WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
amesema katika kipindi cha wiki mbili atafanya `safisha safisha’ katika
baadhi ya taasisi zilizo chini ya wizara yake.
Amesema hatua hiyo inatokana na kutoridhishwa na utendaji wa baadhi
ya watendaji wake. Mbarawa alizitaja taasisi hizo kuwa
Wakala wa Majengo
(TBA), Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) na Kampuni ya Simu Tanzania
(TTCL) kutokana na taasisi hizo kuhujumiwa na watendaji wake wachache.
Alitoa kauli hiyo juzi wakati akizungumza na wafanyakazi mkoani
Simiyu na Shinyanga kwa nyakati tofauti kutoka taasisi na mashirika
yaliyoko chini ya wizara yake kwa viongozi wa chini kufanya kazi kwa
mazoea.
Kauli hiyo ilikuja baada ya waziri huyo kupokea malalamiko kutoka kwa
baadhi ya wafanyakazi wa taasisi hizo, ambao walidai kutolipwa fedha za
uhamisho, kutokupandishwa madaraja pamoja na wengine kufanyakazi kama
vibarua kwa muda wa zaidi ya miaka mitatu.
Alisema anatambua matatizo makubwa yanayowakabili wafanyakazi kutoka
Temesa, TTCL na TBA kwa kile alichoeleza kuwa viongozi wamefanya taasisi
hiyo kama sehemu ya kujinufaisha wenyewe.
“Matatizo yenu siyo mageni kwangu na wala sishangai kuyasikia...
lakini nawaomba ndani ya wiki moja au mbili nafanya zoezi kubwa la
safisha safisha kwenye mamlaka hizi kusema ukweli nachukia sana utendaji
wa taasisi hizi,” alisema Mbarawa.
Alisema Temesa wamekuwa wakipata kazi kubwa na nyingi za kutengeneza
magari ya serikali, ambapo alisema amekuwa akishangazwa kusikia wakala
huo hauna uwezo wa kujiendesha.
Kwa upande wa TTCL, alisema tayari amepata taarifa na anafahamu
kuwepo kwa baadhi ya wafanyakazi ndani ya shirika hilo wanaolihujumu
kupitia mashirika ya mawasiliano mengine ya binafsi yakiwamo ya simu za
mkononi.
Kuhusu TBA, alisema kuwa kasi ya utendaji wake imekuwa hairidhishi
kutokana na wakala huyo kushindwa kujiendesha licha ya kupata kazi
nyingi za ujenzi kutoka serikalini.
Katika ziara hiyo iliyokuwa ya kukagua miradi mbalimbali iliyoko
chini ya wizara yake ikiwemo barabara pamoja na kuzungumza na
wafanyakazi wake, aliwataka watendaji kuhakikisha wanafanya kazi kwa
ufanisi na ufasaha.
Alisema hatawavumilia watendaji wasio waadilifu, na wala rushwa.
Alizitaka taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, ikiwemo Tanroads kutumia
kwa njia sahihi fedha za umma, ikiwa pamoja na kuhakikisha zinakusanya
kodi kama inavyotakiwa kwa zile taasisi zinazojihusisha na ukusanyaji
kodi.


0 comments :
Post a Comment