Tuesday, December 1, 2015
Watendaji
wa mashirika ya ndege nchini wameiomba Serikali kupanua Barabara ya
Nyerere ili kuwawezesha abiria wanaosafiri kwa ndege kuwahi usafiri
kufuatia ongezeko lao kubwa na la ndege pia linalotarajiwa kufuatia
kuwepo kwa jengo jipya la abiria (TB III) linalotarajiwa kukamilika
mwaka 2016.
Rai
hiyo imetolewa jana na watendaji wa mashirika 19 ya ndege yanayoendesha
shughuli zake katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere
(JNIA) walipozuru ujenzi TB III ikiwa ni moja ya ziara za wadau
zinazoandaliwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Baadhi ya CEOs wa mashirika ya ndege wakitoka kutembelea TB III (nyuma yao) jana JNIA.
Akijibu
rai hiyo, Mkurugenzi wa Mradi wa TB III, Mhandisi Mohammed Millanga
amesema, wameipokea kama changamoto lakini tayari walishawasiliana na
mamlaka husika kuomba kuboreshwa kwa usafiri kwenda JNIA lakini jibu
walilopata halioneshi suluhisho la haraka.
“Tuliwasiliana
na Wakala wa Barabara (TANROADS) na Shirika la ReliTanzania (RAHCO).
RAHCO walisema hawana mpango wowote kuhusu eneo hili. Wakala wa Mabasi
ya Mwendo Kasi (DARTS) wao wameiweka Barabara ya Nyerere katika awamu ya
tatu ya mradi wao. “amesema.
Mmoja
wa CEOs akimwonesha Mhandisi Carloline Ntambo wa Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege Tanzania (TAA) inayojenga TB III, eneo ambalo wangependa kufanyia
shughuli zao za huduma kwa abiria wa ndege.
Mhandisi
Millanga amesema, katika kuhakikisha hakuna tatizo hilo, TAA
iliwasiliana na wawekezaji wa treni ya juu kutoka Afrika Kusini lakini
mpango huo haujazaa matunda. Hata hivyo, amesema, anaamini Serikali ya
awamu ya tano itapata suluhisho la tatizo hilo mapema.
Watendaji
hao walitaka kujua TAA imejiandaaje kukabiliana na foleni kubwa ya
magari Jijini kuanzia eneo la TAZARA ili abiria wasichelewe ndege
kufutia kuongezeka kwa abiria wakati TB III itakayokuwa na uwezo wa
kuchukua abiria milioni sita kwa mwaka, itakapoanza kazi 2016.
Pamoja
na changamoto hiyo, watendaji hao waliipongeza TAA kwa kujenga TB III
kwa wakati muafaka na kueleza matumaini yao kuwa maeneo mengi ya
miundombinu ya usafiri wa anga inayotakiwa kuwekwa TB III kwa ajili yao
kama maofisi, maeneo ya biashara yatawekwa pia.
Watendaji
hao walitaka kujua idadi ya ofisi za mashirika ya ndege na wakala wa
huduma za usafiri wa anga,idadi ya kaunta za kuhudumia abiria, maeneo ya
maofisa Uhamiaji, Usalama, Forodha, mizigo, ukatishaji tiketi,
uunganishaji safari na mwingiliano wa TB III na TB II,
Pia
walitaka kujua uwezo wa maegesho ya magari, ndege, biashara za maduka
ya bidhaa zisizolipiwa ushuru, mahoteli, biashara ya magari ya kukodi na
teksi, kituo cha ujazaji mafuta katika ndege na anayekiendesha, uhakika
wa umeme, mfumo wa usalama wa abiria na mizigo.
Mhandisi
Millanga amewaambia TAA imezingatia mahitaji mengi muhimu TB III
ikiwemo kutenga maeneo ya abiria kusali, watoto kucheza na kuoga, sehemu
za abiria na wafanyakazi kula, huduma za benki, jenereta la dharura la
KV 33, umeme na mifumo mtambuka ya usalama.
Amesema
wameweka mfumo mzuri kuzuia majanga ya moto na kutakuwa na mwingiliano
wa mfumo wa usalama kati ya TB III na TB II na ndege za mashirika yote
zitaruhusiwa kunywa mafuta katika kisima kinachojengwa na kuendeshwa na
Puma Energy iliyopewa zabuni hiyo.
Pia
amesema, awamu ya kwanza ya TB III inayochukua abiria milioni 3.5
itakamilika Juni 2016 na ya pili Desemba 2017 ambapo TB II itafanyiwa
ukarabati mkubwa kwa fedha zitakazotolewa na Ufaransa iliyolijenga mwaka
1984 likiwa na uwezo kuchukua abiria milioni 1.5 ( sasa 2.5m).
Hivi
sasa TB III imekamilika kwa asilimia 65. Tayari wadau mbalimbali
wametembelea ujenzi huo. Watendaji waliotembelea leo walitoka katika
mashirika ya ndege ya Swissair, Oman Air, Air Seychelles, Mauritius Air,
Fly Dubai, ATCL, South African Airways, Qatar Airways, Emirates n.k.
Mkuu
wa Idara ya Masoko TAA, Ndugu Scolastica Mukajanga akiwaelekeza baadhi
ya CEOs , maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za mashirika yao TB
III walipotembelea jengo hilo jana.
CEOs wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kutembelea TB III
Mkurugenzi
wa Mradi wa ujenzi wa jengo la tatu (TB III) la abiria katika Kiwanja
cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Mhandisi Mohammed
Millanga akitoa taarifa kwa Watendaji Wakuu (CEOs) wa Mashirika ya Ndege
kuhusu ujenzi wa TB III unavyoendelea walipotembelea jengo hilo jana.
Baadhi ya CEOs wakiangalia dari la TB III walipotembelea jengo hilo jana JNIA.
0 comments :
Post a Comment