Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Profesa Jumanne Maghembe (MB) akisalimiana
na Mhifadhi Ashery Loishooki mara baada ya kuwasili katika eneo la
Nyasirori, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa ajili ya kuachia huru kundi
la sita la mbwa mwitu 11 waliokuwa wamehifadhiwa kwa miezi sita katika
boma maalumu la mradi wa mbwa mwitu.
Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Prof. Jumanne Maghembe (MB) akiongeawakati wa tukio la kuachia
huru kundi la sita la mbwa mwitu 11 waliokuwa wamehifadhiwa kwa miezi
sita kwenye boma maalumu la mradi wa mbwa mwitu.
………………………………………………………………………………………………………
Waziri wa Maliasili na Utalii
Profesa Jumanne Maghembe amepongeza jitihada zinazofanywa na watafiti
kwa kurudisha mbwa mwitu katika Hifadhi ya Taifa Serengeti baada ya
kutoweka katika miaka ya tisini. Waziri Maghembe alitoa pongezi hizo
mwishoni mwa wiki alipokuwa akiachia huru kundi la sita la mbwa 17
waliokuwa wamehifadhiwa katika boma maalum ili kurejea katika makazi yao
ya asili.
Profesa Maghembe amesema serikali
itaendelea kuwekeza katika eneo la utafiti ili kuwezesha sekta ya
uhifadhi nchini kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa. Alisema
mabadiliko ya tabia nchi yameathiri sekta nyingi ikiwemo ya uhifadhi na
kuwa wanyama wamekuwa wakiathirika na mabadiliko hayo hivyo ni vema
uwekezaji mkubwa ukafanyika katika eneo la utafiti ili kujua namna
ambavyo uhifadhi unaweza kukabiliana na mabadiliko hayo.
Mradi wa uhifadhi wa mbwa mwitu
unalenga kurudisha mbwa mwitu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambao
walitoweka kabisa tangu mwaka 1994 kwa sababu ambazo hadi leo
hazijaweza kubainika kisayansi. Mradi huu unasimamiwa na kuendeshwa na
watafiti wa kitanzania.
Tangu kuanza kwa mradi huu mwaka
2011, jumla ya makundi sita ya mbwa mwitu wamesharudishwa ndani ya
Hifadhi ya Serengeti. Makundi haya ni pamoja na Vodacom ambapo Kampuni
hii ya simu ilifadhili gharama za mradi; Serengeti; Loliondo; Kikwete;
Nyasirori na hili la mwisho ambalo lilipewa jina la Markus Borner,
mwanasayansi kutoka nchini Ujerumani aliyetumia miaka 35 akifanya
shughuli za uhifadhi katika hifadhi ya Serengeti.
Mradi wa mbwa mwitu Serengeti
unaendeshwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI), Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro, TANAPA na Chuo Kikuu cha Glasgow.


0 comments :
Post a Comment