Na Benedict Liwenga-Maelezo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Hamis Kigwangala leo
amemtembelea na kumjulia hali Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar
es Salaam, Mwadhama Kadinali Polycarp Pengo aliyelazwa katika Taasisi ya
Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
jijini Dar es Salaam.
Akiongelea kuhusu hali ya
Kadinali Pengo, Mhe. Kigwangala alisema kuwa Kadinali Pengo yuko salama
katika mikono ya madaktari wa taasisi hiyo na hali yake inaendelea
vizuri ambapo ameweza kuongea nae ana kwa ana kiasi cha kuweza kukaa na
kuongea.
‘’Manzoni alilazwa katika
Hospitali ya TMJ iliyopo hapa jijini Dar es Salaam, lakini ikaonekana ni
vema akiletwa hapa kwenye Hospitali yetu hii ya juu kabisa ya matibabu
ya moyo (Tasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete), hivyo napenda kuwapa taarifa
Watanzania kwamba yuko salama kabisa katika mikono ya madaktari wetu na
hali yake inaendelea vizuri.’’
Awali Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli akiongozana na Mkewe mama
Janeth Magufuli walienda pia kumjulia hali Kadinali Pengo katika
taasisi hiyo na kumtakia afya njema ili aweze kuendelea na shughuli zake
za kiroho.
Kadinali Pengo alifikishwa
katika taasisi hiyo ya moyo kwa ajili ya kuchunguzwa afya yake ambapo
afya yake kwa sasa imezidi kuimarika.


0 comments :
Post a Comment