Nkupamah media:
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Mahakama hiyo imesema madai kwamba ilitoa zuio la uchaguzi huo ni
ya uongo na kwamba, zuio lake lilikuwa la uchaguzi uliopangwa awali
kufanyika Februari 8, mwaka huu, ambalo baadaye lilifutwa baada ya
walalamikaji kutoobnekana mahakamani.
Uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ulikuwa ufanyike Februari
27, mwaka huu, lakini uliahirishwa baada ya Kaimu Mkurugenzi wa jiji
aliyekuwa mwenyekiti wa uchaguzi huo, Theresia Mmbando, kusoma kile
alichodai ni zuio la Mahakama ya Kisutu lililokuwa linalenga kusitisha
uchaguzi huo.
Hatua hiyo ya Mmbando ambaye pia ni Katibu Tawala Dar es Salaam,
ilizua sintofahamu iliyosababisha wajumbe wa pande mbili (CCM na wa
kutoka vyama vya CUF na Chadema kwa upande mwingine), kurushiana maneno
hali iliyolazimu polisi waingilie kati kumtoa kiongozi huyo wa serikali
chini ya ulinzi baada ya kupata misukosuko kutoka kwa baadhi ya wajumbe.
Jana Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Warialwande Lema,
alisema siyo kweli kwamba mahakama hiyo imetoa zuio la uchaguzi huo.
“Mahakama ilitoa amri ya zuio la muda Februari 5, mwaka huu la
kuzuia uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 8,mwaka huu … ilipanga
kusikiliza maombi hayo Februari 15 lakini walalamikaji hawakufika
mahakamani,” alisema na kuongeza:
“Mahakama ilipanga tena maombi hayo kusikilizwa Februari 23, mwaka huu lakini pia walalamikaji hawakutokea mahakamani.”
Walalamikaji katika shauri hilo walikuwa ni Susan Massawe na Saad Khimji, dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.
Akiendelea kufafanua, Hakimu Lema alisema baada ya walalamikaji
kushindwa kufika mahakamani kusikiliza maombi yao, mahakama hiyo
ililiondoa maombi ya zuio yaliyokuwa yamewasilishwa mbele yake na
walalamikaji hao pamoja na zuio lililokuwa limetolewa awali.
“Aliyesema mahakama imetoa zuio ni uongo kwa kuwa walitumia amri
ambayo ilipitwa na wakati… sijui chochote kuhusu zuio la Februari 27,
mwaka huu” alisema Hakimu Lema.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mkuu, Mfawidhi Cyprian Mkeha, alisema
baada ya maombi hayo kuondolewa mahakamani hajapokea maombi mengine
kuhusu kuzuia uchaguzi huo.
Februari 27, mwaka huu, Mmbando akisoma zuio alilodai ni la
mahakama alisema: “Nimeshauriana na wanasheria zuio linadumu kati ya
miezi mitatu hadi sita, hivyo tunapaswa kuheshimu sheria za nchi na
Katiba… naahirisha uchaguzi hadi taratibu zitakapokamilika.”
Baada ya kutoa maelezo hayo ilizuka tafrani kubwa wajumbe wa
mkutano huo kutoka vyama vya Chadema na CUF ambao walikuwa wakipinga,
kwa kile walichosema zuio hilo halihusiani na uchaguzi huo.
Akizungumza kwa njia ya simu jana, Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge
na Halmashauri wa Chadema, John Mrema, alisema wanashukuru mahakama
kujitoa kwenye madai ya uongo dhidi yao.
“Ukweli uliotolewa na mahakama unaonyesha ni jinsi gani mhimili huo
uko makini kusimamia majukumu na kuwaongezea wananchi imani kwamba
hakuna aliye juu ya sheria,” alisema na kuongeza:
“Namuomba Rais John Magufuli kuingilia kati suala hili ili uchaguzi
wa meya ufanyike jiji liweze kuendelea na shughuli wake kwa mujibu wa
taratibu za nchi yetu.”
Mrema alidai kuna mipango ya siri ya kuzuia uchaguzi huo usifanyike
kwa kuwa baadhi ya madiwani pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee
wanashikiliwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mmbando alipopigiwa simu na gazeti hili, alisema yuko hospitali ni mgonjwa hawezi kufanya mahojiano.
“Niko hospitali naumwa siwezi kufanya mahojiano…” alisema Mmbando.
0 comments :
Post a Comment