CUF wadai sasa ameanza kuyumba.



Rais John Magufuli
Chama cha Wananchi (CUF), kimedai kuwa Rais John Magufuli ameanza kuigeuka kauli yake juu ya amani na utulivu wa kisiasa visiwani Zanzibar baada ya kudaihataingilia mgogoro uliopo kuhusiana na Uchaguzi Mkuu wa visiwa hivyo.
 
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui, alisema hayo visiwani Zanzibar jana wakati akitoa tamko la CUF kuhusiana na kauli aliyoitoa Rais Magufuli mbele ya wazeee wa jijini Dar es Salaam juzi.
 
Katika mkutano huo na wazee, Rais Magufuli alisema kamwe hataingilia mgogoro wa uchaguzi Zanzibar na badala yake anaiachia Tume ya Uchaguzi visiwani (ZEC) kuamua suala hilo kwa kuwa iko huru kama zilivyo tume zingine za aina hiyo duniani kote.
 
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la Vuga, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja jana, Mazrui alisema Rais Magufuli amewashangaza CUF kwa kuwa kauli yake imeanza kupingana na kile alichokieleza Novemba 20, 2015, kwenye hotuba yake ya uzinduzi wa  Bunge 11 mjini Dodoma.
 
“Rais Magufuli amejikanyaga na kujikanganya kwa kauli yake kwani wakati akizindua Bunge, alisema atalishughulikia tatizo la Zanzibar, lakini sasa anasema hawezi kuingilia mambo ya Zanzibar,” alisema Mazrui.
 
Aliongeza kuwa kuwa viongozi wa kitaifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaonyesha kuwa hawako tayari kushughulikia matatizo ya ndani ya nchi na badala yake wanachukua juhudi kubwa kushughulikia migogoro ya kisiasa katika Ukanda wa Maziwa Makuu na nchi zingine barani, zikiwamo za Burundi, Libya na viswa vya Comoro.
 
Mazrui alidai kuwa msimamo ulioonyeshwa na Rais Magufuli dhidi ya Zanzibar umewasikitisha kwa kuwa inashangaza kuona kuwa wanahangaikia kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya nje ya nchi huku wakipuuzia masuala ya ndani.
 
Akitoa mfano, alisema ni jambo la kushangaza kuona Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, akienda Libya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa nchi hiyo wakati Zanzibar iko katika mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa tangu Mweneyekiti wa ZEC, Jecha Salim Jecha, atangaze kufutwa kwa matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
 
Mazrui alisisitiza kuwa msimamo wa (CUF) bado uko pale pale, yaani kutoshiriki uchaguzi wa marudio kwa vile uliofanyika Oktoba 25 haukuwa na kasoro zozote kubwa kiasi cha kuufuta. Alisema ZEC inapaswa kuendelea na mchakato wa majumuisho ya kura na kumtangaza mshindi.
 
Kabla ya kufutwa kwa uchaguzi huo, mgombea wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad alidai kuwa anaelekea kushinda baada ya matokeo waliyokusanya kwenye vituo vyote vya uchaguzi kuonyesha kuwa anaongoza kwa zaidi ya asilimia 50 dhidi ya mpinzani wake, Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM.
 
Mazrui aliongeza kuwa uchaguzi wa Oktoba 25 ulikuwa huru na wa haki ndiyo maana ukasifiwa na waangalizi wote wa uchaguzi kutoka ndani na nje ya nchi, wakiwamo kutoka Umoja wa Afrika (AU), Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Madola.
 
Kadhalika, Mazrui alisema wagombea walioshinda kwa nafasi mbalimbali walikuwa tayari wamekabidhiwa vyeti vya ushindi na ZEC na pia matokeo yote yalishabandikwa katika kila jimbo.
 
Hivi karibuni, ZEC ilitangaza kuwa uchaguzi mkuu wa Zanzibar utarudiwa Machi 20, mwaka huu, baada ya ule wa awali kufutwa kutokana na madai ulitawaliwa na kasoro nyingi, hivyo kutokuwa ‘huru na wa haki’.
 
Juzi, wakati akizungumza na wazee wa mkoa wa Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema kamwe hataingilia mgogoro huo kwa kuwa ZEC ina uhuru wa kujiamulia mambo yake.
 
Magufuli alisema kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, ZEC ina uhuru wa kuendesha mambo yake bila ya kuingiliwa na hivyo, haoni sababu ya (yeye) kuingilia suala hilo.
 
Hata hivyo, aliwataka viongozi ambao wanaona tafsiri hiyo ya kuipa uhuru ZEC ni mbaya basi wakatafute tafsiri mahakamani na si kumshinikiza aingilie masuala ya Zanzibar.
 
Wakati huohuo, akizungumza jana, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Makungu, alisisitiza kuwa CUF hawakuwa na nia ya kwenda mahakamani na hivyo hawapaswi kuzungumzia kile alichokieleza kuhusiana na suala hilo.
 
Alisema CUF haikupaswa kumshangaa yeye bali Sheria ya Uchaguzi ambayo ndio inayosema ndani ya siku 14 ya kufutwa kwa uchaguzi ndipo mtu huwa na haki ya kuipinga tume hiyo kwa kwenda mahakamani.
 
ALICHOKISEMA MAGUFULI BUNGENI KUHUSU ZANZIBAR
Wakati akilihutubia Bunge Novemba 20, 2015, Rais Magufuli alisema kuwa daima atalinda Muungano wa Tanzania kwa kuwa licha ya kiapo chake wakati akiapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pia yeye ni muumini mzuri wa Muungano.
 
Ifuatayo ni sehemu ya hotuba yake (Magufuli) kuhusiana na Zanzibar, ikiwa ni kichwa cha habari kisemacho, ‘Kuimarisha Muungano’:
 
“Nilipoapa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, niliapa kuulinda Muungano wa nchi yetu. Hata bila kiapo, mimi ni muumini wa dhati wa Muungano wetu wa kipekee, uliounganisha nchi mbili zilizokuwa huru za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, tena kwa hiari na kwa wino wa kalamu, na si mtutu kama miungano mingine duniani. 
 
Naamini kwa dhati ya moyo wangu kuwa Muungano wetu ndio umoja wetu, amani yetu na salama yetu. Ninayo kila sababu ya kuulinda na kuuenzi Muungano wetu adhimu na adimu. Ni azma yangu kuwaona wananchi wa Zanzibar na Bara wakifurahia matunda ya Muungano wetu badala ya kuwa kikwazo kwa ustawi wao na ustawi wa nchi yetu. 
 
Aidha, kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa siasa hususan vyama vya CUF na CCM tutahakikisha kuwa majaribu ya kisiasa yanayoikabili Zanzibar yanamalizika kwa salama na amani. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujalie busara na hekima tumalize kwa utulivu na amani.” 
 
WACHAMBUZI WA SIASA WANENA 
Kauli ya Rais Magufuli kuwa hataingilia mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar imepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na wasomi. 
 
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Israel Sosthenes, alisema alichokitamka Rais Magufuli juzi ni sahihi kwa kuwa atakuwa amepewa ushauri mzuri. Alisema Rais Magufuli ataingilia suala la Zanzibar endapo ikitokea vurugu ama dalili ya uvunjifu wa amani.
 
“Rais Magufuli alitamka kauli hiyo akiwa sahihi na wala hakukosea. Wananchi wa Zanzibar hivi sasa hawako katika mazingira mazuri hivyo wanapaswa kusaidiwa,” alisema Sosthenes.
 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi, alisema Rais Magufuli ameteleza kwakauli hiyo aliyoitoa, alisema kwa sasa nchi iko katika utawala wa kidemokrasia, hivyo hakupaswa kutoa kauli ya vitisho.
 
Alisema Rais Magufuli akiwa bungeni akilihutunia bunge na kulifungua alihaidi ataushughulikia mgogoro wa Zanzibar kwa amani, alisema kukiuka kauli hiyo anapaswa kuwaomba radhi watanzania.
 
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Abdulkarim Atik, alisema Rais  amesimamia sheria ya uchaguzi ya Zanzibar na anayeona kasoro anatakiwa afuate sheria ndio msimamo wake na kusema amani ataisimamia na hilo ndiyo jukumu lake.
 
Alisema Rais Magufuli yuko sahihi kwa kauli hiyo lakini wakosoaji hawataacha kumpinga kwa sababu tatizo la Zanzibar siyo la kisheria pekee bali ndani yake ni kisiasa, kikatiba na kijamii.
 
Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema Rais Magufuli hawezi kukwepa kushughulikia mkwamo wa kisiasa uliopo Zanzibar kwa kuwa yeye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano, hivyo anahusika kuhakikisha anamaliza mkwamo huo.
 
Alisema Rais Magufuli akiwa kama Rais wa Jamhuri hawezi kukwepa kushughulikia hali ya kisiasa Zanzibar na kwamba anachopaswa ni kuhakikisha anachukua hatua stahiki kwa mamlaka aliyopewa kikatiba kuhakikisha umoja na amani ya taifa inaendelea kuimarika kwa kuzingatia misingi ya kidemokrasia.
 
Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini NCCR-Mageuzi, David Kafulila, alisema kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, kwa sasa Zanzibar haina Rais, na hata aliyeko madarakani hayupo kikatiba.
 
Alisema Rais Magufuli ndiye mwenye mamlaka kwa kuwa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Zanzibar na anapaswa kuiokoa Zanzibar.
 
Alisema endapo Zanzibar kutatokea machafuko, nchi za kimataifa zinaweza kuwa na uhusiano mbaya na Tanzania na hata kuweka vikwazo vya misaada.
 
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, alisema Rais Magufuli ametumia kisingizio kuwa ZEC ni huru wakati ilishaingiliwa katika kutoa uamuzi wa  kufuta uchaguzi.
 
Alisema Rais Magufuli amekwepa wajibu wake kama mkuu wa nchi na badala yake amejiandaa kutumia mabavu na kudhihirisha kuwa ameshindwa kushughulikia mgogoro wa Zanzibar.
 
*Imeandikwa na Mwinyi Sadallah, Rahma Suleiman, Zanzibar, Gwamaka Alipipi na Elizabeth Zaya, Dar
 
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment