Katika
hali isiyokuwa ya kawaida, mwanamke mmoja amepanda katika paa la jengo
la Wizara ya Fedha na Mipango huku tukio hilo likizua sintofahamu kwa
wafanyakazi wa wizara hiyo na wapita njia.
Tukio
hilo lilitokea jana Dar es Salaam majira ya asubuhi ambapo mwanamke
huyo anayedaiwa kuwa raia wa Kenya alipanda juu ya paa hilo na kuanza
kupiga kelele.
Katika
tukio hilo, inadaiwa mwanamke huyo aliwasili katika eneo hilo la wizara
akionekana kama mmoja wa wananchi ambao walikwenda kwa ajili ya
kupatiwa huduma, lakini baada ya muda alionekana akiwa juu ya paa huku
akipiga kelele.
Mwanamke
huyo aliyekuwa amebeba mkoba, ambao haikufahamika mara moja nia yake
ya kupanda juu ya paa hilo, ilimchukua saa kadhaa akiwa juu na pale
walinzi wanaolinda ofisi za wizara hiyo walipokwenda katika eneo hilo na
kumwomba ateremke aligoma.
Hata
hivyo hali hiyo ilionekana kutowakatisha tamaa walinzi hao wanaolinda
majengo ya Wizara ya Fedha na Mipango yaliyopo mita chache kutoka Ikulu
ya Dar e Salaam, ambao walikwenda tena wakiwa na ngazi na kuanza
kumbembeleza ambapo jaribio hilo lilifanikiwa na mwanamke huyo
kuteremka.
Wakati
mwanamke huyo akiwa juu ya paa, wananchi waliokuwa chini walianza
kumuuliza maswali, lakini hakusikika majibu yake kutokana na kelele za
watu ambao kila mmoja aliimuuliza swali lake.
Hata
hivyo mmoja wa askari wa kikosi cha Usalama Barabarani ambaye alisogea
kwa karibu kumuuliza mwanamke huyo, alisema kuwa alimwambia amechukua
uamuzi huo kutokana na kuteswa na askari nchini Kenya.
“Tukio
hili ni la ajabu na linaibua maswali… hivi inakuwaje kwa jengo kama
hili la wizara ambalo lipo jirani na Ikulu mtu anapanda juu na walinzi
wapo?
“Hii
inasikitisha sana na ni ajabu kwa kweli, ipo siku tutakuta watu
wanaingia Ikulu na kufanya mambo ya ajabu kwa viongozi wetu,” alisema mmoja wa wananchi waliokuwa katika eneo hilo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini.
Alipotafutwa
Msemaji wa wizara hiyo, Ingiahedi Mduma ili kuzungumzia suala hilo,
alisema kwa sasa yupo mjini Dodoma katika maandalizi ya vikao vya Bunge
na hana taarifa ya tukio hilo.
Mwanamke
huyo akizungumza na watu waliokusanyika lakini alikuwa hasikiki vizuri
maneno aliyokua akiongea kutokana na wananchi waliokusanyika kumuuliza
maswali mengi kwa wakati mmoja.
Polisi
akiwa pembeni ya uzio wa majengo ya wizara ya fedha na mipango mara
baada ya mwanamke huyo kuwa juu ya paa la nyumba hizo. Baada ya muda
wafanyakazi wa wizara hiyo walimwekea ngazi na kumshusha ili kumhoji
zaidi nini kimemfanya apande juu ya paa la majengo hayo.


0 comments :
Post a Comment