Nkupamah media:
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imekuwa ikifuatilia kwa makini majadiliano
yanayoendelea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kufuatia video
iliyotumwa katika YouTube
https://www.youtube.com/watch?=iveX49WE7fw na
imekuwa ikisambazwa kupitia njia mbalimbali za habari ikimuonesha mtu
mmoja kutoka nchi jirani akisema kuwa Olduvai Gorge ambayo kimsingi iko
Tanzania kwamba iko Kenya.
Video hii imeibua majadiliano katika mitandao ya kijamii baina ya
watanzania na watu wengine ambao wanaitakia mema Tanzania na wanaoelewa
vizuri kuwa Olduvai Gorge iko Tanzania.
Bodi ya Utalii Tanzania kama taasisi ya Umma yenye jukumu la kuvitangaza
vivutio vyetu vya utalii imeshtushwa na video hii iliyojaa upotoshwaji
mkubwa ambao tunaamini mbali ya malengo mengine inalenga kuchafua kazi
nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Bodi kwa kushirikiana na wadau wengine
katika kutamgaza vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Olduvai Gorge.
Tunapenda kuchukua fursa hii kupinga vikali upotoshwaji huu uliofanywa
na mtu huyo wakati akihutubia mkutano ambao tumeambiwa ulikuwa ni wa
Vijana wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Amerika mwezi Agosti mwaka jana.
Tunapenda dunia ifahamu kuwa kama ilivyo kwa Mlima Kilimanjaro, Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti, Zanzibar n.k Olduvai Gorge mahali panapoaminika
kuwa ndipo binadamu wa kwanza duniani aliishi na ambako Dr. Louis na
Mary Leakey waligundua fuvu la binadamu huyo wa kale anayesadikiwa
kuishi miaka takribani milioni 2 iliyopita iko pia Tanzania na si mahali
pengine popote duniani. Eneo hili la Olduvai Gorge liko katika bonde la
ufa katikati ya bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
mkoani Manyara nchini Tanzania.
Tunatoa wito kwa watanzania mahali popote walipo kuendelea kuunga mkono
juhudi za Bodi ya Utalii Tanzania za kuitangaza Tanzania na vivutio
vyake vya Utalii kwa kujibu na kusahihisha papo hapo bila woga mara tu
taarifa ya upotoshaji kuhusu nchi yetu inapotolewa iwe ni kwenye
mikutano ya ndani ya nchi au ya Kimataifa.
Tunaamini kuwa ni jukumu la
kila mtanzania kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya Utalii badala ya
kuiachia TTB kazi hii peke yake.
Yawezekana katika mkutano huo wa vijana ambao mjumbe huyo wa nchi jirani
alipata fursa ya kuzungumza na kufanya upotoshaji huzo, wajumbe wa
Tanzania pia walikuwepo ambao wangweza kukosoa upotoshaji huo papo hapo
na kuelezea ukweli na usahihi wa mahali ilipo Olduvai Gorge.
Imetolewa na:
Ofisi ya Uhusiano
BODI YA UTALII TANZANIA
0 comments :
Post a Comment