Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais-TAMISEMI Mhe. George Simbachawene amemuagiza Mkurugenzi wa Manispaa
ya Dodoma kuwasimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa
ya Dodoma Bw. Elias N. Kamara na Bibi Donatila D. Vedasto (Afisa
Biashara) kuanzia jana tarehe 30/12/2015 kwa kosa la kusababisha urasimu
katika
utoaji wa leseni za biashara.
Kutokana na hali
hiyo Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI amemuagiza Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma kumuondoa kwenye nafasi yake Kaimu
Afisa Biashara wa Manispaa na Msaidizi wake na nafasi zao kukaimishwa
kwa watu wengine ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizotolewa
dhidi yao.
Agizo hili limetolewa na Mhe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI baada ya kupokea malalamiko mengi
kutoka kwa wafanyabiashara ambayo yalionyesha kuwepo kwa mazingira ya
rushwa.
Katika uchunguzi ambao umefanyika
katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imegundulika kuwa kulikuwa na
maombi ya leseni 750 ambayo yalikuwa hayajashughulikiwa bila sababu za
msingi na hali hiyo ilipelekea kuikosesha Halmashauri ya Manispaa ya
Dodoma kiasi cha shilingi Milioni 75.
Aidha, Mhe. Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Rais – TAMISEMI ameagiza Mamlaka za Serikali kote nchini kuhakikisha
wanatoa leseni za biashara bila urasimu wowote na muombaji apate leseni
ndani ya siku 2 au 3 anapoomba leseni.
Mhe. Simbachawene ametoa agizo
kwa Maafisa biashara wote nchini kuacha urasimu katika kutoa leseni na
kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Imetolewa na:
Rebecca Kwandu
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais – TAMISEMI
30 Desemba, 2015
0 comments :
Post a Comment