Serikali yatangaza 31 Oktoba 2017 Mwisho wa kudai malimbikizo ya mishahara

Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuanzia tarehe 31 Oktoba, 2017 imeelekeza madai ya malimbikizo ya mishahara ya Watumishi wa Umma kwa kujaza fomu za madai kufikia ukomo. Maafisa Utumishi wanatakiwa kupokea na kujaza madai hayo kupitia Mfumo wa Taarifa Shirikishi za Kiutumishi na Mishahara.
Waziri Kairuki (Mb) amesema hayo jana katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Tarafa ya Ukonga, kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa shule ya Sekondari ya Pugu, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kairuki amesema katika kikao kilichowakutanisha watumishi wa umma kutoka kata 13 za Ukonga kuwa kumekuwa na adha kubwa ya mlundikano wa makaratasi ambao umekua ukichelewesha watumishi wa umma kupata haki zao kwa wakati kwa kupitia hatua mbalimbali, hivyo kuanzia tarehe 31 Oktoba, 2017 kila hatua itafanyika kielektroniki ili kuleta mabadiliko na kuboresha utendaji kazi.
“Nawaagiza waajiri kupitia kwa Maafisa Utumishi kuingiza taarifa za malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma kwa usahihi ili mfumo uweze kukokotoa moja kwa moja na malipo kufanyika haraka” Mhe. Kairuki amesema.
Ameongeza kuwa Maafisa Utumishi wawe makini katika kupokea na kujaza taarifa za watumishi wa umma katika mfumo, pia watumishi nao watoe ushirikiano wa dhati katika kuweka kumbukumbu za taarifa zao ili wapate haki yao inavyostahili.
Aidha, Waziri Kairuki amesema Serikali inaendelea kupitia muundo wake upya ili kupunguza ukubwa, kuunganisha taasisi zinazofanya kazi zinazofanana na kuleta uwiano sawa wa stahili kwa watumishi wa umma serikalini.
“Huko nyuma, tumeshuhudia baadhi ya taasisi za Serikali zikijipangia stahili mbalimbali pamoja na mishahara, sasa hivi ni lazima kuomba kibali kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora” Mhe. Kairuki amesema na kusisitiza lengo ni kuwa na uwiano sawa.
Ameongeza kuwa Serikali ina nia nzuri na inaijali rasimaliwatu yake ambapo katika zoezi hili tathmini ya kazi inafanyika ili kila kada itendewe haki katika kupata stahili kulingana na majukumu yake.
Waziri Kairuki katika ziara yake amewataka watumishi kufanya kazi kwa ushirikiano na kuwasisitiza Maafisa Utumishi kuwasikiliza wateja wao, wakiwamo watumishi wenzao na kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na kuwaelemisha kuhusu nyaraka za kiutumishi.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment