Bodi
ya Utalii Tanzania (TTB) imekuwa ikifuatilia kwa makini majadiliano
yanayoendelea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kufuatia video
iliyotumwa katika YouTube https://www.youtube.com/watch?=iveX49WE7fw
na kusambazwa kupitia njia mbalimbali za habari ikimuonesha mtu mmoja
kutoka nchi jirani akisema kuwa Olduvai Gorge ambayo kimsingi iko Kenya.
Video hii imeibua majadiliano
katika mitandao ya kijamii baina ya watanzania na watu wengine ambao
wanaitakia mema Tanzania na wanaoelewa vizuri kuwa Oldupai Gorge iko
Tanzania.
Bodi ya Utalii Tanzania kama
taasisi ya Umma yenye jukumu la kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii
imeshtushwa na video hii iliyojaa upotoshwaji mkubwa ambao tunaamini
mbali ya malengo mengine inalenga kutia doa kazi nzuri ambayo imekuwa
ikifanywa na Bodi kwa kushirikiana na wadau wengine katika kutagaza
vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Oldupai Gorge.
Tunapenda kuchukua fursa hii
kupinga vikali upotoshwaji huu uliofanywa na mtu huyo wakati akihutubia
mkutano Newyork tumeambiwa ulikuwa ni wa Vijana wa Umoja wa Mataifa
uliofanyika Amerika mwezi Agosti mwaka jana. Tunapenda dunia ifahamu
kuwa kama ilivyo kwa Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
Zanzibar n.k kuwa Olduvai Gorge mahali panapoaminika kuwa ndipo binadamu
wa kwanza duniani aliishi na ambako Dr. Louis na Mary Leakey waligundua
fuvu la binadamu huyo wa kale anayesadikiwa kuishi miaka takribani
milioni 2 iliyopita iko pia Tanzania na si mahali pengine popote
duniani. Eneo hili la Olduvai Gorge liko katika bonde la ufa katikati ya
bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Arusha
nchini Tanzania.
Tunatoa wito kwa Watanzania
mahali popote walipo kuendelea kuunga mkono juhudi za Bodi ya Utalii
Tanzania za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya Utalii kwa kujibu
na kusahihisha papo hapo bila woga mara tu taarifa ya upotoshaji kuhusu
nchi yetu inapotolewa. Tunaamini kuwa ni jukumu la kila mtanzania
kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya Utalii.
Imetolewa na:
Ofisi ya Uhusiano
BODI YA UTALII TANZANIA
0 comments :
Post a Comment