
yaliyotengwa.
Alisema
ili kurahisisha zoezi hilo kila mtaa unapaswa kutenga maeneo maalum
ambayo wananchi watahifadhi taka hizo na pia kuchukuliwa kwa urahisi na
magari ya kuzoa taka.
Waziri
Simbachawene aliongeza kuwa ni wajibu wa kila mkazi katika familia
kuhakikisha anazihifadhi taka katika eneo lililotengwa ili kutoleta
bughudha kwa wakazi wengine.
Pia
aligusia uwezekano wa serikali kuchukua hatua ya kupiga marufuku
utengenezwaji wa mifuko ya plastiki maarufu kama Rambo kwani mifuko hii
inachangia kwa kiasi kikubwa uchafu katika miji na hasa kwa kuzingatia
kuwa mifuko hiyo haiozi na imekuwa kero kubwa kwa wananchi.
Alisema
hata katika zoezi la usafi lililofanyika wakati wa sherehe za uhuru
tarehe 9 desemba ilidhihirika kuwa mifuko ya plastiki kwa kiasi kikubwa
ndiyo chanzo kikuu cha uchafu katika maeneo mengi nchini hasa mijini.
Mbali
na mifuko ya plastiki, chanzo kingine kikuu cha uchafu hasa katika
masoko yaliyopo mijini ni majani yanayotumika kwa ajili ya kufungashia
matenga ya nyanya au ndizi, ambapo Mheshimiwa Simbachawene aliagiza kuwa
kuanzia sasa gari itakayoleta bidhaa hizo ikiwa na vifungashio hivyo
haina budi kubeba uchafu huo ili kupunguza ongezeko la uchafu sokoni.
Katika
ziara hiyo, Waziri Simbachawene aliongozana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam Mhe. Saidi Meck Sadiki,na alitembelea masoko ya Temeke Sterio, na
Tandika katika Manispaa ya Temeke, Buguruni katika Manispaa ya Ilala na
Tandale katika Manispaa ya Kinondoni.
Waziri Simbachawene akizungumza na Wafanyabiashara na Viongozi wa Manispaa ya Temeke katika Soko la Temeke Sterio.
Mwenyekiti
wa Wafanyabiashara wa soko la Buguruni bwana Said Habibu kondo
akimweleza Waziri Simbachawene hali ya usafi na changamoto mbalimbali za
soko hilo
Waziri Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari katika soko la Tandale mara baada ya kuhitimisha ziara yake.
0 comments :
Post a Comment