Pia kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima amesema Yanga itafanya vizuri na kwamba mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib ni wa
kawaida na asiye na madhara, huku mshambuliaji wa Azam FC, Didier Kavumbagu akiipa nafasi kubwa Simba kuibuka na ushindi kesho.
Simba imepiga kambi mkoani Morogoro katika eneo la Kigurunyembe, wakati Yanga yenyewe imejichimbia Chake Chake, Mkoa wa Kaskazini Pemba kujiandaa na mchezo huo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika kambi za timu hiyo umebaini ulinzi mkubwa katika mazoezi tofauti na mechi zilizopita, ambapo mashabiki wamekuwa wakizuiwa kushuhudia mazoezi hayo.
“Tunafanya mazoezi yetu kwa siri, hatuhitaji mashabiki ndiyo sababu tumeamua timu yetu kuificha eneo hilo kama alivyotaka kocha wetu,” ni kauli ya Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.
Manara akizungumza na gazeti hili juzi, alisema waliamua kuificha timu Morogoro na kuzuia mazoezi yao yasihudhuriwe na mashabiki kutokana na maombi ya kocha wao Jackson Mayanja, ingawa baadaye mashabiki wachache walipata fursa kuhudhuria mazoezi hayo.
Alisema Simba imeweka kambi kituo cha michezo cha Highlands cha Kanisa la Baptist Mission Morogoro ambacho ni cha kisasa eneo la Kigurunyembe.
Kwa upande wa Yanga yenyewe pia imekuwa na mkazo zaidi katika mchezo huo, ambao Kocha Mkuu, Hans Pluijm amesema wanauchukulia uzito mkubwa, lakini wanaomba waachwe wafanye maandalizi ya kuifunga Simba.
Pluijm alisema sababu ya kuweka kambi nje ya Dar es Salaam ni kupata muda wa kuelekeza nguvu zao kwa mchezo huo na kwamba hilo litafanikiwa kama hawatapata usumbufu wa aina yoyote.
Wakati huohuo, Niyonzima nahodha wa Yanga, amesema hadhani kama Ajib anaweza kuwa na madhara kwa Yanga na kwamba mashabiki wao wajitokeze kwa wingi kesho.
Niyonzima kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter aliandika jana kuwa haamini kama Simba ina wachezaji watakaowanyima raha mashabiki wa Yanga na kwamba hana wasiwasi na hilo hata kidogo.
Niyonzima ambaye ndiye nahodha wa Yanga kwa sasa baada ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuumia amepania kuonesha kiwango cha juu katika mchezo wa kesho ikiwa ni pamoja na kuisaidia timu yake kupata ushindi.
“Ukweli nimefurahi kurudi kuichezea timu yangu Yanga na kwa sasa nafanya mazoezi mara mbili kwa siku kwa ajili ya kujiweka fiti ili kocha aweze kunipanga kwenye kikosi kitakachocheza na Simba na nimedhamiria kufunga moja ya bao katika ushindi mnono wa siku hiyo,”alisema Niyonzima.
Kwa upande wake Kavumbagu, mchezaji wa zamani wa Yanga, ambaye sasa yupo Azam FC alisema anaipa nafasi kubwa Simba kushinda kutokana na matokeo iliyopata katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alisema wachezaji wa Simba wana ari, viongozi na hata mashabiki jambo ambalo katika mpira lina nafasi kubwa hasa wakati huu ambao timu yao itaingia uwanjani ikiwa inaongoza ligi hiyo.


0 comments :
Post a Comment