Magufuli uso kwa uso na Nkurunziza, Museveni.

Nkupamah media:

Rais John Magufuli.
 
Rais John Magufuli, kwa mara ya kwanza atakutana na wakuu wenzake wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), katika mkutano wa 17 wa kawaida wa jumuiya hiyo, utakaofanyika jijini Arusha keshokutwa.
 
Rais Magufuli ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa jumuiya hiyo,  jana aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwa ajili ya kwenda Arusha kuhudhuria mkutano huo na kupata  mapokezi  makubwa, huku akiwashukuru wananchi, watendaji  na  viongozi kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea.
 
Aidha, Rais Magufuli aliwaomba viongozi hao na wananchi kuendelea kujitokeza  kuwapokea wageni wengine wakiwamo  marais wa nchi zote za Jumuiya ya Afrika  Mashariki wanaotarajiwa kuanza kuwasili leo kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo.
 
Marais wengine wa nchi wanachama wa EAC wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo ni, Yoweri Museveni wa Uganda, Pierre Nkurunzinza wa Burundi, Paul Kagame wa Rwanda na Uhuru Kenyatta wa Kenya.
 
RAIS NKURUNZINZA
Rais Nkurunziza atawasili nchini baada ya miezi 10 ya jaribio la kumpindua Mei mwaka jana.
 
Jaribio hilo lilitokea wakati Rais huyo wa Burundi akiwa jijini Dar es Salaam kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, mwaka jana wakati akiwa bado madarakani.
 
Mkutano huo ulikuwa na lengo la  kuzungumzia mvutano uliokuwapo kati ya Rais Nkurunziza na vyama vya upinzani nchini Burundi vilivyokuwa vikipinga asigombee urais kwa muhula wa tatu.
 
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano katika Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Othieno Owora, jana alithibitisha kuwa Rais Nkurunziza atakuwa miongoni mwama marais wa EAC watakaohudhuria mkutano huo.
 
“Wakuu wote wa nchi wanachama wa EAC wamethibitisha kuhudhuria mkutano huu,” alisema.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda, alithibitishakuwa Rais Nkurunziza atahudhuria mkutano huo.
 
RAIS MUSEVEN1
Rais Museveni atahudhuria mkutano huo wa viongozi wa EAC ikiwa ni mara ya kwanza na siku chache tangu alipochaguliwa kuongoza Uganda kwa muhula wa tano katika uchaguzi mkuu ulofanyika Februari 18, mwaka huu, ambao unalalamikiwa kuwa haikuwa huru na haki.
 
Akiwa kiwanjani hapo, Rais Magufuli, pia alitoa salama  za  pongezi  kwa  Chama  Cha Mapinduzi Mkoa wa  Arusha kwa kukamilisha uchaguzi wa viongozi wa  kuziba nafasi ya  mwenyekiti wa mkoa, katibu mwenezi na  mwenyekiti wa vijana,  zilizokuwa zimeachwa  wazi na waliohamia Chadema,  ambao katika uchaguzi  huo, Lekule Michael Laizer  amechaguliwa kuwa  mwenyekiti, Shabani  Mdoe (Katibu Mwenezi) na Lengai Olle Sabaya  akichaguliwa kuwa  mwenyekiti wa vijana. 
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini  Arusha jana, Waziri wa Mambo  ya Nje Ushirikiano wa  Afrika Mashariki, Kikanda  na Kimataifa, Balozi Dk. Agustine Mahiga, alisema  maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki yamekamilika na kwamba  kikao cha Baraza la  Mawaziri kinatarajiwa  kuanza leo jijini Arusha .
 
Alisema  akiwa Arusha, Rais  Magufuli ataongoza  viongozi wenzake katika  hafla ya kuweka jiwe la  msingi la ujenzi wa  barabara ya Arusha hadi  Holili kupitia Taveta na kwa siku mbili za mwanzo   atakuwa anaendelea na kazi zake nyingine ambazo  hakuzitaja.
 
Ziara ya Magufuli mkoani Arusha ni ya pili tangu achaguliwe  kuwa Rais na anatarajiwa kurejea  jijini  Dar es Salaam Machi 3, mwaka huu, ingawa Balozi Mahiga, alisema yanaweza pia yakawapo  mabadiliko.
 
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment